SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeingia kwenye hatua kubwa ya kuimarisha ulinzi na doria angani baada ya Kamishna wa Uhifadhi, Massana G. Mwishawa, kukagua ndege ndogo mbili (2) mpya aina ya Savannah zilizonunuliwa hivi karibuni.
Ndege hizo zimenunuliwa kupitia mradi unaofadhiliwa na BMZ, uliotekelezwa chini ya Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani. Lengo kuu la ununuzi huo ni kuongeza nguvu katika doria na uhifadhi wa wanyamapori kwenye Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere.
Ukaguzi huo umefanyika leo katika Karakana iliyopo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, ambapo ndege hizo zinaendelea kuunganishwa tayari kwa kazi.
Akiwa uwanjani hapo, Kamishna Mwishawa amewapongeza mafundi wanaoendelea na kazi ya uunganishwaji wa ndege hizo kwa umakini mkubwa.
Pia, ametoa pongezi za kipekee kwa marubani wawili (2) ambao ni Askari Uhifadhi wa TANAPA. Marubani hao kwa sasa wapo kwenye hatua za mwisho za mafunzo yao maalum ya kurusha ndege hizo ili kuhakikisha usalama na ufanisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Ndege hizo za kisasa aina ya Savannah zinatarajiwa kuanza doria rasmi angani mwanzoni mwa mwezi Oktoba, 2026, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili na kulinda rasilimali za taifa.






0 Comments:
Post a Comment