MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela emelipongeza Jeshi la polisi kwa kupunguza matukio ya ajali za barabarani na ubunifu wa kwenda katika maeneo ya wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto kwa ajili ya kukagua vyombo vyao.
Ametoa pongezi hizo, Oktoba 23,2021 wakati akifungua rasmi zoezi la ukaguzi wa vyombo vya moto kuelekea maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Arusha kuanzia Novemba15 mpaka 20,2021.
Mongela aliwapongeza wadau wa usalama barabarani hususani madereva kwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya ukaguzi wa vyombo vyao.
Alisema ni muhimu wananchi waendelee kuelimishwa kuhusiana na sheria za usalama barabarani na kukemea vitendo vya rushwa kwa Askari wachache ambao wanachafua taswira ya Jeshi la Polisi.
Mongela alitoa wito kwa wadau wa usalama barabarani kushikama na kujitoa kwa pamoja ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa hali ya amani na utulivu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,(RPC), ACP Justine Masejo, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa aliwataka watumiaji wa vyombo vya moto wafuate kauli mbiu ya utii wa Sheria bila shuruti ili kupunguza ajali nyingi za barabarani ambazo zimepelekea watu wengi kupoteza maisha, ulemavu pamoja na uharibu wa vyombo vya moto.
Naye, Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Arusha, (RTO), Mrakibu wa Polisi, Solomon Mwangamilo amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa nafasi kwa baraza la usalama barabarani kufanya tathmini ya jumla kwa mwaka mzima kuhusiana na usalama wa watumiaji wote wa vyombo vya moto.
Pia itawawezesha kuangalia maeneo ambayo yanapelekea ajali nyingi za barabarani na kuja na mikakati ya kupunguza ajali izo.
Alisema katika wiki hiyo watatoa elimu ikiwa ni pamoja na kukagua vyombo vyote vya moto vilivyopo mkoani Arusha, ambapo amesema wametenga maeneo tofauti kwa ajili ya zoezi hilo kwa kuzingatia ukubwa wa Jiji.
Mwangamilo aliyataja maeneo hayo kuwa no pamoja na vituo vya Polisi, viwanja vya Soweto na kwa upande wa wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto watapeleka Wakaguzi wa magari kwenda kufanya ukaguzi katika maeneo yao baada ya kupokea maombi lengo likiwa ni kupunguza ucheleweshwaji wa utoaji huduma.
0 Comments:
Post a Comment