WATOTO WA WAFUNGWA WAKUMBUKWA



WATOTO ambao wazazi wamefungwa katika gereza kuu la Kisongo mkoani Arusha, jana wamepewa misaada ya vyakula, mafuta,nguo na sukari kutoka kwa wafanyakazi wa shirika la Posta mkoa wa Arusha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya posta duniani.



Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo,Kaimu Meneja wa Posta mkoa wa Arusha,Renada Mtitima alisema msaada huo ni sehemu  ya mchango wa shirika hilo kwa jamii, katika kuwafariji watoto ambao wazazi wao wamefungwa.


Mtitima alisema msaada huo pia sehemu ya jukumu la shirika la posta kurejesha faida ambayo wanaipata kwa jamii lakini pia kuthibitisha shirika hilo ni mali ya serikali inayo jukumu la kisheria kuhudumia jamii.


"Tunaomba kuwajulisha kuwa shirika la posta limeanzisha huduma mpya za kidigitali ambazo ni duka la mtandao wa posta,virtual box na huduma za pamoja za posta"alisema


Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo msimamizi wa kituo cha kulea watoto hao cha St Gabriel home, mtawa Frola  Ndwata  alisema kituo hicho kilichoanza 2006 hasa baada ya kubaini uwepo wa watoto wadogo katika gereza la Kisongo hadi sasa kina watoto 18.


Hata hivyo alisema kuna changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikiwakabili  ikiwepo majengo ya kutosha, chakula, mavazi, baadhi ya wazazi ambao wanatoka magereza kuwatelekeza watoto na wengine kutokuwa na uwezo wa kukaa nao na kuwasomesha.


Afisa mwandamizi wa posta mkoa wa Arusha, Benedict Mkini, awali alieleza shirika hilo limeboresha utendaji wake baada ya kuzindua  mfumo mpya wa  uendeshaji na usambazaji shughuli za posta(PMIS) ambao sasa  unawezesha mteja kufatilia mzigo wake unaosafirishwa kutumia simu yake au kompyuta.


Mkini aliwataka wakazi wa Arusha pia kujitokeza kupata huduma za kusafirisha barua, mizigo, sampuri za kimaabara na nyingine kwa gharama nafuu.



0 Comments:

Post a Comment