Homa ya mapafu ni aina ya maambukizi
yanayoathiri mapafu. Ni ugonjwa ambao
unaua watoto wengi hasa katika nchi
zinazoendelea duniani. Inakadiriwa
kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio
chini ya miaka 5 wanakufa kila mwaka
kutokana na ugonjwa huu. Kutokana na
vifo vingi vinavyotokana na homa ya
mapafu tarehe 12 ya mwezi wa Novemba
kila mwaka imefanywa kuwa siku rasmi
ya homa ya mapafu duniani, ambapo
nembo ya siku hiyo ni nguo za rangi ya
bluu.
Muundo wa Mapafu
Mapafu yanajumuisha mirija mikubwa ya
hewa ( bronchi) ambayo hugawanyika
kufanya mirija midogo zaidi ya hewa
(bronchioles ), ambayo nayo hutengeneza
vifuko vidogo vidogo ya hewa ( alveoli ).
Vifuko hivi vidogo vya hewa (alveoli ) vina
mishipa ya kupitisha damu (capillaries )
ambayo husaidia kuchuja na kusafirisha
hewa safi ya oksijeni tunayovuta kuingia
kwenye damu na hewa chafu ya ukaa
(kaboni dioksidi) kuondolewa kwenye
damu na kuingizwa kwenye mapafu tayari
kwa kutolewa nje ya mwili.
Kwa kawaida vifuko hivi vidogo hujaa
hewa muda wote tayari kwa kusafirishwa.
Inapotokea mtu akapata homa ya mapafu,
vifuko hivi hujaa maji au usaha hivyo
kuathiri upitishaji wa hewa safi kwenye
damu na kusababisha tatizo la kupumua.
Homa ya mapafu husababishwa na nini?
Kuna aina kadhaa ya vimelea ambao
vinaweza kusababisha maambukizi ya
mapafu. Vimelea hivi hujumuisha bakteria,
virusi, parasite na fangasi.Vimelea hawa
hushambulia mwili wa binadamu
kulingana na umri na kinga ya mwili. Kwa
mfano, bakteria wanaosababisha homa ya
mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na
wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa
watoto wakubwa .
Baadhi ya vimelea wa bakteria
wanaoshambulia watoto ni pamoja
na Streptococcus pneumoniae ambao ni
aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha
homa ya mapafu kwa watoto. Wapo
pia Haemophilus influenzae aina b (Hib)
ambao ni aina ya pili ya bacteria walio
maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa
wa homa mapafu kwa
watoto. Staphylococcus aureus ni aina
nyingine ya bacteria ambao hushambulia
zaidi watoto wachanga. Kuna pia Group
B streptococci ambao pia hushambulia
zaidi watoto wachanga.
Kwa upande wa virusi, virusi wa aina
ya Respiratory syncytial virus ndiyo
wanaoongoza kwa kusababisha homa ya
mapafu kwa watoto.
Aidha, vimelea wa Pneumocystis
jiroveci ambao kwa sasa huwekwa kwenye
kundi la parasite ni maarufu zaidi
miongoni mwa parasite wanaosababisha
homa ya mapafu kwa watoto wenye
upungufu wa kinga mwilini hususani
watoto wenye VVU.
Aina nyingine za bakteria ambao
hushambulia zaidi watoto wakubwa ni
pamoja na Mycoplasma
pneumonia na Chlamydia pneumonia.
Jinsi Homa ya Mapafu inavyoenezwa
Kuna namna nyingi za kuenea kwa homa
ya mapafu. Kwa kawaida, virusi na
bacteria hupatikana katika sehemu ya juu
ya mfumo wa njia ya upumuaji (upper
respiratory tract ). Inapotokea kinga ya
mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu
yeyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa
na kufika mpaka sehemu ya chini ya
mfumo wa njia ya upumuaji (lower
respiratory tract ) na hatimaye
kushambulia mapafu. Hali kadhalika,
vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia
ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto kabla ya kuzaliwa yaani kipindi cha
mimba.
Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu
Dalili za vichomi au homa ya mapafu kwa
watoto hutegemea na umri wa mtoto. Kwa
watoto wadogo, dalili za awali zinaweza
kuwa homa kali pamoja na mtoto
kuhangaika na kunyong'onyea. Watoto
wanaozaliwa wakiwa na uambukizi wa
bacteria aina ya Streptococcus kundi B
wanaweza kuwa na homa na kupumua
kwa shida. Wakati mwingine mtoto
anaweza kuwa na dalili ambazo si maalum
(no-specific symptoms) kama vile
kuhangaika na kushindwa kunyonya au
kula vizuri bila kuwa na dalili yeyote ya
kushindwa kupumua. Hali hii inaweza
kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.
Dalili za kawaida za homa ya mapafu
ambazo huwapata karibu watoto wote
wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja
na:
homa
Kuhisi baridi
kikohozi
Kupumua kwa haraka kuliko kawaida
kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa
kupumua
Mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa
kupumua
maumivu ya tumbo
kupoteza hamu ya kucheza
kupoteza hamu ya kula na kushindwa
kunyonya
Mtoto kubadilika rangi na kuwa na rangi
bluu katika midomo na kucha
Hata hivyo, si lazima dalili zote hizi
ziwepo kwa kila mtoto. Baadhi ya watoto
huonesha kupumua kwa haraka kama
dalili pekee ya homa ya mapafu. Iwapo
vimelea vimeshambulia sehemu za chini
ya mapafu karibu ya tumbo, sehemu
ijulikanayo kama kiwambo au diaphragm,
mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya
kushindwa kupumua ingawa anaweza
kuwa na homa na kujihisi maumivu
makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika.
Watoto wachanga wanaweza kushindwa
kunyonya, na pia kupoteza fahamu na
kupata degedege.
Vihatarishi vya homa ya mapafu (risk
factors)
Katika hali ya kawaida kinga ya mtoto
mwenye afya njema humlinda
asishambuliwe na vimelea
vinavyosababisha magonjwa mbalimbali.
Hali huwa ni tofauti pale ambapo kinga ya
mtoto ni ndogo au dhaifu, kwa vile mfumo
mzima wa ulinzi huathirika na hivyo basi
inakuwa ni rahisi kwa mtoto kupata homa
ya mapafu.
Mfumo wa kinga wa mtoto unaweza kuwa
dhaifu kwa ukosefu wa lishe bora hasa
kwa watoto wachanga ambao
hawanyonyeshwi ipasavyo. Aidha uwepo
wa magonjwa mengine, kwa mfano,
maambukizi ya VVU, saratani na ugonjwa
wa Surua hupelekea kinga ya mwili kuwa
dhaifu.
Lakini vile vile kuna mazingira
yanayoweza kusababisha mtoto kuwa
katika hatari ya kupata homa ya mapafu
mfano moshi wa sigara, au moshi ndani
ya nyumba unaosababishwa na kupikia
kuni au mkaa. Vilevile msongamano ndani
ya nyumba kutokana na watu kuwa wengi
sehemu moja nayo huweza kusababisha
watoto kupata homa ya mapafu.
Uchunguzi na Vipimo
Daktari humchunguza mtoto mgonjwa kwa
kusikiliza dalili za ugonjwa kutoka kwa
mzazi/mlezi wa mtoto, kuchunguza
viashiria vya ugonjwa huu na kisha
kumpima mtoto kwa kutumia kifaa
kinachosaidia kusikia sauti mbalimbali
katika mfumo wa hewa wa mgonjwa
kiitwacho stethoscope.
Ili kujiridhisha na kuwa na uhakika wa
tatizo hili, vipimo vifuatavyo vinaweza
kufanywa kulingana na mazingira na
upatikanaji wake. Vipimo hivyo ni pamoja
na X-ray ya kifua, au CT-scan ya kifua,
pamoja na damu ili kuchunguza madhara
yaliyoletwa na homa hii ya mapafu.
Faida ya kipimo cha CT-scan ni ule uwezo
wake wa kutofautisha aina tofauti za homa
ya mapafu na aina ijulikanayo
kama Atypical pneumonia ambayo si rahisi
kuonekana kwa kutumia X-ray ya kawaida
ya kifua. X-ray ya kifua na CT-scan ya
kifua kwa pamoja vina uwezo wa
kuonesha tatizo hata pale ambapo daktari
ameshindwa kusikia sauti maalum kwa
kutumia kifaa chake cha stethoscope.
Matibabu
Maamuzi ya Matibabu kwa watoto wenye
homa ya mapafu hutegemea aina ya
vimelea, umri na hali ya mtoto. Mara
nyingi antibiotics ndizo hutumika katika
kutibu homa ya mapafu inayosababishwa
na maambukizi ya bakteria. Kwa homa ya
mapafu inayosababishwa na virusi,
antibiotics hazina uwezo wowote wa
kutibu. Ieleweke kuwa ni tabibu
anayeweza kufahamu kama mtoto wako
anahitaji antibiotics au dawa za aina
nyingine, kwahiyo ni muhimu kwa mzazi
ama mlezi kumpeleka mtoto hospitalini
haraka pindi mtoto anapoonesha dalili za
ugonjwa huu badala ya kuamua kumpa
dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu
wa afya.
Namna ya kuzuia Homa ya mapafu
Homa ya mapafu inaweza kuzuiwa kwa
chanjo, lishe bora na ya kutosha na mtoto
kuishi katika mazingira yenye hewa safi.
Kuzuia homa ya mapafu kwa watoto ni
sehemu muhimu ya mkakati wa Taifa wa
kupunguza vifo vya watoto. Chanjo dhidi
ya Hib, pneumococcus, surua na kifaduro
ni njia mojawapo ya kuzuia homa ya
mapafu.
Lishe ya kutosha ni muhimu kwa
kuboresha kinga ya mwili ya mtoto
ambapo inashauriwa mama kunyonyesha
mtoto bila kuchanganya na kitu chochote
walau kwa miezi sita ya mwanzo ya
maisha yake.
Kuhimiza usafi katika makazi kama
kutotumia jiko la mkaa au kuni ndani ya
nyumba na uvutaji wa sigara ni jambo
linaloshauriwa pia. Hii inasaidia
kupunguza idadi ya watoto kupata homa
ya mapafu. Kwa watoto wenye VVU,
matumizi ya dawa ya cotrimoxazole kila
siku husaidia kupunguza uwezekano wa
kupata homa ya mapafu.
Utafiti umeonyesha kwamba kinga na tiba
sahihi ya homa ya mapafu inaweza kuzuia
vifo milioni moja kwa watoto duniani kila
mwaka. Hivyo ni wajibu wetu sote
kushirikiana kupambana na ugonjwa huu
wa homa ya mapafu

0 Comments:

Post a Comment