MAJAJI WATATU KUSIKILIZA KESI YA KABUGA

 ARUSHA


Mahakama ya Umoja wa Mataifa (Mechanism) ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika Rwanda mwaka 1994 imewateua majaji watatu kusikiliza kesi inayomkabili mtuhumiwa mkuu Felicien Kabuga.


Kabuga (87) alikamatwa Mei 16 mwaka huu akiwa mafichoni katika viunga vya mji mkuu wa Ufaransa Paris baada ya kuepuka vyombo vya sheria kwa miaka 25 na hivi sasa anashikiliiwa huko.


Mchakato wa kumleta Arusha ili kukabili mashtaka ya kufadhili mauaji ya kimbari katika mahakama hiyo yanaandaliwa baada ya mahakama mmoja ya Ufaransa kutoa uwamuzi wa Kabuga kushtakiwa Arusha.


Majaji hao ni Ian Bonomy  kutoka Uingereza, Elizabeth Ibanda-Nahamya (Uganda) na Graciela Susana Gatti Santana, mzaliwa wa Uruguay. Wote wana uzoefu baada ya kuhudumu katika mahakama mbali mbali za kimataifa ya makosa ya jinai.


Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Rais wa Mahakama hiyo (Mechanism) iliyoko Arusha Jaji Carmel Agius imesema imewateua majaji hao kutokana na uwezekano wa Kabuga kuletwa Arusha.


Mahakama ya Ufaransa iliamua wiki iliyopita kwamba Kabuga aletwe Arusha kujibu mashtaka dhidi yake katika mauaji hayo ya kimbari ambapo watu takribani 800,000 waliuawa nchin Rwanda.


Mauaji hayo yaliyolenga zaidi watu wa jamii ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani yalianza baada ya kuuawa kwa aliyekuwa Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana April 6, 1994.


Kiongozi huyo wa Rwanda alifikwa na umauti baada ya ndege yake aliyesafiri nayo kutoka Dar es Salaam kutunguliwa ilipokuwa ikikaribia kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali.


Jaji Carmel amesema akishaletwa Arusha Kabuga atakabiliwa na mashtaka saba yanayohusiana na mauaji ya kimbari, ikiwemo kufadhili mauaji hayo na kuhamasiha maauaji yanayodaiwa yaliwalenga zaidi Watutsi. 


Kabuga amekuwa akisakwa pote duniani tokea Mahakama ya Mauaji ya Rwanda iliyomaliza muda wake (ICTR) ilipotoa hati ya kukamatwa kwake mwezi Novemba mwaka 1997.


Taarifa hiyo ilisema Jaji Kiongozi katika kesi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na wanaharakati mbali mbali duniani, hasa kutoka Rwanda, atakuwa Jaji Bonomy.


Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Mahakama ya sasa ya mauaji ya kimbari Rwanda haikusema Kabuga ataletwa lini Arusha ili kukabili mashtaka hayo.

 

Kabla ya mauaji hayo ya Rwanda yaliyofanyika kati ya Aprili hadi Julai 1994, Kabuga anasemekana alikuwa mtu tajiri kuliko watu wote Rwanda na alikuwa na ukaribu na serikali iliyokuwa madarakani wakati huo.


Tokea hati ya kukamatwa kwake ilipotolewa mwaka 1997, mtuhumiwa huyo amekuwa mafichoni katika nchi mbali mbali licha ya dau la Dola milioni tano za Kimarekani iliyotolewa kwa mtu yeyote atakayemkamata.

 







0 Comments:

Post a Comment