MAWAKILI WA MBUNGE NGORONGORO WAIBUA MAZITO

 SAKATA la Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangay na wananchi  kushikiliwa na polisi limechukua sura mpya baada ya mawakili wao kufungua shauri mahakamani Kuu Kanda ya Arusha wakitaka watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani.



Aidha, mawakili hao wameibua madai mazito kuwa wamefanikiwa kuongea na wananchi hao wanaoshikiliwa na jeshi la polisi wilayani Karatu kuanzia Agosti 16,2023 ambapo baadhi wameumizwa vibaya wakati wakihojiwa na jeshi la polisi.



Mawakili hao wamefanya mkutano na waandishi wa habari leo Agosti 23,2023 Sakina, wilayani  Arumeru wakiwa na baadhi ya wananchi na madiwani kutoka Ngorongoro.


Wakili wa washitakiwa hao, Joseph OleShangay amesema kuwa wameamua kufikisha suala hilo mahakamani ili muhimili huo uweze kutoa amri ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani baada ya kushikiliwa na jeshi la polisi bila kufikishwa mahakamani licha ya muda wa kisheria unaotakiwa kisheria kupita.


Amesema kuwa Mbunge ambaye kwa sasa hajulikani alipo licha ya wao kumuacha akishikiliwa na jeshi la polisi kuanzia  Agosti 21, 2023, na wananchi wengine 31 wanashikiliwa na jeshi hilo tokea Agosti 16, 2023 kinyume cha sheria kwani tuhuma ya ya kujeruhi mwili inayowakabili ina dhamana kisheria.


Amesema juzi baada ya mbunge huyo kukamatwa, yeye kama wakili wake alikuwa pamoja naye na kwamba polisi walimuahidi kuwa mteja wake angepata dhamana jana Agosti 22, 2023, japo had leo, inadaiwa hakuna dhamana na kwamba hajui mteja wake yupo wapi.


"Siku ile usiku pale Karatu baada ya kuandika maelezo niliwaomba dhamana, polisi wakaniambia ingetolewa jana, hata hivyo, nilipofika asubuhi siku iliyofuata, sikumkuta kituoni hapo, tukaelezwa kuwa ameletwa Arusha...hadi leo hatujuwi alipo," amesema Joseph na kuongeza.


...Wamekamata watu tangu Agosti 16 mpaka leo hawajafikishwa Mahakamani na wamekuwa wakiteswa kwa tuhuma za kujeruhi lakini pia wanahojiwa kuhusu kuhamia Msomera,".


Joseph amesema sheria ipo wazi ndani ya  masaa 24 baada ya Watuhumiwa kukamatwa wanapaswa kufikishwa Mahakamani lakini kinachoendelea sio sahihi.


"Binafsi nimezungumza na wote waliokamatwa wamepigwa na wengine ni wagonjwa Sasa kama wanatuhumiwa kwa kujeruhi kwanini na wao wanajeruhiwa,"amehoji wakili Joseph.


Hata hivyo ameweka wazi kuwa hawapingi kukamatwa watu na hawapingi Jeshi la polisi kufanyakazi zao lakini wanachopinga ni kukiukwa sheria kwa kile alichadai kuwa kinachofanyika ni kuwatisha wananchi wasiendelee kuzungumza kuhusu haki zao jambo ambalo hawakubaliani nalo.

Akizungumzia shauri walilofungua mahakamani, wakili, Alayce Melau amesema kuwa  wamefungua shauri kuwa wamepeleka maombi ya kesi kwa msajili na wanaimani kesi itapangiwa hakimu wa kusikilizwa haraka uwezekavyo ili haki ijulikane.


Amesema baadhi ya wananchi waliokamatwa tangu Agosti 17, 2023; wanadaiwa kuwa na hali zao ni mbaya kutokana kile kinachoelezwa kuwa ni ‘vipigo’ huku wengine wakidaiwa kuwa ni wagonjwa.


Melau amesema kati ya wananchi wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kuna mmoja ambaye ni mgonjwa wa kifua kikuu na alikamatwa akiwa anatoka kuchukuwa dawa.

"Huyu mgonjwa analalamika alitakiwa kupata dawa lakini hapati na kibaya zaidi hatakiwi kuchanganywa na watu lakini hadi jana amewekwa sero  oja na watu zaidi ya 20,"amesema wakili huyo.


Kamanda wa polisi mkoa Arusha Justine Masejo ametoa taarifa leo usiku akieleza kuwa upelelezi wa tukio hilo umekamilika na jalada limepelekwa ofisi ya taifa za mashitaka kwa hatua za kisheria.

0 Comments:

Post a Comment