HIFADHI ya Taifa ya Mlima
Kilimanjaro, (KINAPA) imesema iko mbioni kuanza kutumia 'cable cars'
kupandisha watalii kwenye mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi
TANAPA, Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho ameyasema hayo Oktoba 10, mwaka huu
wakati akiongea kwenye hafla ya kuwapokea wapanda mlima 150 waliopelekea
bendera ya Taifa kwenye kilele cha mlima huo kwa ajili ya maadhimisho ya miaka
60 ya uhuru wa Tanzania Bara wakiongozwa na Kanali, Martin Msumari.
Amesema KINAPA imeendelea
kuboresha miundo mbinu yake ikiwemo njia za kupanda na kushuka, vifaa vya
uokoaji badala ya kutumia baiskeli ya kitanda ya mguu mmoja kwa uokoaji sasa
wanatumia helkopta kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
"KINAPA imeweza kuongeza mazao
ya utalii kutoka yale ya kutembea kwa miguu kupanda mlima mpaka sasa wengine
wanapanda mlima kwa baiskeli na tuko mbioni kuanza kutumia 'cable car' jambo
ambalo litawezesha watalii hata wale ambao ni walemavu waweze kufika na kuona
hifadhi yetu na mandhari mbalimbali zilizopo kule," anasema Batiho na
kuongeza.
..Shughuli kama parachuti
zinafanyika kwenye kile kilele cha mawenzi watalii wanapanda lakini na
kuna watalii wanafanya safari za siku moja kuona maporomoko ya maji ya Marangu
na wengine wanaenda mpaka kituo cha Mandara...
...Kuna utalii wa kimichezo,
tumeshuhudia kuna watalii nakuja kufanya michezo kwenye Uhuru Crater,
kuruka vikwazo pamoja na kukimbia hivi ni moja ya vitu vinavyovutia watalii
wengi kuja na kuongeza mapato,".
Batiho amesema kuwa wamepanga mpaka
kufikia mwaka 2026 watalii wawe wameongezeka kufikia watalii milioni 5 kwa
mwaka kutoka watalii milioni 1.5 wanaotembelea hifadhi hiyo kwa mwaka ambapo
itaongeza mapato kufikia dola za Marekani milioni 6.
Amesema kuwa wameweka mikakati ya
kufikia malengo hayo ikiwemo hilo la kuanza kupandisha watalii mlimani kwa
kutumia 'cable car', kuboresha miundo mbinu kwa kujenga mabanda katika njia ya
Kidia na Marangu.
"Wapandaji nadhani mmeshuhudia
pale Horombo kuna ujenzi wa mabanda unaendelea na bado kuna 'plan B' ya
kuongeza mabanda zaidi ili kutosheleza mahitaji pale pamoja na kituo cha
Kibo," amesema Batiho.
Hata hivyo amesema kuwa hayo
yatawezekana endapo kwa pamoja wadau wote wakiwemo wananchi watashirikiana
kulinda mazingira ya mlima huo kwani KINAPA haiwezi kuulinda mlima huo kwa
mtutu wa bunduki pekee.
Pia Batiho amewaomba wale
wanaoongoza na kuwahudumia watalii kufanya kazi hiyo vizuri na kwa uaminifu kwa
kuacha kuwaibia wageni na kuwaomba fedha (Tip) kwani vitendo hivyo huwakera
watalii.
"Sisi kama KINAPA tumejipanga
kupanda miti kwa kushirikiana na wananchi wanaotuzunguka kwa sasa tumeanza na
miche laki moja na zoezi hili limeashaanza na nia ni kupunguza hewa ya ukaa
ambayo kwa kiwango kikubwa ndiyo inayochangia kuharibu ozoni,amesema -Batiho na
kuongeza
....Nikuombe Mkuu wa mkoa muweze
kuhamasisha wananchi ili hii miti tunayopanda wahakikishe inakua ili
kukabiliana na hewa ya ukaa lakini wao wapate kuni na matunda,".
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Kampuni ya uwakala wa utalii ya ZARA, Zainab Ansel alisema kuwa wametumia zaidi
ya miezi sita kuandaa safari hiyo hivyo anamshukuru Mungu kwa safari hiyo
kukamilika kwa mafanikio.
" Mwaka huu wamepanda watu 153
mwakani tutaomba tupewe muda wa kutosha kufanya matangazo ili watu wengi zaidi
wajitokeze kupanda kusherekea miaka 61 ya uhuru,"alisema Zainab.
Hata hivyo aliwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi kutembelea vivutio vingine vilivyopo nchini kwani
Tanzania imebarikiwa vivutio vingi sana vya utalii vulivyopo kwenye
maeneo mbalimbalimbali ya nchi.
Akiwapokea wapanda mlima hao, mgeni
rasmi , mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaiga amesema
mlima Kilimanjaro una umuhimu zaidi ya inavyofikiriwa na wengi kuwa ni
kwa ajili ya utalii kwani ndiyo unaopeleka maji kwenye bwawa la nyumba ya Mungu
linalotumika kwa shughuli za uvuvi na kuzalisha umeme hivyo kila mmoja ana
wajibu wa kulinda na kutunza mazingira ya mlima huo.
Amesema kuwa maji yanayotoka kwenye
mlima Kilimanjro ni muhimu kwa maisha ya wananchi kwani ndiyo ynayotumika kwa
matumizi ya nyumbani, kilimo cha umwagiliaji na kwenye bonde la Pangani.
"Watu wengi wanafikiri mlima
huu uko kwa ajili ya utalii tu ila huyu mama (Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi
KINAPA,Angela Nyaki) nikifika Kilimanjaro alikuja ofisini alinieleza kuwa kumbe
maji ya kilimo yanatokana na mlima juu. Maji ya nyumba ya Mungu, bonde la
Pangani yote yanatokana na mlima huu, hata umeme wa Nyumba ya Mungu
chanzo ni hapa," alisema Kigaogai na kuongeza.
....Kuanzia pale niliamua kuwa
balozi wa huu mlima, na kuanzia pale nilikuwa mkali kuhakikisha mazingira
yanahifadhiwa, huu mlima ni kitega uchumi na ni maisha ya wananchi wa Tanzania
...
Wananchi waunge mkono jitihada za
kuuhifadhi mlima huu itakuwa vibaya tukiharibu mazingira kwa kukata misitu na
kufanya shuguli za kilimo ndani ya hifadhi ya mlima huu ,".
Kigaigai amesema kuwa takwimu
zinaonyesha utalii wa ndani kwa ajili ya kupanda mlima Kilimanjaro unasuasua
hivyo akatoa rai kwa wananchi wa Jumiya ya Afrika Mashariki, (EAC) wajenge
utamaduni wa kutembelea vivutio vilivyo kwenye ukanda huo ili kukuza utalii wa
ndani.
Kiongozi wa msafara huo kutoka Jeshi
la Wananchi wa Tanzania, (JWTZ), Kanali, Martin Msumari amesema kuwa wapanda
mlima 79 wamefanikiwa kufika kwenye kilele cha uhuru.
"Desemba 9, tuliandika historia
kwa kuwa uhuru 'peak' (kilele) palisongamana watu kutoka ndani na nje ya nchi,
watu 75 kufika hapo si jambo dogo," alisema Kanali Msumari.
Aidha aliuomba uongozi wa TANAPA kumtumia
Mtangazaji wa Shirika la habari la Uingereza, (BBC), Salim Kikeke kama balozi
wa hiari wa kuutangaza mlima huo kwani ana watu wengi wanaomfuatilia ndani na
nje ya nchi aweze kuwashawishi kuja kufanya utalii kwenye mlima huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi
ya TANAPA, Jenerali Mstaafu, George Waitara, alitoa zawadi ya shilingi milioni
tano kwa waongoza utalii na wabeba mizigo wa kampuni ya uwakala wa utalii ya
ZARA kazi nzuri waliyofanya kuhudumia msafara huo kwa siku siku suta walizokuwa
mlimani.
"Namshukuru sana mama
Zara(Zainab Ansel) kwa kuweza kufanikisha zoezi hili. Kabla ya kustaafu kama
mkuu wa majeshi tuliweka utaratibu wa kupanda kila mwaka nikishirikisha watu
mbalimbali. Nashukuru Jeshi wameendeleza na nilipoteuliwa kuwa Mwenyekiti
wa bodi ya TANAPA nikahakikidha wanaliweka kwenye kalenda zao,"alisema
Waitara na kuongeza.
.....Nilienda mpaka kituo cha
Mandara ili nione watu 150 wanapandaje mlima nikajiridhisha huduma ziko vizuri,
sehemu za kulala ziko za kutosha chakula kiko vizuri...
... 'Guide' (muongoza utalii)
Faustini Chombo ni mzuri na timu yake alinihakikishia wengi watafika na
wamefika na wagumu (wabeba mizigo) mmefanya kazi kubwa kwa kuwatambua na kuwapa
soda . Nawapa shilingi milioni tano.Mmefanya kazi nzuri sana mara zote
niliwaona mnatabasamu mnajitolea kuumia ili mpanda mlima asiumie,".
Alisema kuwa suala la Mtangazaji,
Kikeke kutangazwa kuwa balozi wa utalii wa mlima huo ataliwasilisha kwa Waziri
wa Maliasili na Utalii, Damas Ngombaro huku akidaI anaamini atalikubali
kwani anaamini mtangazaji huyo atakuwa anakuja kila mwaka na marafiki zake kwa
ajili ya kupanda mlima huo .
Hifadhi ya KINAPA ilianza mwaka 1973
na kwa msaada wa shirika la Misaada la Norway, (NORAD) waliweza kujenga mabanda
kwenye kutuo cha Mandara na Horombo.
KINAPA kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali waliweza kufungua njia nyingi za kuweza kufika kileleni kwani
walianza na njia moja ambapo kwa sasa zipo njia saba tano za kupanda mlimani na
mbili za kushuka.
Hifadhi hiyo imekuwa na manufaa kwa
wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi hiyo na Taifa kwa ujumla huku ikifanikiwa
kupata tuzo mbalimbali ambapo mwaka 2013, ilipata tuzo tano kama sehemu nzuri
zaidi ya kutembelewa na watalii.

0 Comments:
Post a Comment