MABULA ATAJA KIINI MIGOGORO YA ARDHI KUONGEZEKA

 Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema chanzo cha migogoro ya ardhi nchini ni watumishi wanaojitolea, ulipaji wa fidia na umilikishaji ardhi kwa watu zaidi ya mmoja.

 



Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Mei 25, 2023 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti 2023/24.


Waziri amesema mikoa iliyoathirika zaidi ni Dar es Salaam na Dodoma ambapo migogoro hiyo hukolezwa zaidi na watumishi wanaofanya kazi za kujitolea bila kuwa na mishahara kwani kwenye maeneo mengine wanakabidhiwa mifumo licha ya kuwa hawana hata mikataba ya utumishi.


Waziri Mabula ametolea mfano Jiji la Dodoma ambapo hivi karibuni aliwatimua kazi watumishi 126 waliowa wanafanya kazi bila kuwa na mikataba lakini wanaendesha maisha yao vizuri na wanaijua mifumo kama waajiriwa wengine.


“Watumishi wengi wanafanya kazi za kujitolea, hawana mikataba lakini wanaendesha maisha yao vizuri tu, Dodoma peke yake tuliwakuta 126 lakini tulipowahoji ilionekana wapo kwenye mfumo,” amesema Mabula.


Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Dodoma ilikuwa na migogoro ya ardhi 815 ambayo ilipaswa kupatiwa ufumbuzi lakini hadi sasa 429 ndiyo imeshughulikiwa huku migogoro 386 ikiwa katika hatua za utatuzi.


Katika hatua nyingine waziri Mabula amesema kuanzia sasa hakuna ruhusa kwa kampuni au mtu binafsi kuchukua ardhi ya mwanakijiji ikiwa hajajipanga kwenye malipo.


Waziri amesema mtu yeyote anayechukua ardhi ya mwananchi alipe si zaidi ya miezi sita tangu tathimini ilipokubaliwa na ikizidi hapo riba itahusika lakini muda ukienda zaidi inapaswa uthamini ufutwe na uanze upya.


0 Comments:

Post a Comment