MAHAKAMA: WAZIRI HAKUFUATA SHERIA KUTANGAZA PORI LA POLOLETI

MAHAKAMA imesema kuwa Waziri wa Maliasili na utalii hakuzingatia sheria kwenye mchakato wa kutangaza pori Tengefu la Pololeti kwani wananchi wa vijiji vilivyopo ndani ya eneo hilo hawakushirikishwa.


Hata hivyo mahakama hiyo ilishindwa kutoa amri ya kumtaka waziri kurudia mchakato huo kwa kile ilichoeleza kuwa tayari Rais ameshalipandisha hadhi eneo hilo kuwa pori la akiba.


Hayo yameelezwa leo, Septemba 19,2023 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga wakati akisoma uamuzi kwenye shauri la mapitio namba 21/2022 ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na wananchi wengi hasa jamii ya wafugaji ambao walijitokeza kwa wingi mahakamani hapo.



Amesema kuwa Waziri alikiuka haki ya kushirikisha wahusika ambao ni wananchi wa vijiji vilivyokuwa ndani ya pori tengefu la Loliondo na kusisitiza kuwa jambo lolote linalofanywa dhidi ya mtu anapaswa kushirikishwa hivyo  ilitakiwa kuzingatiwa.



"Waziri alikosea kwa kushindwa 'kuconsult' wale waliotakiwa kuwasiliana nao kama sheria inavyoelekeza. ..Eneo husika limeshapandishwa hali kuwa  'game reserve' pori la akiba kutoka kutoka 'game controlled area' poro tengefu ambapo Rais alilipandisha hadhi kwa mujibu wa sheria," ameeleza Jaji Tiganga akisoma uamuzi huo na kuongeza 

... Mahakama inajiuliza kuwa inaweza kumrejesha waziri kushuhulikia suala hilo wakati aliye juu yake ameshafanya mamuzi na sheria inampa mamlaka Rais kupandisha hadhi ya eneo,".

"Basi kama kuna upingaji basi unapaswa kupinga uamuzi huo wa Rais wa kutangaza eneo hilo kuwa pori la akiba  ....kutoa amri kuwa waziri narudie arekebishe itakuwa si sahihi kwa sasa Tangazo la serikali la waziri halipo kwani Rais ameshalifuta na kutangaza Pololeti kuwa Game Reserve kwa GN namba ....ya Oktoba 14,2022,".

Hata hivyo Jaji Tiganga alitupilia mbali hoja nyingine tisa zilizowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa waleta maombi watano, Latang'amwaki Ndwati, Ndamalia Taiwap, Megwari Moko, Ezekiel Sumare na Latajewo Sayari.



Waleta maombi hao waliwakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Joseph Ole Shangai, Yonas Masiaya, Joseph Alais na Dennis Mosses huku wajibu maombi ambao ni Waziri wa Maliasili na Utalii na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwakilishwa na mawakili Mkama Msalama na Ian Mbise.

Kwenye shauri hilo waleta maombi hao walikuwa wanaiomba iiagize Serikali kuondoa zuio dhidi ya  Wananchi  kuingia kwenye eneo la Kmilometa za mraba  1,502 ambalo wamekuwa wakitumia kwa ajili ya malisho ya mifugo yao na kufanyia shughuli za imani yao.

Aidha walikuwa wanaiomba  mahakama itengue Tangazo la Serikali namba 421  (GN421) la Juni, 17  2022  kwa kuwa ni batili na limetangazwa kinyume na sheria na pia haikuwashirikisha wananchi kama sheria inavyotaka

Ombi lao la tatu walikuwa wanaiomba mahakama itamke kuzuia Serikali na Mawakala wake wasifanye oparesheni zote kwenye eneo hilo.

0 Comments:

Post a Comment