Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanya hatua ya kihistoria kwa kugawa karatasi za mitihani (Rim paper) 800 kwa shule za msingi na sekondari, za serikali na binafsi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha sekta ya elimu na kupunguza mzigo kwa wazazi.
Hatua hii inakuja kama suluhu kwa changamoto ya fedha za ununuzi wa karatasi kwa ajili ya mitihani ya majaribio, ambayo imekuwa ikiwafanya wazazi kuchangia fedha kwa ajili ya mitihani mashuleni.
Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo, amesema kwamba hatua hii ni sehemu ya jitihada za halmashauri kuondoa adha hii na kuimarisha ubora wa elimu katika jiji hilo.
Kayombo, alisema halmashauri hiyo imeamua kulibeba jukumu la kugawa karatasi hizo ili kupunguza mzigo kwa wazazi.
“Kuanzia sasa ni marufuku kuwachangisha fedha na kuwatuma karatasi wanafunzi. Halmashauri imeamua kugawa karatasi hizi na kwamba suala hili litakuwa endelevu,” alisema Kayombo.
Aliongeza kuwa karatasi hizo zitumike kwa shughuli iliyokusudiwa, na aliahidi kwamba zoezi hili litaendelea kuendelea wakati wote atakapokuwepo katika utendaji wake katika jiji hilo.
“Ninaamini Walimu wote hawa ni waelewa na watazingatia maelekezo kama yalivyotolewa juu ya rim hizi.
Zoezi hili limefanyika kwa muda muafaka ambapo wanafunzi wanaelekea kufanya mitihani ya kumaliza mwaka,” alifafanua Mkurugenzi Kayombo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Jiji la Arusha, Peter Pantaleo, alisema msaada huo wa karatasi za mitihani utasaidia kupunguza gharama za michango ya ununuzi wa karatasi kwa ajili ya mazoezi na mitihani mashuleni.
“Msaada huu utasaidia kumpunguzia mzazi gharama za michango ya ununuzi wa karatasi kwa ajili ya kufanya mazoezi pamoja na mitihani mashuleni,” alisema Pantaleo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Msingi (TAPSHA) Halmashauri ya Jiji la Arusha, Peter Malealle, alitoa shukrani kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa mwezi uliopita.
“Tunamshukuru Mkurugenzi wetu ametekeleza ahadi yake aliyoahidi mwezi uliopita ili kufanya elimu yetu kuwa na tija, na tunaahidi kutendea kazi,” alisema Malealle.
Aidha, Mwakilishi wa Walimu, Yusta Njau, alimpongeza Mkurugenzi kwa hatua hiyo ya kuwapunguzia mzigo wazazi na kuwataka wanafunzi kuongeza jitihada katika masomo yao ili kuunga mkono juhudi za Mkurugenzi katika kuboresha sekta ya elimu.
"Tunampongeza Mkurugenzi kwa hatua hii ya kuwapunguzia wazazi mzigo na tunawaomba wanafunzi kuongeza jitihada ili kuunga mkono juhudi hizi,” alisisitiza Njau.
Hatua hii ya Halmashauri ya Jiji la Arusha inakuja ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha elimu na kupunguza changamoto zinazowakabili wazazi na wanafunzi, hasa katika kipindi hiki cha mitihani ya kumaliza mwaka.
0 Comments:
Post a Comment