KURUGENZI YA MAMBO YA NJE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
SERIKALI YA TANZANIA ICHUKUE HATUA ZA HARAKA KUNUSURU
WATANZANIA WAISHIO AFRIKA KUSINI DHIDI YA GHASIA NCHINI HUMO
Kumekuwepo na hali ya raia wa Afrika Kusini kushambulia ,
kujeruhi na kuua raia wa kigeni wa Kiafrika wanaoishi nchini Afrika Kusini.
Hali hii inadaiwa kuchochewa na ukosefu mkubwa wa ajira kwa
wananchi wa Afrika Kusini wanaodai ajira hizo kuchukuliwa na Waafrika wa
mataifa mengine na hivyo wao wenyeji kubakia kwenye dimbwi kuu la umasikini.
Ni mtazamo wa kuimarika kwa kiwango cha umasikini kwa
wananchi wengi nchini humo dhidi ya kuimarika kwa kiwango cha utajiri kwa
wachache kunakopelekea ghasia hizi
Zaidi, mali za Waafrika wageni nchini humo zimekuwa
zikiharibiwa baada ya wamiliki kukoswa
katika mashambulizi hayo.
Aidha, kama nchi nyingine za Kiafrika, Tanzania ina idadi
kubwa ya raia wake wanaoishi nakufanya kazi nchini Afrika Kusini. Na mpaka sasa
inadaiwa kuwa watanzania wawili (2) wameuwawa katika ghasia hizo za wenyeji
dhidi ya Waafrika wageni.
Kwa misingi hiyo:
1.
CHADEMA
inalaani vikali hali ya raia kudhuru na kutwaa uhai wa raia yoyote yule.
CHADEMA kama muumini wa haki za binadamu inayojumuisha haki kuu ya kuishi
inasikitishwa na hali hiyo ya machafuko inayoondoa usalama wa sio tu kwa raia
wa kigeni wa Kiafrika walioko Afrika Kusini bali pia kwa raia wengine wa Afrika
Kusini ambao hawawezi kufanya shughuli zao kwa ukosefu wa usalama nchini humo.
CHADEMA inawasii raia wa Afrika
Kusini kuwachukulia Waafrika wenzao kutoka mataifa mengine kama ndugu zao ambao
kwapamoja walishrikiana kupambana na ubaguzi wa rangi na hatimaye kuleta uhuru kwa taifa hilo. Ni muhimu raia wa
Afrika Kusini wakatatua matatizo yao ya ndani
hasa ya kiuchumi kwa kushirikina na wenzao wa mataifa ya Afrika waishio
nchini humo na si kuwaona kama maadui zao.
2.
CHADEMA
inaitaka serikali ya Tanzania ishirikiane na serikali ya Afrika Kusini kuchukua
hatua za haraka kunusuru maisha ya watanzania waishio nchini Afrika Kusini
dhidi ya ghasia hizi kwa kuwahakikishia usalama wao ama kuwawekea utaratibu wa
kuondoka ama nchini humo na kurejea nyumbani ama kwenye miji yenye machafuko
kama Durban na kuwapeleka kwenye miji ya usalama zaidi mpaka hali
itakapotengamaa kwenye miji hiyo kama ilivyofanya kwa Watanzania waishio Yemen
ambako nako machafuko yamekithiri. Ni muhimu Serikali ikawa makini kwa jambo
hili kwani teyari mataifa mengine ya kiafrika ya Botswana, Malawi na Zimbabwe yaneshaanza
kuwaondoa raia wake nchini humo kwa kuhofia usalama wao.
3.
CHADEMA
inazikumbusha nchi za Kiafrika ambazo zina utajiri mkubwa wa rasilimali kuhakikisha
inatatua matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo ikiwa ni pamoja na
kupunguza tofauti ya kipato kati ya wengi wasio nacho na wachache wenye nacho.
Ni muhimu serikali hizi kujikita
katika kupambana na umasikini kwa kutengeneza fursa za ajira kwa raia wake na
hivyo kupunguza kiwango cha umasikini na hatimaye kuondoa mazingira ya
machafuko yanayosababishwa na hasira za wananchi kutokana na hali yao ya
umasikini.
Kwa mantiki hiyo, ni muhimu Jumuiya
za kikanda na Umoja wa Afrika wenyewe (AU) zikaweka msisitizo wa ukombozi wa
kiuchumi unawaweza kukidhi haja na matakwa ya raia wa bara hili.
4.
Kipekee,
CHADEMA inaikumbusha serikali ya Tanzania kuichukilia hali ya Afrika Kusini
kama taadhari kwake kwani hali ya
umasikini na ukosefu wa ajira hapa nchini imekuwa kubwa kiasi cha kuibuka kwa
vikundi vya kihalifu vya Komando Yoso na Panya Road vilivyofanya mashambulizi
na uporaji kwa raia wengine. Tofauti ndogo iliyopo kati ya Afrika Kusini na
Tanzania ni kwamba Afrika Kusini raia wazalendo wanashambulia waafrika wa
mataifa mengine wakati hapa Tanzania ilikuwa ni kushambuliana baina ya
Watanzania.
Imetolewa leo tarehe 18.04.2015 Jijini Dar es salaam na;
Deogratias Munishi
Mkuu wa Mambo ya Nje – CHADEMA
+255715887712
0 Comments:
Post a Comment