MPANGO ATAKA NGOs ZIZINGATIE MAADILI




MAKAMU wa Rais,  Dkt. Philip Mpango ameyapongeza Mashirika Yasiyo ya Serikali, (NGOs) kwa kazi kubwa wanayoifanya, wakiigusa jamii kwa njia mbalimbali. 

Ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2023 wakati akifungua jukwaa la mwaka la NGOs jijini Dodoma.

Aidha amesisitiza nia ya Serikali kuweka mazingira mazuri ya kufanikisha shughuli za NGOs na kuondoa changamoto zinazowakabili. 

Pia, alitoa wito kwa NGOs kuzingatia maadili ya Kitanzania na kuepuka kutumiwa kinyume cha sheria na mila za nchi.


Dkt akizungumzia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, aliwapongeza NGOs zinazoshiriki katika kukabiliana na suala hili na kuwataka kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira. 


Aliunga mkono pendekezo la kuimarisha ushirikiano baina ya NGOs za Tanzania na nyingine duniani.


Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima  alisisitiza jukumu la Wizara yake katika kusajili na kuratibu shughuli za NGOs ili ziweze kuleta mchango wenye tija katika jamii.

 Alizungumzia juhudi za kuongeza uelewa kuhusu sera na sheria za kodi zinazowaongoza NGOs. Pia, alitaja juhudi za Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa NGOs, ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya uratibu katika sekta mbalimbali.


Kwa upandw wake , mMuu wa Mkoa wa Dodoma,  Rosemary Senyamule alimshukuru na kumpongeza Rais wa Tanzania kwa kuimarisha ushirikiano kati ya NGOs na Serikali.

 Alitambua mchango muhimu wa NGOs katika Mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla huku akikumbusha kuwepo kwa NGOs 415 zinazofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya sekta za kijamii.


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Seif Shekalaghe alitangaza mafanikio ya kukamilisha ramani ya kidijitali ya utambuzi wa mashirika yasiyo ya Kiserikali, lengo likiwa kusaidia kuondoa changamoto za utekelezaji wa miradi inayofanana katika maeneo yanayofanana.


Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Dkt. Lilian Badi aliwakumbusha washiriki juu ya ukuaji wa sekta ya NGOs na mchango wao muhimu katika maeneo mbalimbali. 

Aliahidi kuendelea kushirikiana na Wizara husika kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.


Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Serikali,  Mwantumu Mahiza,  aliongelea umuhimu wa Serikali kuwaunga mkono NGOs, na kuwataka viongozi wa mikoa na wilaya kushirikiana kwa karibu na mashirika hayo ili kuleta maendeleo ya Taifa.

0 Comments:

Post a Comment