MAJALIWA ACHARUKA, AZISHUKIA KAMPUNI BINAFSI ZA UPIMAJI ARDHI

 


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa kampuni zote zilizopewa jukumu la upimaji wa viwanja katika Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba au hazikuwa nayo, zichukuliwe hatua kali za kisheria.


"Watumie makampuni yenye uaminifu badala ya kutumia makampuni yanayotuletea migogoro," alisema Waziri Mkuu.


Agizo hili limekuja baada ya kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, ambapo viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma walijadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.


"Kampuni nyingi hapa Dodoma zina watumishi wake wenyewe wakiwa ni sehemu ya mradi. Hatutaki hili liendelee," alisema.


Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha Kamishna Msaidizi wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa wanafanya kazi ya upimaji wenyewe bila kuchukua watumishi wa muda ili kuepusha mianya ya rushwa.


Pia, aliagiza kukamatwa kwa vibarua wanaotembea na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa Jiji.


"Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazotumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji la Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama."


"Hawa ni vibarua, lakini wanavijua viwanja vyote na wanafanya mauzo na kisha kuzipeleka hati kwa watu wao pale Jiji. Watafutwe na nyaraka hizo zinyang’anywe ili wasiendelee kuuza viwanja," aliagiza Waziri Mkuu

0 Comments:

Post a Comment