LEMA, NANYARO NA RPC WAVUTANA TUKIO LA POLISI KUVAMIWA NGOME YA CHADEMA ARUSHA

 Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, (RPC), Salum Hamduni

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo,(CHADEMA), kimelaani  hatua ya jeshi la polisi kuvamia ngome yao wanayoitumia kuratibu shughuli za uchaguzi .


Wanadai polisi hao wakiongozwa na mkuu wa Upelelezi wa mkoa, (RCO) hawakufuata utaratibu kisha wakapekua na kuwakamata watu watano akiwemo Kaimu Katibu wa wilaya ya Arusha Mjini, Viola Lokindikoki.




Mwenyekiti wa Chadema, wilaya ya Arusha Mjini, Ephata Nanyaro, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa polisi hao walichukua kompyuta mpakato mbili, kumpyuta ya mezani moja, simu nane za mkononi za hao waliowakamata.

Alisema kuwa polisi walifika kwenye ofisi hizo majira saa 12 jioni ambapo walipotakiwa kutoa hati ya ukaguzi kama sheria inavyowataka walikataa ambapo baada ya mibashano ya mufa mrefu walianza ukaguzi huo kisha kuchukua vifaa hivyo pamoja na watu watano.

Alisema kuwa waliokamatwa mbali na Kaimu Katibu wa wilaya, Likindikoki wengine ni pamoja na mdogo wake Lema, Nelson Lema, Mdogo wa mke Lema,  Wilbert Tarimo, Joshua Lukumay na  Mohames Degera.


"Baada ya mabishano ya muda mrefu huku wakizuia viongozi wetu wa mkoa na mawakili wetu kuingia kwenye ofisi waliamua kutumia ubabe kwa kufanya upekuzi,"alisema Nanyaro na kuongeza.

"Walipoingia kwanza walisema wamekuja kukamata raia wa Kenya, walipokagua wakakuta wote ni raia wa Tanzania wakabadilika wakasema wale watu watano ni watu wa ITatafuta watuhumiwa wanaoingilia mifumo ya kibenki na kuchukua fedha za kusaidia kwenye kampeni za Chadema,".

"Polisi waliofika ni zaidi ya 30, polisi zaidi ya 20 walikuwa na silaha za moto. Ofisi zetu hizi mbili pamoja na eneo la mbele lilikuwa liko chininya polisi kuanzia saa 12 jioni mpaka saa tatu usiku,".

Nanyaro alisema kuwa upekuzi huo haukufuata sheria kwani polisi walikataa kutoa hati ya ukaguzi wala kueleza sababu za ukaguzi.



LEMA ADAI WALIJUA WATAVAMIWA

Kwa upande wake mgombea Ubunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kuwa ofisi hizo wanazitumia kuweka mikakati  juu ya namna ya kuwatoa madarakani wagombea wa CCM kuanzia Rais, wabunge na madiwani.

"Hapa tunafanya digital kampeni, tunawapigia simu wapiga kuta wote tunawaomba kura mmoja mmoja. Tunawapigia tunawaambia wasiwape kura wagombea wa CCM kuanzia Rais, Mbunge na madiwani hii ndiyo kazi tunayofanya hapa," alisema Lema.

Alisema kuwa hata jana jioni ana mikutano ya kampeni kazi kubwa anayoifanya huko ni kuhakikisha wanaitoa madaralani serikali ya CCM jambo alilodai kuwa kitendo cha polisi kuvamia ofisi zao ni kuingilia shughuli za kisiasa.


Alisema Chadema haiweko wahamiaji harama kutoka Kenya wala Israel ambapo polisi walikuta wasaidizi wake  wa viongozi wa chama, vijana wa hamasa pamoja mdogo wake na shemeji yake.

"Baada ya polisi kuchukua simu na kompyuta wamebadilika imekuwa wale waliokamtwa ni wataalam wa IT kutoka Kenya na Israel yaani wale watu wa hamasa wanaozunguka kutangaza mikutano yetu, na Kaimu Katibu wetu, Viola na mdogo wangu na shemeji yangu yaani wamekuja kuingilia mawasiliano ya benki ili kuiba fedha za kuisaidia Chadema na kuja kuingilia mawasiliano ya tume ya uchaguzi," alihoji Lema. 





Lema alisema kuwa inasikitisha sana kuona tokea viongozi na wafuasi wao kupelekwa polisi wamefanya juhudi bila mafanikio kuwaona lakini imeshindikana ambapo mawakili wao wamezuiwa kuonana nao hata waliopeleka chai asubuhi wamenyimwa kuwapatia hivyo hawajala kitu chochote tokea walipokamatwa juzi.





POLISI WAELEZA




Kamanda wa polisi mkoani hapa, Salum Hamduni, alisema kuwa ni kweli walifanya upekuzi kwenye ofisi hizo na wanawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuingilia mifumo ya mawasiliano ya kibenki kwa nia ya kufanya uhalifu.


Alisema watu hao walikamatwa juzi majira ya saa 11:45 jioni kwenye ofisi binafsi za Lema zilizopp mitaa ya ESSO kwenye eneo la jengo la TFA.

"Watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia taarifa fiche kwamba, katika ofisi hiyo kuna watu wanajihusisha na uhalifu wa aina hiyo wakiwemo pia raia wanaodaiwa kutoka nchi jirani, mara baada ya taarifa hiyo askari walikwenda katika eneo hilo lolilopo ndani ya jengo la TFA na kufanikiwa kuwakamata," alisema Kamanda Hamduni.

Hata hivyo alikanusha taarifa zilizotolewa na viongozi wa Chadema kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa chakula kwa kile alichoeleza kuwa viongozi hao wamefanya mawasiliano naye tokea tukio hilo litokee na hawajamweleza.

Alisema kuwa upelelezi unaendelea na ushahidi utakapopatikana utaelekeza hatua gani zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa hao.





1 comment: