Matinyi Afungua Kikao Kazi cha Mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji


Mnamo tarehe 30 Oktoba 2023, jijini Morogoro, Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Mobhare Matinyi, alifungua kikao kazi cha mapitio ya Sera ya Taifa ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003. Kikao hicho kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kupitia Habari (MAELEZO), kilikusudia kufanya marekebisho na kuboresha sera hiyo ili iendane na mifumo ya kisheria, kiteknolojia na viwango vya kimataifa vya habari na utangazaji.


Lengo la kikao hiki cha kitaalamu kilichohudhuriwa na wataalamu wa sekta mbalimbali ni kufanya tathmini ya sera ili kuboresha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia. Kwa mujibu wa Matinyi, mapitio haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha tasnia ya habari inakwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya sasa.


Malengo muhimu ya kikao hiki ni kufanya tathmini ya athari za sera kwa uhuru wa vyombo vya habari na ubora wa habari, kuchambua maeneo ya kuboresha sera kwa ujumuishaji, ufikiaji wa kidijitali na uhifadhi wa kitamaduni, pamoja na kuhakikisha kanuni bora za kimataifa na viwango vya haki za binadamu vinazingatiwa.


Wakati akitoa shukrani zake, Matinyi aliwashukuru UNESCO kwa ushirikiano wao na Idara ya Habari, na kuonyesha matarajio yao kwa ushirikiano huo kuendelea katika hatua zinazofuata.


 Alisisitiza kuwa mapitio ya sera hii ni msingi wa kuhakikisha upatikanaji wa habari sahihi na kukuza maadili ya kidemokrasia na haki za binadamu.



Mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya habari, huku Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiazimia kuendelea kuleta maendeleo kwa kasi, kukuza uchumi na kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari.


Baada ya maboresho, inatarajiwa kwamba Sera mpya itakayopatikana itaimarisha upatikanaji wa habari sahihi kwa umma, ikizingatia mabadiliko ya kiteknolojia, masuala ya usalama wa kidijitali na malengo ya maendeleo endelevu.


Kikao hicho ni hatua muhimu katika safari ya kuwa na sera bora itakayowezesha upatikanaji wa habari zenye ukweli na uhalali kwa umma, na vilevile kuendelea kudumisha maadili ya kidemokrasia na haki za binadamu. 


Hatua hii inalenga kuhakikisha tasnia ya habari inakuwa shirikishi, inayowiana na mabadiliko ya kisasa, na inayokwenda sambamba na malengo ya maendeleo ya taifa

0 Comments:

Post a Comment