TAASISI ya Kiislam ya Twariqa Tul Qadiriyya imesitisha shughuli zao zote kwa siku 21 kuungana na Watanzania wengine kwenye maombolezo ya kifo cha Hayati, Rais John Magufuli aliyadai kuwa aliwaunganisha wananchi wote bila kujali tofauti zao za kiumani.
Aidha, wamempongeza Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania huku wakiomba wananchi wote bila wamuombee ili Mungu amuepushe na mabaya aweze kuendeleza mambo yote mazuri waliyoyapanga akiwa na Hayati, Rais Magufuli.
Mwenyekiti wa Taifa wa taasisi hiyo, Sheikh Salimu Mubarak maarufu kama Dar-Weish Mti Mkavu alitoa tamko hilo jana jijini hapa akiwa na viongozi kutoka wilaya mbalimbali za mikoa ya Arusha, Dodoma, Tanga na Dar es Salaam waliokuwa wakihudhuria kikao cha bodi ya taasisi hiyo.
"Mimi kama Mwenyekiti wa Taifa wa Twariqa Tul Qadiriyya kwa siku 21 nahairisha masherehe yote, maulid, zikikiri na shughuli zote mpaka maombolezo ya kitaifa yamalizike," alisema Sheikh Salimu na kuongeza.
...Naomba mnapokwenda kwenye mikoa yenu mkawahabarishe wote juu ya masimamo wetu huu kwa sababu ya msiba huu tulio nao kama Taifa. Hayati Rais Magufuli hajazikwa lakini ametuingia moyoni sana,"...
...Alituunganisha soote Watanzania tukawa watu wamoja. Sisi na Wazanzibar tumekuwa wamoja tumeona juzi (machi 23, mwaka huu) matokeo yake. Zanzibar tulidhani hawatampokea ni Waislam lakini kazi waliyoifanya Allah Wakbar hatukuielewa,"...
...Watu wametupa kanga zao akina mama, mashati yao vijana wanajeshi wetu, askari polisi na watu wa chama cha msalaba mwekundu walifanya kazi kubwa kuhakikisha watu wanakuwa salama,".
Sheikh Dar-Weish alisema Hayati, Rais Magufuli alifanya kazi kubwa kuwaunganisha Watanzania wote, Waislam, Wakristu, Wapagani, Wabanian na dini zote na matokeo yake yameonekana namna watu wanavyomlilia kila kona ya nchi.
Aidha alielezea kufurahishwa na hatua ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kusitisha kwa muda hotuba yake aliyokuwa akiitoa katika hafla ya kitaifa ya kumuaga Hayati Rais Magufuli mkoani Dodoma ili kusubiri kumalizika kwa adhana kwa kile alichoeleza imeonyesha ni namna gani kiongozi huyo anaheshimu uhuru wa kuabudu.
WAHIMIZA USHIRIKIANO NA RAIS SAMIA
"Tunaungana na Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, ni mwanamke lakini ndiyo Rais wetu, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kutupatia Rais ambaye anafahamu kwa kina kile kinachopaswa kuendelea kufanyika," alisema Sheikh Dar-Weish na kuongeza.
... Mama Samia alikuwa na Rais Magufuli kwa miaka mitano wakiendesha nchi, anamfahamu hayati Rais Magufuli kuliko sisi. Sisi hata tukasema yapi mazuri lakini bado hatujafikia yale anayofahamu Rais Samia,"..
...Tunamuombea Rais Samia kwa Mwenyezi Mungu aendeleze pale alipoacha Hayati Rais Magufuli. Yeye na Mawaziri wake wawe kitu kimoja kupona kwa wao ndiyo kupona kwetu raia,".
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Twariqa Tul Qadiriyya, Rehema Athuman aliwaomba wananchi wote kwa umoja wao waungane kuomboleza na kumuombea heri Hayati, Rais, Magufuli mbele za Mungu na kumuombea pumziko jema.
Naye, Katibu mkuu wa Twariqa Tul Qadiriyya, Abdi Kisiu, Hayati, Rais, Magufuli wakati wa uhai wake aliwanyanyua wanyonge na kuwaunganisha wananchi wote bila kujali tofauti zao za kiimani huku akitolea mfano namna alivyoweza kuchangisha fedha kanisani kwa ajili ya kuwajengea msikiti, Chamwino Dodoma.
Alisema kuwa kila alipokuwa akipelekewa matatizo hakuyadharau alikuwa akifanya kazi akishirikiana na viongozi wote wa dini bila kubagua.
0 Comments:
Post a Comment