DKT MPANGO ATOA MAELEKEZO KUKABILIANA NA MIMEA VAMIZI NGORONGORO

 



 

MAKAMU wa Rais, Dkt Philip Mpango ameiagiza Mamlaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,(NCAA) kushirikiana na watafiti wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi kupatia ufumbuzi tatizo la mimea vamizi iliyo ndani ya hifadhi hiyo.  

 

 

Aliyasema Mei 16,2023  wakati akiweka jiwe la msingi kwenye jengo la makao makuu ya NCAA  linalojengwa kwenye mji wa Karatu hivyo kuzihamisha ofisi za taasisi hiyo toka ndani hifadhi ikiwa ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa kuhakikisha shughuli za binadamu zinapungua ndani ya hifadhi hiyo.

 

Dkt Mpango alisema kuwa ni vema NCAA wakashirikiana na taasisi nyingine za kiutafiti pamoja na  ofisi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kutafutia ufumbuzi tatizo hilo la mimea vamizi.

 

“NCAA mshirikiane na vyuo vya utafiti kama Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Chuo Kikuu cha Sokoine Chuo Kikuu cha Nelson Mandele na vyuo vikuu vingine ndani na nje ya nchi mfanye utafiti wa kina na kuja na mbinu ambazo zitatuwezesha kumaliza hili tatizo la mimea vamizi kwenye hifadhi zetu zote na pia sehemu nyingine hapa nchini,” alisema Makamu wa Rias na kuongeza.

 

Dkt Mpango alisema kuwa changamoto ya uvamizi wa wananchi kwenye hifadhi na mapito ya wanyama uongozi wa mkoa wajielekeze kutoa elimu kwa wananchi sanjari na kuwatumia viongozi wa jamii wanaoishi maeneo kuzunguka hifadhi na wa vyama vya siasa wabunge na viongozi wa dini.

 

“Tusipodhibiti uvamizi huu hata malengo yetu ya kuzilinda hifadhi hizi nzuri ambazo mwenyezi Mungu ametupatia hayatafikiwa,” alisisitiza Dk Mpango.

 

Awali Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi NCAA, Elibariki Bajuta alimweleza Makamu wa Rais kuwa wananakabiliwa na tatizo la mimea vamizi ndani ya hifadhi ambalo linasababisha adhari kwenye masuala ya uhifadhi.

 

“NCAA kwa kushirikiana na  taasisi za Uhifadhi na wanasayansi tunaendelea kutafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na mimea hiyo ambayo imekuwa tishio kwa maeneo ya uhifadhi. Moja ya majukumu tunayoyafanya ni kuyafeka na kuyang’oa kabla hayajakomaa,” alisema Bajuta .

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na NCAA Mwezi Mei, 2021, mimea vamizi ya aina mbalimbali imeathiri maeneo ya ndani ya Hifadhi hususan maeneo ya Ndutu, Olduvai na eneo la Kreta ya Ngorongoro ambalo takribani hekta 5000 sawa na asilimia 22 ya eneo lote la Kreta limeathirika na mimea hiyo.

 

 

Mimea Vamizi iliyopo katika eneo hilo kuwa ni pamoja na Bidens schimperi, gutenbergia cordifolia, Datura, stramonium na argemone Mexicana ambapo njia za kitaalamu zinazotumika kuangamiza mimeo hiyo ni pamoja na kufyeka na kuchoma.

 

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa mimea vamizi katika eneo la hifadhi husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, vifaa vya ujenzi, mazao kama mahindi na mifugo inayoingia ndani ya Hifadhi ambapo kwa pamoja huchangia uwepo wa mimea hiyo.

 

Hifadhi ya NCAA ilianzishwa mwaka 1959 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 8,298 likiwa ni eneo la matumizi mseto lenye majukumu ya kuendeleza uhifadhi na malikale, wafugaji wenyeji  waliokuwa ndani ya hifadhi na  kuendeleza shughuli za utalii.

 

Kwa sasa Ngorongoro wanasimamia eneo la Pori la Akiba la Pololeti lenye Kilimeta za Mraba 1,500 maeneo ya mali kali Mapango ya Amboni na eneo la Engaruka.

 

0 Comments:

Post a Comment