# Ni siku nyingine ngumu katika historia ya nchi yetu, ila kwangu ni ngumu zaidi, ilianza ugumu tangu nilipotangaza kifo cha Rais Machi 17, 2021 nilihisi nafanya makosa kumtangaza Rais wangu kuwa amefariki lakini nikaambiwa hakuna wa kulitangaza hili isipokuwa mimi, nilijipa moyo kutangaza
# Binadamu wote lazima siku moja turudi kwa Muumba wetu, lakini kifo hiki hatukukitarajia kwa wakati huu tulionao, tuko katika bumbuwazi, tuko katika majonzi na simanzi tele, ni vigumu sana kukabiliana na ukweli kuwa Rais Magufuli leo hatuko nae tena
# Nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana viongozi wenzetu kutoka nchi mbalimbali kuja kujumuika nasi katika kutufariji katika kipindi hiki kigumu, huu ni ushahidi kuwa Rais wetu alikuwa kipenzi cha watu si kwa watanzania pekee bali duniani kote
# Ndugu zangu, Rais Magufuli ni mtu aliyebahatika kusikia na kupokea sifa zake angali yu hai, hili ni jambo la nadra sana kwa maisha ya mwanadamu, inatupa faraja kwamba ameondoka akiwa anajua watanzania tulithamini na kuenzi mchango wake na Mungu alimjalia karama ya kujua kwamba tutamkumbuka kwa yote aliyoifanyia nchi hii, na kweli leo hata milele tutamkumbuka
# Rais Magufuli hakuogopa kutetea kile alichoamini kuwa ni sahihi kwa maslahi ya Taifa hata kama kingehatarisha maisha yake
# Siwezi kusahau mchango wa Mhe. Rais Magufuli katika maisha yangu ya kisiasa, daima namshukuru kwa imani kubwa kwangu na kwa wanawake wa Tanzania, aliiandika historia ya usawa na uwiano wa kijinsia kwenye nyanja za siasa nchini
# Kupitia Rais Magufuli Tanzania ilipata mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais *na sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania*, nafarijika alinipa fursa ya kuuonesha uwezo wangu na kwamba wanawake tunaweza tukijengewa mazingira ya kufanya kazi kisawasawa
# Kwa tuliofanya naye kazi tunajua jinsi saa 24 hazikumtosha, hakuwa na mchana wala usiku, tulizoea kupigiwa simu na kupewa maelekezo muda wowote hata iwe usiku wa manane, bidii yake ilikuwa zaidi ya mchwa, alipenda kuona matokeo kutoka kwetu na sio visingizio na lawama
# Alitukumbusha kuwa amejitolea maisha yake kuwa sadaka kwa watanzania, hivyo hakuwa na budi kufanya kazi usiku na mchana ili kuwaletea maendeleo watanzania, sote tulihoji sana kama alipata muda wa kupumzika na familia, hivyo hii ilitusukuma nasi nyuma yake kufanya kazi kwa bidii
# Tunapoenda kumpumzisha, sisi viongozi tunaahidi kwamba tutaendeleza kazi yake nzuri kwa nguvu na kasi ile ile
# *Naomba niseme kidogo, kwa wale wenye mashaka na mimi kwamba mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Tanzania, nataka niwaambie kuwa aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke*
# Ndugu waombolezaji wenzangu, tumempoteza kiongozi mahiri, shupavu, jasiri, mchapakazi, mwadilifu, mnyenyekevu, mcha Mungu, mfuatiliaji, mzalendo kwa Taifa lake, mtetezi wa wanyonge, mwana mwema wa Afrika, mwana mapinduzi wa kweli, mwana mageuzi wa kweli, mtu asiye na makuu na mtumishi wa wote
# Kwa tuliomfahamu na kupata fursa ya kuishi nae tuliona unyenyekevu, upendo na huruma yake uvunguni mwa taswira yake ya ukali tuliyoiona katika matamshi yake
# Aliamini kwenye kuhakikisha watanzania wote wanapata haki ya usawa wa kujitafutia riziki ya halali popote nchini, hivyo alirasmisha sekta isiyo rasmi na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanya biashara na majasiriamali wadogo kufanya kazi na kujipatia riziki
# Alikuwa si kiongozi pekee bali pia mzazi na mlezi kwa wengi, mwenye kusamehe, kuvumilia, kulea sana, mkweli na mtumbuaji kwa waliokithiri kwa kutenda kinyume na maadili
# Kama walivyosema viongozi kutoka mataifa ya nje, Rais Magufuli hakuwa mtu wa kusafiri nchi za nje kwa sababu aliamini katika kutumia muda wake mwingi ndani ya nchi kutatua kero za wananchi wake waliomchagua, alinipa kazi ya kwenda mataifa ya nje kumwakilisha, hii inanifanya nimshukuru kwani ni kama alijua kwamba mbeleni kutatokea kitu, imenijengea uwezo wa kufanya kazi na watu pamoja na taasisi za nje
# Hayati Magufuli alienzi na kuthamini mchango ya Marais na viongozi wastaafu wote waliotangulia na kumlea kwenye utumishi wa umma, alikuwa muungwana aliyempa mtu sifa zake akiwa angali hai, hakuwa mtu wa kujikweza, alitambua kuwa Tanzania ni zaidi yake na ndiyo maana tuliwaona viongozi mbalimbali wastaafu katika shughuli zote za kitaifa wakifika kumuunga mkono
# Nami nawaomba wazee wangu, Marais wastaafu wa pande zote mbili za Muungano na viongozi wote wastaafu kwamba mimi ni kijana wenu pia, niko tayari kushirikiana nanyi bega kwa bega katika kuijenga Tanzania aliyoitamani mpendwa wetu na sisi sote, *nawahakikishia kuwa hakuna jambo litakaloharibika*
# Kwa nchi za majirani zetu na marafiki, nawahakikishia kuwa tutaulipa wema mliotuonesha kwa kuimarisha uhusiano wetu, Tanzania itaendelea kuwa na ujirani mwema katika ushirika wa kikanda na kimataifa, mahusiano haya yataendelea kuwa salama na kuimarika zaidi chini ya uongozi wangu
# Familia ya Hayati Magufuli tunaahidi tutakuwa nanyi siku zote, mama Janeth na watoto tunatambua jinsi Taifa lilivyotumia muda mwingi na mpendwa wenu kwa ajili ya kuwatumikia watanzania, mlikubaliana nasi ili nchi inufaike huku subira yenu ikiwa ni siku akistaafu baada ya kumaliza muda wake mfurahie pamoja lakini haikutokea, huku tukipanga sisi wanadamu na Mungu hupanga yake, nazidi kuwahakikishia kama Taifa tutaendelea kuwa pamoja
# Nawashukuru sana watanzania wenzangu, tumedhihirisha umoja na mshikamano wetu kama Rais Magufuli alivyotuhasa enzi za uhai wake, asante pia viongozi wa dini kwa kuzidi kutuombea katika kipindi hiki, navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kusimamia amani na utulivu, pongezi kwa vyombo vya habari kwa habari zote, asanteni wasanii kwa nyimbo za kutufariji kipindi hiki cha maombolezo
0 Comments:
Post a Comment