Na Gift Mongi,Moshi
Wawekezaji mbali mbali kutoka nje na ndani ya Tanzania kwa sasa wana kila sababu yakuvutiwa na mazingira ya uwekezaji ambayo yamewekwa na serikali tangu kupatikana kwa uhuru miaka 60 iliyopita ikiwemo amani,utulivu,usalama pamoja na ardhi na malighafi nyinginezo nyingi.
Mwakilishi wa kituo cha uwekezaji nchini, (TIC), Daud Riganda aliyasema hayo mara baada ya kushuka mlima Kilimanjaro akiwa ni mmoja wa wapanda mlima 150 ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru ambapo alisema hakuna mwekezaji yoyote anayependa kuwekeza sehemu kusipokuwa na mazingira rafiki.
Riganda ambaye pia ni meneja wa kituo hicho Kanda ya Kaskazini alisema kuwa rasilimali zote ambazo zinafaa kwa uwekezaji zinapatikana nchini tangu uhuru hadi Sasa na kuwa amani na utulivu ambavyo ni muhimu kwenye uwekezaji pia vipo kwani hakuna mwekezaji anayependa kuwekeza sehemu isiyo na utulivu au amani.
"Sisi TIC tumeadhimisha miaka hii 60 ya uhuru tukiwaambia wawekezaji kuwa Tanzania bado ni sehemu salama kwa kufanya shughuli za kiuwekezaji kwani rasilimali zipo pamoja na amani na utulivu ambavyo ndio vivutio muhimu"alisema Riganda
Alisema zipo sekta mbalimbali ambazo bado zinahitaji uwekezaji kama kilimo,uvuvi,viwanda vya kuongeza thamani,sekta ya utalii na miradi mbalimbali na kuwa bado kituo hicho kinahitaji wawekezaji hao kwani mazingira ni rafiki na yanaruhusu kwa kazi hizo.
"Mazingira yanaruhusu kwa uwekezaji hapa nchini katika sekta mbalimbali na ndio maana tumeenda kuiambia dunia na Afrika kwa ujumla kuwa sisi ninwakonhwe katika kuilinda amani na utulivu hivyo waje wasiwe na wasiwasi wowote Tanzania ni sehemu salama kabisa"alisema
Alisema kituo cha uwekezaji (TIC) kilianzishwa rasmi mwaka 1997 baada ya kupitishwa kwa sheria ya uwekezaji kimekuwa na dhima kuu ya kukuza uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha,kuratibu,na kuwezesha uwekezaji wenyewe sio tu kwa wageni bali hata kwa wazawa.
Kwa upande wake afisa habari na Uhusiano wa bodi ya utalii nchini(TTB) Augustina Makoye aliwapongeza wananchi kwa mwitiko mkubwa waliouonyesha kwa kujitokeza kwa wingi kuupanda mlima huo huku akiwahimiza kuendeleza ari hiyo katika kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivyopo maeneo mbalimbali hapa nchini.
Safari hiyo iliyoandaliwa na shirika la hifadhi za Taifa, (TANAPA) kwa kushirikiana na kampuni ya uwakala wa utalii ya ZARA ilijumuisha watu kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi ikiwemo TANAPA wenyewe, JWTZ, Bodi ya utalii nchini(TTB), Wakala wa Huduma za Misitu nchini,(TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,(NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori, (TAWA), Benki ya NBC na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
0 Comments:
Post a Comment