MAANDAMANO YAMEZUKA ISRAEL BAADA YA WAZIRI MKUU NETANYAHU KUMFUTA KAZI WAZIRI WA ULINZI YOAV GALLANT



Maandamano makubwa yamezuka nchini Israel kufuatia uamuzi wa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, kumfuta kazi Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant. Netanyahu alisema kuwa "mgogoro wa uaminifu" kati yake na Gallant ndio ulisababisha kumvua wadhifa wake, akiongeza kuwa imani yake kwa Gallant "imepungua" katika miezi ya hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje, Israel Katz, anatarajiwa kuchukua nafasi ya Gallant kama Waziri wa Ulinzi.


Netanyahu alieleza kuwa, ingawa kumekuwa na ushirikiano mzuri katika miezi ya mwanzo ya vita vya Gaza, "katika miezi iliyopita, uaminifu huo umepungua." Aliongeza kuwa kulikuwa na "tofauti kubwa" kati yake na Gallant katika uendeshaji wa vita. "Haya yaliambatana na kauli na vitendo vinavyokinzana na maamuzi ya serikali," alisema Netanyahu.


Kufuatia uamuzi huo, Gallant alichapisha taarifa kupitia mitandao ya kijamii akisema: "Usalama wa taifa la Israel ulikuwa na utabaki daima kuwa ndio misheni ya maisha yangu." Gallant alikumbusha kuwa alikubaliana na msimamo wa kipaumbele cha kurudisha mateka wa Israel kutoka mikononi mwa Hamas, akiongeza kuwa "inawezekana kufikia lengo hili."


Katika taarifa yake, Gallant alieleza kuwa kuondolewa kwake kunatokana na "kutokubaliana katika masuala matatu," akisisitiza kuwa hakupaswi kuwepo kwa ubaguzi kujiunga na jeshi, uchunguzi wa kitaifa unahitajika, na mateka wanapaswa kurudishwa haraka iwezekanavyo.


Katika hali ya kisiasa, kuondolewa kwa Gallant kumekuja wakati ambapo Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wanasiasa wa mrengo wa kulia kupitisha mswada utakaoruhusu raia wa Israel wa Ultra Orthodox kutotumikia jeshi, jambo ambalo Gallant alikuwa mpinzani mkubwa.


Wanachama wa vyama vya upinzani vimeitisha maandamano ya umma kupinga uamuzi huo. Hali hii imeibua maswali kuhusu ushirikiano wa kisiasa kati ya Israel na Marekani, ambapo Gallant alionekana kuwa na uhusiano mzuri zaidi na Ikulu ya White House kuliko Netanyahu. Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani alisema: "Waziri Gallant amekuwa mshirika muhimu katika masuala yote yanayohusiana na ulinzi wa Israel. Kama washirika wa karibu, tutaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na waziri ajaye wa ulinzi wa Israel." 


Hali hii inakuja siku moja baada ya uchaguzi wa rais nchini Marekani, mfadhili mkuu wa Israel katika vita vyake vya Gaza, na inadhihirisha mgawanyiko mkubwa katika siasa za Israel wakati wa mgogoro wa Gaza.


0 Comments:

Post a Comment