MAWAKILI WASHANGAZWA EACJ KUTUPA RUFAA YA WANANCHI LOLIONDO

 




Na Grace Macha, Arusha

MAWAKILI wa wananchi wa Tarafa ya Loliondo wameelezea kusikitishwa kwa namna maombi yao ya msingi yalivyotupwa kwenye mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki,(EACJ) ambayo ilitoa uamuzi huo kwa mdomo huku ikiahidi kutoa uamuzi wa maandishi uliosainiwa baada ya siku 15.

Mawakilil hao na wateja hao walifika mahakamani hapo kupokea uamuzi juu ya pingamizi lililowekwa na mawakili wa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania,(AG) lakini badala yake mahakama hiyo ikaamua kutoa uamuzi juu ya shauri lao la msingi kuwa limetupwa bila kueleza zaidi.


Uamuzi huo ulitolewa na majaji watatu wa mahakama hiyo leo Novemba 15, 2023 wakiongozwa na Jaji Charles Nyachae ambapo uamuzi wa maandishi uliosainiwa walisema utatolewa Novemba 30,2023.

Maombi yao ya msingi yalikuwa kuieleza mahakama kuwa kuna dalili za kuvunjwa kwa amri ya mahakama hiyo ya mwaka 2018  iliyotaka serikali ya Tanzania na taasisi zake zisifanye jambo lolote kwenye ardhi ya vijiji 15 vya tarafa ya Loliondo mpaka uamuzi itakapotolewa.


Mawakili wa wanachi hao, wanaoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Wanasheria Afrika, (PALU) Donald Deya walisema kuwa walifika mahakamani kupokea uamuzi wa mahakama juu ya pingamizi za awali lililowekwa na mawakili wa mwanasheria Mkuu wa Tanzania,(AG) kwenye kikao cha mahakama hiyo kilichokaa Kampala nchini Uganda, Novemba 2022.




"Cha kushangaza ni kwamba badala ya kutoa uamuzi juu ya pingamizi hizo mahakama imetoa uamuzi juu ya maombi yetu juu ya kudharauliwa kwa amri ya mahakama," alieleza Deya kwa masikitiko na  kuongeza


"Kwa kweli tumesikitika sana ila hatuwezi kusema chochote tunasubiri ule uamuzi dhahiri ili tujue tunafanyaje ikiwemo kuona kama tutakata rufaa kwenye mahakama ya juu ya Afrika Mashariki,".


Awali shauri hilo lilifunguliwa mwaka 2017 ambapo mwaka unaofuata 2018 mahakama ili ilitoa amri kwa serikali ya Tanzania na taasisi zake wasiguse wala kufanya jambo lolote kwenye eneo la vijiji 15 vya tarafa ya Loliondo mpaka shauri lao limalizike mahakamani.

"Wasisumbue jamii kwenye maeneo yao mpaka kesi imalizike kusikilizwa mahakamani. Mwaka jana januari tuliona maafisa wa serikali wakizungumza na kuanza kufanya maandalizi ikiashiria watakiuka amri hiyo ya mahakama," alisema Deya kuongeza


"Tuliamua kurejea mahakamani (EACJ) kusema kuwa amri mliyotoa kutaka kitu kisiguswe ni kama itakiukwa. Mahakama ilisema itatusikiliza na kweli amri ya mahakama ilikiukwa kuanzia mwezi Juni mwaka jana  mpaka Novemba mwaka huu,".

"Hili ni suala kuheshimu amri ya mahakama, mahakama haitakuwa na maana kama inatoa amri na watu wanaamua kwamba wataitii au hawataitii,".

"Suala kwamba ujumbe watalipeleka kwa wananchi ni kwamba mahakama haina kazi na wananchi wakishajua kwamba mahakama haina kazi na haiwezi kuwasaidia inamaanisha wachue mambo yao kwa mkononi na hiyo sii sehemu au jumuiya tuliyoamua kuwa nayo,".

"Ni muhimu sana kwamba kila Mahakama ikahakikisha amri zake zinatiiwa vinginevyo watu watajilinda wenyewe 
Hatujaridhika tumesikitishwa lakini tutasubiri tuona maamuzi yote waliyoyaandika,".


Wakati shauri hilo likisubiriwa kufanyiwa uamuzi mwezi Juni, 2022 serikali ya Tanzania iliweka mipaka kwenye eneo la pori la Loliondo na la zaidi ya kilometa za mraba 1,500 ambazo walililipandisha hadhi na kuwa pori Pololeti huku wananchi wakiachiwa kilimeta za mraba 2,500.

Baadaye mwezi Oktoba 2022, Rais alipandisha hadhi eneo hilo kuwa poli la akiba la Pololeti.

Rejea ya taarifa nyingine kuhusu shauri hili gusa link

https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2023/02/appeal-by-evicted-loliondo-herders-set.html


https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2023/02/rufaa-ya-wananchi-wa-loliondo.html

https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2022/01/ngorongoro-herders-file-second-stop.html


0 Comments:

Post a Comment