Showing posts with label Mwinyi. Show all posts
Showing posts with label Mwinyi. Show all posts

 Samia; Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi Kama 'Maktaba Inayotembea' 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hussein Ali Mwinyi wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hayati Rais Mstaafu Dkt Ali Hassan Mwinyi muda mfupi kabla hajazikwa visiwani Zanzibar 
Samia Suluhu, ikiwa ya kumuaga Hayati Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Rais staafu wa awamu ya 
Wake wa Hayati Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi,  Bibi Siti Mwinyi na Khadija Mwinyi / Picha : Ikulu Tanzania



Viongozi waliohudhuria mazishi ya Hayati ALi Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu y apili Zanzibar /Picha: Ikulu Tanznaia 

Samia Suluhu Hassan amesifu kumbukumbu ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wakati wa mazishi yake huko Zanzibar, akimtaja kuwa "maktaba inayotembea na inayosheheni vitabu vyenye mafunzo ya uadilifu na uzalendo." 

Alimkumbuka kama kigingi kilichosimama kukuza na kulea maendeleo ya nchi, na kuongeza kuwa licha ya changamoto alizokumbana nazo, aliweza kuliongoza taifa kwa uadilifu na mafanikio makubwa.


Rais Samia pia alimulika uongozi wa Marehemu Mwinyi katika kusukuma ajenda ya haki za binadamu na uongozi bora, pamoja na kuhimiza uhuru wa uandishi.


Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar, aliwaomba Watanzania washikilie kauli ya hayati Dkt Mwinyi ya kusuluhisha nyoyo za wananchi, akisema maendeleo yanahitaji amani na utulivu. 


Hayati Rais Mstaafu Dkt Ali Hassan Mwinyi, ambaye alikuwa Mtanzania wa kwanza kuwa rais wa Zanzibar kisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anasifiwa kwa kuzipa nguvu taasisi za kiraia na kusimamia mageuzi ya kisasa, ikiwa ni pamoja na kurudisha mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 baada ya kufutwa mwaka 1965.



  MWINYI ALIENDAJE ZANZIBAR?:





Baba yake,  alitaka awe mwanazuoni wa Kiislamu, akampeleka  Unguja akasome madrasa. Alimuacha kwa rafiki yake anaitwa Suwedi Bin Mgeni. Maisha hapo nyumbani kwa Mgeni hayakuwa rahisi kwa sababu mke wa Swedi Mgeni hakukubaliana na suala la Ali kuwa hapo kwake, hivyo akamgeuza kijakazi, akiosha vyombo, kuteka maji na kazi nyingine za kwa kiwango kisichomfaa mtoto. Lakini  kwa mapenzi makubwa ya Swedi Mgeni, Ali aenda shule , akawa mwalimu na baadae kuingi kwenye uongozi hata kuwa Rais.


UWAZIRI: Mwaka 1970, Ali aliteuliwa kuwa Waziri, 1972 akawa Waziri wa Afya, 1975 akawa Waziri wa Mambo ya Ndani. 1977 yalitokea mauwaji ya kutisha huko Shinyanga na Mwanza, jambo ambalo lilimfanya Ali aamue kujiuzulu (aliona yeye kama Waziri wa Mambo ya Ndani alipaswa kuwajibika). 1978 akawa Balozi huko Misri, 1981 akarudishwa kwenye Uwaziri (Maliasli na Utalii na Baadae Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais).


URAIS WA ZNZ: Januari 1982, #Mwinyi alialikwa kwenye kikao cha CCM huko Dodoma, hakuwa Mjumbe wa Kamati Kuu. Alikosa sehemu nzuri ya kulala kulingana na cheo cha Uwaziri na Ujumba wa NEC, akishia kulala kwenye vyumba vya Wanafunzi pale CBE.

.

Kwenye mkutano kikawaka (mjadala ulikuwa kuhusu Muungano/ Serikali tatu). Wajumbe toka Zanzibar wakagawanyika kwenye Makundi: Wakombozi/Walinzi wa Mapinduzi na Frontliners (Mwinyi hakuwa kwenye kundi lolote). Hao Frontliners ndio walishinikiza kujiuzulu kwa Rais wa Zanzibar wa wakati huo (Alhaj Aboud Jumbe aliyefariki 2016). Januari 29,1982 Jumbe akajiuzulu, swali kubwa likawa nani atakuwa Rais wa #Zanzibar?.


Mwinyi hakutegemea kuwa Rais, watu walipendekeza jina lake. Baada ya mjadala mkali wa majina (kukaimu Urais), Mwalimu Nyerere akatafuta mtu mmoja kumaliza mjadala. Nyerere alimuamini sana Shekhe Thabiti Kombo, wakati wa mkutano Kombo alikuwa amelazwa KCMC Moshi. Nyerere akamtumia ndege aje Dodoma, akamuomba ashauri nani akaimu Urais, Thabiti Kombo akasema “ Twende na #AliHassanMwinyi”. Mwinyi akakaimu Urais.


Machi 10 1984, NEC ikakaa kujadili majina kwa ajili ya uchaguzi maalum, majina yalikuwa mawili tu: Shekhe Idriss Abdulwakil na Mzee Mwinyi. Shekhe Abdulwakil akaomba jina lake liondolewe, Mwinyi akabaki na ndio akawa Rais Wa Zanzibar hadi mwaka 1985.


Jina la #MzeeRuksa lilianzia pale. Mwinyi alipandisha mishahara ya wafanyakazi wa Zanzibar, sekt binafsi ikaruhusiwa kuingiza chakula Zanzibar, kukawa na usafiri rahisi kwa umma (zile Chai Maharage zilianzia hapo), na ruksa nyingine kibao).


URAIS WA TANZANIA: 1985 Mwalimu Nyerere alimua kung’atuka madarakani. Kulikuwa na majina matatu: Mwinyi, Dkt Salim Ahmed Salim (chaguo namba 1 la Mwalimu Nyerere) na Mzee Rashid Kawawa. 


Kawawa alijiweka pembeni, Dkt Salim Ahmed Salim akakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wajumbe wa Zanzibar. Mwinyi akaja kushinda na kuwa Rais wa Awamu ya Pili wa JMT.


NYERERE ALIMPINGA?: Ni kweli kwamba Mzee Mwinyi hakuwa chaguo ka kwanza la Nyerere (hii kaeleza Mwinyi mwenyewe), lakini hakumkataa. Mwinyi anasema Nyerere angeamua kuzuia Mwinyi asiwe Rais angeweza, hasa kwa kutumia kofia yake kama Mwenyekiti wa CCM, na nguvu yake ya ushawishi. Kwa ufupi Nyerere alikuwa na chaguo lake, lakini alikubaliana na mawazo ya wengi. Alimnadi Mwinyi kwenye uchaguzi, alimpa ushirikiano katika uongozi wake (Kuna  nyakati walitofautiana kimtazamo, mfano kwenye mtazamo juu mauwaji ya Rwanda, na mwaka 1994 hotuba ya Mwalimu Nyerere kwenye siku ya Wafanyakazi huko Mbeya).


Kuelezea heshima yake kwa Nyerere, Mwinyi anasema; huwezi kufananizha Mlima Kilimanajaro na kichuguu, kama wangeshindanishwa, Mwinyi alijiona kuwa kichuguu mbele ya Mlima Kilimanjaro.


Mwinyi ni muungwana asiye na makuu, mfano halisi wa kuinuliwa toka mavumbini kwenda juu sana. 


Habari kwa msaada wa mitandao ya kijamii 

 Askofu Bagonza Aomboleza Kifo cha Rais Mwinyi kwa kueleza milima na maponde aliyopitia 

Aliwaheshimu Marais Wote Bila Kujali Kama Wanapingana

Amedumisha Muungano Amefia Bara Kazikwa Zanzibar.




Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ameondoka. Umri wa karne moja umetimia ukihesabu na muda wa mimba yake. Ndo maana tunazuia utoaji mimba kwa sababu anakuwa ni mtu yule! Kwa heri Mzee Ruksa. Nimemtafakari:


1. Alionja furaha na ghadhabu ya Kambarage. Wengine wanamsikia Kambarage. Mwinyi alikabidhiwa nchi ikiwa hoi lakini hakuwa huru kusema kuwa nchi ni hoi. Kimya kimya akaingia kazini na kiranja akiwa Butiama. Ukikooa Ikulu anasikia.


2. Alipojaribu kuanza mageuzi, alikumbana vikwazo ndani na nje. Kwa ndani kikubwa kilikuwa Kambarage. Nje IMF na World Bank. Alikemewa kama mtoto na kutungiwa kitabu na akatii. Si kawaida mwenye rungu kumfokea mwenye bunduki. Ilitokea na maisha yakaendelea.


3. Tukiwa wanafunzi vyuo vikuu, tukapimana vifua na Mzee Mwinyi. Tukagoma na kuandamana. “Punch” akampunch rais na kusababisha kifo cha punch.  Vyuo vikafungwa, tukauza blanketi kupata nauli ya kwenda nyumbani. Wengine hawakurudi mpaka leo. Tunamtamani Punch lakini hatorudi. Mzee Mwinyi msalimie Punch huko uendako.


4. Mwinyi alizima ndoto za wengi. Kabla yake hakuna aliyedhani wala kuota kama kuna Tanzania bila Kambarage. Ikawezekana. Kwa uungwana wake akagawa madaraka: Sehemu akawa nayo Kambarage; nyingine akampa Mrema; na nyingine Mama Sitti. Tukavuka.


5. Ameishi na maraisi wote waliowahi kutuongoza. Hata walipotofautiana, aliwaheshimu na kuwasifia wote. Akamlinganisha Kambarage na Mlima Kilimanjaro na yeye ati, ni kama kichuguu. Akampokea bila kinyongo Ben Mkapa hata kama hakumtegemea awe mrithi wake. Alimpenda JK kuliko hata JK alivyojipenda. Akamsifia JPM kuwa amefanya makubwa kuliko wote waliomtangulia wakijumlishwa pamoja! Akachombeza “kwa nia njema” kuwa katiba itazamwe ili JPM aendelee. Alimpenda sana SSH mpaka akachombeza “mwanamke aliyekuzidi kwa shughuli hata kwa kimo, ni mama yako huyo”.


6. Rais Mwinyi aliingia madarakani akibebwa na historia ya kuwajibika pale watendaji walio chini yake wanapofanya makosa. Tangu hapo hajaonekana mwingine. Waliofuata walijiuzuru kwa makosa yao. Sijui kwa kifo chake, na tabia hiyo njema tunaizika rasmi?


7. Rais Mwinyi aliutikisa na kuuimarisha Muungano kwa namna yake. Alizaliwa Tanganyika. Akakulia Zanzibar. Akatumikia wizara za hayati Tanganyika. Akawa rais wa Zanzibar. Akawa rais wa Muungano. Akaishi bara kama mstaafu. Akafia bara. Akazikwa Zanzibar. Angekuwa Mkiristo tungesema atafufukia alipofia - Bara!

Rais Mwinyi si kero ya Muungano bali changamoto ya Muungano.


8. Kwa wasiopenda Muungano, aliwatendea haki wote. Akiwa rais wa Zanzibar alionekana mkoloni wa bara anayetawala Zanzibar. Alipokuwa rais wa Muungano, alionekana mkoloni kutoka Zanzibar akiwatawala Watanganyika waliovaa koti la Muungano. Nchi mbili ziliungana, zikabakia mbili. Asiyeelewa amfufue Kambarage amweleweshe.


9. Alishika dini ikamshika. Hata alipozabwa kibao kwa msimamo wake wa dini, hakuacha dini. Kwa wahafidhina alikuwa mhafidhina. Kwa waliberali alicheka nao kama wenzake. Ulipomchukia ulijishangaa kabla hajakushangaa. Aliruhusu kila kitu isipokuwa KUTORUHUSU.


10. Siku moja nilikutana naye Maji ya Chai, Usa River. Ilikuwa awamu ya 5. Nikamwuliza, inakuwaje mzazi muungwana na mpole anazaa mtoto mkali na mbabe? Akaniuliza, kwenu hawapo hao? Nikasema wapo, “lakini ukiwashtaki kwa baba zao ambao ni wapole, hutulia na kuwa waungwana”. Nikaendelea, “tuna baba mkali mno huko Ikulu, na wewe ni Babu yetu, kamwonye atulie basi”. Alichekaaa, nikaogopa. Kisha akaniambia, nimekusikia Baba Askofu.


Pumzika kwa Amani Mzee wetu. Ulianza kutuongoza wakati wa uhaba wa kila kitu. Umeondoka wakati wa uhaba wa sukari, umeme na FURAHA.

RAIS MSTAAFU MWINYI AFARIKI: SAMIA AELEZA KILICHOSABABISHA KIFO CHAKE:ATANGAZA SIKU SABA ZA MAOMBOLEZO




RAIS Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia leo Februati 29,2024 wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.


Rais Samia Suluhu Hassan  amelitangazia Taifa kuwa Rais Mstaafu Mwinyi alikuwa akisumbuliwa na saratani ya mapafu.




HISTORIA 

Hayati Rais Mstaafu Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa alikuwa kiongozi shupavu wa kisiasa na rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Alizaliwa tarehe 5 Mei 1925 huko Kivule, Mkuranga, mkoa wa Pwani. Mwinyi alianza kazi yake kama mwalimu wa shule za msingi za Mangapwani na Bumbwini, Zanzibar, kabla ya kujihusisha kikamilifu na siasa.


Akiwa mwanachama wa chama cha Afro Shiraz (ASP), alishika nyadhifa muhimu serikalini, ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Zanzibar, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Afya, Maliasili, na Balozi wa Tanzania nchini Misri.


Elimu yake ilikuwa muhimu katika kujenga msingi wa uongozi wake. Alihitimu cheti cha umahiri wa lugha ya Kiingereza huko Uingereza mwaka 1960 na cha umahiri wa lugha ya Kiarabu huko Cairo, Misri, kati ya mwaka 1972 na 1974.


Mwaka 1984, Alhaj Ali Hassan Mwinyi alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alikuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia tarehe 5 Novemba 1985 hadi 23 Novemba 1995. Uongozi wake ulijulikana kwa sera zake za kuleta maelewano na utulivu ndani na nje ya nchi, pamoja na kufanya mabadiliko kadhaa ya kiuchumi na kisiasa.


Baada ya kuondoka madarakani, Mwinyi alibaki kama kiongozi anayeheshimika na aliendelea kuchangia katika maendeleo ya nchi yake kwa njia mbalimbali. Alifariki dunia tarehe 8 Agosti 2020, akiacha nyuma yake urithi wa uongozi thabiti na jitihada za kuendeleza maendeleo ya Tanzania.