Askofu Bagonza Aomboleza Kifo cha Rais Mwinyi kwa kueleza milima na maponde aliyopitia Aliwaheshimu Marais Wote Bila Kujali Kama Wanapingana Amedumisha Muungano Amefia Bara Kazikwa Zanzibar

 Askofu Bagonza Aomboleza Kifo cha Rais Mwinyi kwa kueleza milima na maponde aliyopitia 

Aliwaheshimu Marais Wote Bila Kujali Kama Wanapingana

Amedumisha Muungano Amefia Bara Kazikwa Zanzibar.




Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ameondoka. Umri wa karne moja umetimia ukihesabu na muda wa mimba yake. Ndo maana tunazuia utoaji mimba kwa sababu anakuwa ni mtu yule! Kwa heri Mzee Ruksa. Nimemtafakari:


1. Alionja furaha na ghadhabu ya Kambarage. Wengine wanamsikia Kambarage. Mwinyi alikabidhiwa nchi ikiwa hoi lakini hakuwa huru kusema kuwa nchi ni hoi. Kimya kimya akaingia kazini na kiranja akiwa Butiama. Ukikooa Ikulu anasikia.


2. Alipojaribu kuanza mageuzi, alikumbana vikwazo ndani na nje. Kwa ndani kikubwa kilikuwa Kambarage. Nje IMF na World Bank. Alikemewa kama mtoto na kutungiwa kitabu na akatii. Si kawaida mwenye rungu kumfokea mwenye bunduki. Ilitokea na maisha yakaendelea.


3. Tukiwa wanafunzi vyuo vikuu, tukapimana vifua na Mzee Mwinyi. Tukagoma na kuandamana. “Punch” akampunch rais na kusababisha kifo cha punch.  Vyuo vikafungwa, tukauza blanketi kupata nauli ya kwenda nyumbani. Wengine hawakurudi mpaka leo. Tunamtamani Punch lakini hatorudi. Mzee Mwinyi msalimie Punch huko uendako.


4. Mwinyi alizima ndoto za wengi. Kabla yake hakuna aliyedhani wala kuota kama kuna Tanzania bila Kambarage. Ikawezekana. Kwa uungwana wake akagawa madaraka: Sehemu akawa nayo Kambarage; nyingine akampa Mrema; na nyingine Mama Sitti. Tukavuka.


5. Ameishi na maraisi wote waliowahi kutuongoza. Hata walipotofautiana, aliwaheshimu na kuwasifia wote. Akamlinganisha Kambarage na Mlima Kilimanjaro na yeye ati, ni kama kichuguu. Akampokea bila kinyongo Ben Mkapa hata kama hakumtegemea awe mrithi wake. Alimpenda JK kuliko hata JK alivyojipenda. Akamsifia JPM kuwa amefanya makubwa kuliko wote waliomtangulia wakijumlishwa pamoja! Akachombeza “kwa nia njema” kuwa katiba itazamwe ili JPM aendelee. Alimpenda sana SSH mpaka akachombeza “mwanamke aliyekuzidi kwa shughuli hata kwa kimo, ni mama yako huyo”.


6. Rais Mwinyi aliingia madarakani akibebwa na historia ya kuwajibika pale watendaji walio chini yake wanapofanya makosa. Tangu hapo hajaonekana mwingine. Waliofuata walijiuzuru kwa makosa yao. Sijui kwa kifo chake, na tabia hiyo njema tunaizika rasmi?


7. Rais Mwinyi aliutikisa na kuuimarisha Muungano kwa namna yake. Alizaliwa Tanganyika. Akakulia Zanzibar. Akatumikia wizara za hayati Tanganyika. Akawa rais wa Zanzibar. Akawa rais wa Muungano. Akaishi bara kama mstaafu. Akafia bara. Akazikwa Zanzibar. Angekuwa Mkiristo tungesema atafufukia alipofia - Bara!

Rais Mwinyi si kero ya Muungano bali changamoto ya Muungano.


8. Kwa wasiopenda Muungano, aliwatendea haki wote. Akiwa rais wa Zanzibar alionekana mkoloni wa bara anayetawala Zanzibar. Alipokuwa rais wa Muungano, alionekana mkoloni kutoka Zanzibar akiwatawala Watanganyika waliovaa koti la Muungano. Nchi mbili ziliungana, zikabakia mbili. Asiyeelewa amfufue Kambarage amweleweshe.


9. Alishika dini ikamshika. Hata alipozabwa kibao kwa msimamo wake wa dini, hakuacha dini. Kwa wahafidhina alikuwa mhafidhina. Kwa waliberali alicheka nao kama wenzake. Ulipomchukia ulijishangaa kabla hajakushangaa. Aliruhusu kila kitu isipokuwa KUTORUHUSU.


10. Siku moja nilikutana naye Maji ya Chai, Usa River. Ilikuwa awamu ya 5. Nikamwuliza, inakuwaje mzazi muungwana na mpole anazaa mtoto mkali na mbabe? Akaniuliza, kwenu hawapo hao? Nikasema wapo, “lakini ukiwashtaki kwa baba zao ambao ni wapole, hutulia na kuwa waungwana”. Nikaendelea, “tuna baba mkali mno huko Ikulu, na wewe ni Babu yetu, kamwonye atulie basi”. Alichekaaa, nikaogopa. Kisha akaniambia, nimekusikia Baba Askofu.


Pumzika kwa Amani Mzee wetu. Ulianza kutuongoza wakati wa uhaba wa kila kitu. Umeondoka wakati wa uhaba wa sukari, umeme na FURAHA.

0 Comments:

Post a Comment