HABARI: Vuta nikuvute Mahakamani kesi ya Mwenyekiti wa UVCCM Arusha

Imeandaliwa na Staff , Grace Macha

(ni kuhusu kesi inayomkabili mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha Lengai ole Sabaya ya kujifanya mtumishi wa idara ya usalama wa Taifa (TISS) ili kujipatia chakula katika hoteli ya kimataifa jijini Arusha)
Picha ya December 14, 2016 ikimuonesha Mwenyekiti UVCCM - Arusha. Ndg. Lengai ole Sabaya. mara alipoachiwa na mahakama mwaka jana

Mvutano mkali umeibuka baada ya upande wa Jamhuri kutaka kuliondoa mahakamani  shauri la kujifanya mtumishi wa umma idara ya usalama wa Taifa (TISS) na  kujipatia chakula hotel ya Kimataifa jijini Arusha, linalomkabili Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, (UV CCM),  Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya.

Wakili wa Serikali, Grace Madikenya aliwasilisha ombi hilo jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha, Gwantwa Mwakuga, ambapo alieleza sababu za kufikia hatua hiyo ni shahidi wao muhimu kuwa nje ya nchi kwa miezi 18 hivyo hataweza kufika mbele ya mahakama hiyo.

Alidai kuwa walifikia uamuzi huo kwa nia njema kabisa baada ya kuona kuwa kuendelea kumsubiri shahidi huyo kwa kipindi hicho ni kumtesa mshitakiwa. 

Wakili wa Ole Sabaya ambaye pia ni diwani wa kata ya Sambasha, Edna Haraka alipinga vikali ombi hilo na kuiomba mahakama hiyo iendelee na shauri hilo huku akidai kuwa upande wa Jamhuri unaitumia Mahakama kama kichaka cha kumnyanyasa kwa kumnyima haki mteja wao.


Alidai kuwa hii ni mara ya pili kwa upande wa jamhuri kuomba kumfutia mashitaka mteja wake ambapo kwa mara ya kwanza walikubali mahakama ikamfutia mashitaka lakini  alikamatwa tena muda mfupi mara baada ya kutoka kwenye chumba cha mahakama ambapo polisi walimshikilia huku wakimnyima dhamana.

“Sasa leo tupo katika kusikiliza shahidi wa tatu na badala ya kuleta shahidi walileta maelezo ya shahidi na leo wanakuja na stori ya
kuiondoa ili waendelee kumnyanyasa mteja wetu, hapana, ofisi  ya mwanasheria mkuu inatumika vibaya kwa kivuli cha Mahakama,” alisema Wakili Haraka.



Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Gwantwa Mwakuga aliahirisha shauri hilo mpaka Aprili 28, mwaka huu,atakapotoa uamuzi wa kukubali au kukataa  shauri hilo kuondolewa mahakamani.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mnamo mei 18 , mwaka jana, katika hotel ya Sky Motel, Ole Sabaya,  alijifanya ni mtumishi wa TISS na kupata huduma ya kulala katika hotel hiyo huku akihudumiwa chakula na vinywaji wakati sio kweli.

Katika shitaka la pili, Ole Sabaya ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti wa mkoa wa UV CCM, anadaiwa kugushi kitambulisho cha utumishi wa TISS kilichosomeka MT.86117 wakati akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Sabaya alikana mashitaka hayo na yuko nje kwa dhamana aliyotakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye mali ya shilingi milioni 10 .

ALIVYOFUTIWA MASHITAKA DESEMBA 15, MWAKA JANA
Mahakama hiyo ilimfutia mashtaka kama hayo Ole Sabaya Desemba 15, mwaka jana baada ya  Wakili wa Serikali, Grace Madikenga, kuieleza  mahakama hiyo mbele ya Hakimu Gwantwa Mwankuga, kuwa shauri hilo lilikuwa limepangwa kuanza kusikilizwa ila jamhuri hawana  nia ya kuendelea nalo huku akitumia kifungu cha 91(1) cha sheria ya uendeshaji wa madhauri ya jinai (CPA) kuliondoa shauri hilo mahakamani hapo.
Image result for Lengai ole Sabaya.
Kitambulisho feki alichotumia mtuhumiwa Lengai Ole Sabaya
Katika kesi hiyo Ole Sabaya, alikuwa anakabiliwa na makosa miwili  ikiwemo  kughushi nyaraka za kitambulisho cha usalama wa Taifa chenye picha yake na kutumia namba Saturday. Code. Eagle 3 idara ya usalama wa Taifa chenye namba MT. 86117.

Hata hivyo wakati wakili wa Serikali aliomba kuondoa shauri hilo, wakati  tayari shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Inspekta Rogathe wa Kituo cha Polisi Arusha alikuwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi  wake.

Hakimu Gwantwa alikubaliana na maombi hayo hivyo  alimuachia huru, Ole Sabaya.
Mara baada ya Mahakama kumuachia huru Ole Sabaya , polisi walimkata tena wakati akitoka mahakamani hapo ambapo walimpakia kwenye  na gari la polisi lililokuwa na namba za usajili T 953 CSZ na kuondoka naye.

Mtandao huu ilimtafuta Kamanda wa Polisi mkoani hapa, (RPC), Charles Mkumbo ambapo alithibitisha jeshi hilo kumkamata tena ole Sabaya ambaye alidai watamrejesha  tena mahakamani kwa tuhuma hizohizo alizofutiwa.

"Ni kweli tumemkamata, hizo ni "technicalities" tu  za kisheria, wamemkamata watafanya taratibu za kisheria watamrudisha tena mahakamani kwa mashtaka hayohayo," alisema kamanda huyo wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.

0 Comments:

Post a Comment