BUNGE la nne la Afrika Mashariki huenda likachelewa kuanza shughuli zake kama lilivyopanga kutokana na Kenya kushindwa kufanya uchaguzi wa wawakilishi wake.
Spika wa bunge la tatu lililomaliza vikao vyake juzi, Daniel Kidega alisema kuwa mpaka sasa nchi zote zimeshamaliza chaguzi zake isipokuwa Kenya.
Aliiomba Serikali ya Kenya kuharakisha mchakato wa kuwapata wawakilishi wa Bunge la EALA ili kuwezesha bunge la nne kuanza shughuli zake juni 5, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Spika Kidega alisema atawasilisha jambo hilo kwa uongozi wa EAC, baraza la mawaziri na wakuu wa nchi wanachama kabla hajaondoka kwenye ofisi ili waweze kushughulikia jambo hilo kwani suala la chaguzi hizo haziko kwenye mamlaka yake kama spika.
" Niwasihi Serikali ya Kenya wafanye Uchaguzi mapema hatutaki yajirudie yale yaliyotokea mwaka 2006 ambapo bunge lilichelewa kuanza kwa zaidi miezi sita kutokana na misuguano kwenye uchaguzi wa Kenya," alisisitiza spika Kidega.
Alivipongeza vyombo vya habari kwa ushirikiano walioonyesha wakati wote wa bunge la tatu kwa kuweza kuhabarisha wananchi wa EAC juu ya shughuli zilizokuwa zikiendelea.
Awali jumanne wiki hii bunge hilo lilishindwa kuendelea kwa siku moja baada ya wabunge nane wa Kenya kushindwa kuhudhuria kikao hivyo akidi kushindwa kutimia.
Baadhi ya wabunge walioongea na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao walidai kuwa wabunge hao wako kwenye kampeni za Uchaguzi mkuu nchini mwao.
"Wengine wameenda kufanya "lobbying" ili waweze kuchaguliwa tena kurudi kwa awamu ya pili kwenye bunge la EALA lakini wako wengine wanagombea nafasi za uongozi ndani ya Kenya hivyo wameenda kushughulikia masuala kukamilisha taratibu za tume ya Taifa ya Uchaguzi hivyo isingekuwa rahisi kuhudhuria ,"
alisisitiza mbunge mmoja.
MVUTANO WA VYAMA VYA JUBILEE NA ODM WAELEZWA KUWA CHANZO
Hata hivyo mbunge wa Kenya, Abubakr Ogle, alisema kuwa mchakato wa kupata wabunge wa EALA kutoka nchini Kenya umechelewa kutokana na mivutano iliyopo baina ya vyama vya siasa.
"Sheria iliyopo inasema kwa nafasi moja ulete mpaka wajumbe watatu wa kupigiwa kura, sasa Chama cha Jubilee ambacho kipo madarakani kina nafasi tano kimepeleka majina 15, na ODM wako na nafasi tatu na wiper moja kile walifanya wao walipeleka majina manne tu wenzao wanawaambia wakaongeze yafike 12," alisema mbunge Ogle.
Alisema kuwa hiyo ndiyo sababu kuu ya kuchelewa kwa uchaguzi huo ambao matokeo yake yanaweza kuathiri shughuli za bunge zima la EALA.
0 Comments:
Post a Comment