FAMILIA YA JPM WAKIWEKA MASHADA YA MAUA


Hayati Rais John Pombe Magufuli , amelazwa katika nyumba yake ya milele,kwenye makaburi ya familia yaliyopo Chato mkoani Geita.



Amezikwa kwa taratibu zote za kijeshi ambazo anapaswa kupatiwa Amiri Jeshi Mkuu. Mizinga 21 imepigwa ikiashiria heshima kubwa kwa kiongozi huyu.


Watu wa karibu na familia pamoja na viongozi ndio wameshiriki moja kwa moja katika mazishi haya kwa kufika Geita na wengine kufuatilia moja kwa moja kwenye matangazo ya Televisheni.


Vilio vimetawala kutoka familia, viongozi, na wananchi wa kawaida hasa wale ambao alikuwa ni kiongozi wao toka akiwa Mbunge wa Chato.


Mapema hii leo Hayati magufuli, aliagwa kwa misa maalum, ambayo ilifanyika katika uwanja cha wazi. Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.


Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete anamkumbuka rais Magufuli kama rafiki, ndugu na kiongozi ambae alikua mchapakazi sana.


Akieleza mahusiano yake na hayati Magufuli tangu alipokuwa waziri wake, Kikwete amesema alikuwa 'jembe lake'.


"Nilipokuwa Rais, Magufuli alikuwa Waziri wangu kwa miaka 10, alikuwa mmoja wa mawaziri niliowaamini na kumtumaini. Alikuwa jembe langu ndio maana nilimuweka kwenye wizara tatu zilizokuwa ngumu ili anyooshe mambo.''


''Yalikuwa matumaini yangu na matarajio yangu angemaliza kipindi chake cha uongozi salama, akastaafu na kuishi maisha marefu baada ya hapo na kupata nafasi ya kutuzika sisi watangulizi wake ambao ni kaka zake, hili la kututoka kabla ya kumaliza muhula wake na sisi kumzika yeye ni jambo ambalo sikuwahi kulifikiria kabisa.'' Alisema Kikwete.


Naye rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, alitoa hotuba yake ambayo ilipunguza huzuni iliyotanda, kwa maneno yake ambao yalifurahisha, na waombelezaji walionekana kufurahia na kusahau kwa muda uchungu wa kumpoteza mpendwa wao.


Mwinyi amesema miongoni mwa mambo ambayo Magufili amewaachia Watanzania, jambo la kwanza nalo ni kubwa, ni pale alipoamua kutekeleza maagizo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.


"Kijana amewaza na kuamua tuhamie Dodoma. Na kutekeleza jambo hilo kwa miaka miwili, jambo ambalo sisi wengine tulichukuwa mika 40, bado hatukujtekeleza"


"Kwa kipindi kifupi cha miaka mitano, nchi yetu imepiga hatua kubwa sana, hata kuushangaza ulimwengu kwa namna alivyoletea taifa lake la Tanzania maendeleo ya haraka sana"


"Mh. Mama Samia, Dkt Magufuli ameondoka ametuachi wewe. Ametuachia wewe ambaye ulikuwa msaidizi wake wa karibu sana. Kwahiyo alichokikusudia Hayati Mgufuli, ndicho ulichokusudia wewe. Nilifurahi sana uliposema siku ile kwenye hotuba yako kuwa " Huyu aliyesimama hapa ndiye Rais mwenyewe huyo" Alisema Mwinyi


Naye Rais wa Tanzania kwa sasa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ataendelea kumuenzi Hayati Magufuli kwakuendeleza mambo yote aliyokuwa ameahidi kuyatekeleza.


"Kwaajili ya kumuenzi Rais Magufuli, kamilisheni mchakato wa Wilaya ya Chato kuwa Mkoa. Kama hamtakuwa mmekidhi vigezo sisi kama serikali tutawaambia nini cha kufanya ili muweze kuwa Mkoa"


"Hapa Rais Magufuli tunazika kiwiliwili chake tu lakini mawazo, falasafa na mipango yake itaendelea kuwepo. Falsafa ya hapa ni kazi tu, itaendelea kuwepo na itaendelea kufanya kazi" Alisema Rais Samia.


Rais Magufuli alifariki tarehe 17 machi kutokana na maradhi ya moyo wakati alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.


Hii ni mara ya kwanza Watanzania kuzika rais aliyefariki akiwa madarakani katika miaka 60 ya Uhuru.


Hayati rais Magufuli amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za ungozi, ikiwa ni pamoja na, ubunge , uwaziri katika wizara mbalimbali na baadae rais wa Tanzania ambapo ameongoza kwa miaka sita.


Atakumbukwa na watanzania kwa sera zake zilizoonwa za kizalendo na imani ya kuweka Tanzania kwanza katika uamuzi wake.


Lakini pia jamii ya kimataifa itamkumbuka kwa jinsi alivyopambana na virusi vya corona kwa namna ya tofauti na mataifa mengine.

0 Comments:

Post a Comment