Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wakiingia kwenye chumba cha mahakama
MAWAKILI wa utetezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabilia aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita hawajafika mahakamani hivyo kusababisha shauri hilo kushindwa kuendelea.
Hali hiyo imesababisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo Jumatano Desemba 29, 2021 kushindwa kutoa uamuzi mdogo kama ilivyokuwa imepanga kufanya.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda Sabaya na wenzake wanatetewa na Mawakili Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka na Fridolin Bwemelo.
Awali , Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia alieleza mahakama kuwa upande wa watuhumiwa hakuna wakili hata mmoja na watuhumiwa wote wapo mbele ya mahakama hiyo.
"Leo upande wa watuhumiwa hakuna wakili hata mmoja ila watuhumiwa wote wapo. Shauri lilikuja kwa ajili ya uamuzi mdogo na kwa kuwa watuhumiwa wana uwakilishi wa mawakili ambao kwa siku ya leo hawapo,"alisema na kuongeza
.....Mahakama inakuwa haipo katika nafasi ya kutoa uamuzi huo mdogo labda kama washitakiwa wataondoa uwakilishi. Tunaomba tupangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutoa uamuzi huo mdogo,"
Hakimu Kisinda aliwauliza watuhumiwa hao iwapo bado wanauwakilishwa na mawakili wao ambapo waliieleza mahakama bado wanawakilishwa.
Aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 3, 2022 kwa ajili ya kutoa uamuzi huo mdogo ambapo pia aliutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha shahidi aliyekuwa anaendelea kutoa ushahidi wake anakuwepo mahakamani hapo kwani baada ya uamuzi huo ataendelea.
Uamuzi huo mdogo ulipangwa kutolewa ulitokana na mawakili wa utetezi kuwasilisha pingamizi kutolewa na wakati shahidi wa 13 wa Jamhuri, Ofisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),Ramadhan Juma, akiendelea kutoa ushahidi.
Desemba 17 mwaka huu, akiwasilisha hoja ya pingamizi hilo Wakili Mahuna aliieleza mahakama kuwa shahidi huyo hana uwezo wa kutambua watu kupitia ripoti hiyo ambayo hajaiandaa yeye na wala siyo mtaalamu kutoka maabara ha kiuchunguzi.
Alisema kuwa shahidi wa nane, Johnson Kisaka (Ofisa uchunguzi kutoka maabara ya kiuchunguzi ya Takukuru), aliieleza mahakama kuwa hawezi kumtambua mtu kupitia ripoti hiyo.
Alieleza kuwa iwapo Juma atawatambua watu hao wakati hajashiriki wala kuandaa ripoti hiyo atakuwa anatoa maoni yake hivyo kuomba mahakama isimruhusu kutambua watu kwenye ripoti ambayo hajaandaa yeye.
Kwa upande wao mawakili wa Serikali waliomba mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi hilo kwa madai kuwa halina misingi ya kisheria wala mashiko na kuwa shahidi huyo alikuwa anataka kuionyesha mahakama kile alichokuwa ameeleza kukibaini kwenye ripoti hiyo iliyopo kwenye flash.
Awali kabla ya pingamizi hilo, Wakili Kwetukia aliiomba mahakama shahidi huyo atambue vielelezo mbalimbali ikiwemo CCTV footage ambayo ilikuwa kwenye ripoti aliyoandaa na kuwasilisha mahakamani hapo kama kielelezo shahidi wa nane (Kisaka).
Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine kwenye shauri hilo ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
0 Comments:
Post a Comment