Dk. Ndugulile Afariki Dunia Akiwa na Miaka 55

 



Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mkuu mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 55.  



Taarifa za kifo chake zimetangazwa leo na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Bunge. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Ndugulile alikuwa nchini India kwa matibabu wakati wa kifo chake.  


“Ofisi ya Bunge itashirikiana na familia ya marehemu kuratibu zoezi zima la mazishi,” imesema sehemu ya taarifa ya Dk. Tulia ambayo hata hivyo haikueleza chanzo cha kifo cha kiongozi huyo.  


Dk. Ndugulile alichaguliwa Agosti 27 mwaka huu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika, nafasi ambayo alitarajiwa kuanza kuitumikia rasmi mwaka 2025.  


Rais Samia atuma salamu za rambirambi  

Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza Watanzania katika kuomboleza kifo cha Dk. Ndugulile kwa kutuma salamu za rambirambi kwa familia yake na Taifa kwa ujumla.  


“Ninatoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote,” ameandika Rais Samia.  


Ameongeza kuwa, “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za msiba wa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mkuu mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.”  


Kifo cha Dk. Ndugulile kimeacha simanzi kubwa miongoni mwa Watanzania, hasa wananchi wa Kigamboni alikohudumu kama Mbunge, na wale waliokuwa wakimtarajia kwa matumaini makubwa katika wadhifa wake mpya wa kimataifa.

0 Comments:

Post a Comment