Ndg. wanabodi,
Sikuwahi kujua kuwa na hapa kulipita mjadala
uliohusu matibabu ya mzazi wangu.
Nimeambiwa kuwa mjadala huu umekuwa
ukififia na kuibuka mara kwa mara. Nimeona
leo niibuke mwenyewe na kusema kidogo
kuhusu hili. Huko nyuma sikuwahi kuona haja
ya kuhangaika kujibu chochote juu ya hili
kwa sababu halina ukweli wowote ule na
halina tija yoyote ile kwenye kazi niliyopewa
na wanaNzega na waTanzania kwa ujumla.
1. Mzee anliyehojiwa ni Baba yangu Mzazi,
sikuwahi kumjua vizuri wakati wa utoto
wangu ninapopata ufahamu na kumbukumbu,
lakini nilipokuwa nakua nilitamani sana
kumjua Baba yangu. Nakumbuka kukutana na
Baba zangu wadogo na wakubwa, mashangazi
zangu na marafiki zake, na 'nikiambiwa kuwa
nafanana sana na baba yangu, na kwamba
nina akili kama Baba yangu', na kwamba
nitakuwa msomi kama Baba yangu!
Niliendelea kusoma nikijiamini kwamba
nitafika mbali kwa kuwa 'nina akili' sana
'kama baba yangu' - walau hili lilinipa
inspiration ya kukomaa na shule. Nilipofaulu
kidato cha sita, nilipata taarifa kwa baadhi ya
ndugu kuwa Baba yangu amerejea nchini
kutoka 'majuu' alikokuwa akiishi...kuanzia
Mississipi, India, Pakistan na Dubai...huko
alikula ujana wake wote! Mimi sikuwahi kuwa
sehemu ya mafanikio au maanguko yake enzi
za nguvu zake, maana hakunilea, wala
hakuwahi hata siku moja kunitumia chochote
kutokea huko 'majuu'. Hata aliporudi
hakuwahi kunitafuta wala kujali kuwa nipo
wapi, nafanya nini, mpaka nilipomtafuta!
Nichukue fursa hii kumshukuru Mungu kwa
kunijaalia uzima, hekima, busara, ufahamu na
kunipa walezi wenye upendo na hekima ya
kutambua umuhimu wa elimu na malezi bora
kwenye maisha ya mtoto. Hawa ni Bibi yangu
Bi. Mtumwa Kibwana Jaffar na Babu yangu
Sheikh Bakari Maulid Lumola (Mungu awalaze
mahala pema peponi) wa umamani kwangu;
pia mama zangu wadogo, wajomba zangu na
walimu wangu. Siwezi kuisahau nafasi ya
kipekee ya Mama yangu mzazi, Bi. Bagaile
Bakari Lumola, kwa upendo usiokadirika na
kwa kuninunulia vitabu vya kujisomea
nyumbani, kuhakikisha navaa na kula vizuri
kwa kuhangaika hadi kufikia kuwa 'mama
ntilie' kwenye migodi ya Isungangwanda,
Bulyanhulu na Bulangamilwa, ikizingatiwa
kuwa Baba yangu alimuachisha kazi yake ya
ualimu ili amfuate Kigoma alipohamishiwa
kikazi (baba alikuwa benki ya NBC ya enzi
hizo) akiwa na ujauzito wangu. Walipoachana,
Baba yangu aliondoka na vyeti vyote vya
mama na hakurudi hadi hapo nilipokutana
naye - wakati nimemaliza Form Six na tayari
nikiwa nimefaulu Div I yangu nzuri ya PCB,
naenda kuanza masomo ya Doctor of
Medicine!
2. Nampenda na kumthamini Baba yangu
mzazi, kwa kuwa alimuoa Mama yangu,
alinizaa na alitutelekeza hadi mdogo wangu
Bakari akakumbwa na kifo (kwa sababu ya
maradhi na shida na umaskini uliopindukia!)
akiwa mdogo; kwa sababu kututelekeza kwake
kumenipa fundisho kubwa sana katika maisha
yangu - kumenipa hekima ya kuifahamu
shida, njaa na ukandamizaji, na namna
ambavyo sote tunawajibika kupigana navyo;
kumenifundisha kuitambua nafasi ya
mwanaume kwenye maisha ya mtoto na
ujenzi wa jamii imara ndani ya nchi na dunia
pana, na zaidi nafasi ya mama kwa mtoto, na
umuhimu wa 'extended family' kwenye jamii
ya kiafrika. Ninaujua udugu na thamani na
umuhimu wake. Nampenda zaidi Baba yangu
kwa kuwa ni mtu aliyejirekebisha na
aliyemrejea Mungu wake. Nampenda kwa
kuwa amenifundisha niwe Baba mzuri na
anayejali maisha ya watoto wake na
kuthamini unit ya familia. Binafsi, naamini
kila kitu kinatokea kwa sababu. Pengine
ningepewa kila kitu kama watoto wengine wa
wazazi waliosoma miaka ya sitini na sabini,
kama Baba yangu, nisingekuwa hivi nilivyo
leo, pengine nisingefika hata hapa nilipofika.
Ninaamini Mungu alinileta duniani kwa
sababu na ninaamini naendelea kuwepo hapa
duniani kwa sababu ambazo anazijua zaidi
yeye, siwezi kumlaumu Baba yangu kwa
lolote. Naweka sawa tu haya mambo, yawe
fundisho kwetu sote. Sijawahi kumtelekeza na
kamwe siwezi kufanya hivyo maana walionilea
walifundisha dini na kufahamu umuhimu wa
wazazi na wanadamu wengine katika maisha
haya na ya kesho akhera. Wazazi wana hadhi
kubwa sana kwa Mungu juu ya mtoto wao.
Naitaka pepo ya Mungu na hivyo nitagalagala
miguuni pa wazazi wangu siku zote za maisha
yangu! Baba yangu amebadilika sana siku
hizi, haswa toka augue, nadhani amekuwa na
sahau ya kupindukia! Mbona hakuwaambia
kuwa nilimuwekea biashara ya 'bodaboda' ili
kila siku ajipatie hela ya kula? Maana
ninabanwa sana na majukum ya kazi zangu
kiasi cha kukosa muda wa kusimamia malezi
hata ya wanangu mwenyewe...muda
haunitoshi kabisa! Nilidhani kumuwekea
sehemu ya matibabu ya uhakika ilitosha,
kumbe alitamani nimtembelee kila mara.
Baba yangu anatibiwa HEAMEDA Medical
Clinic (ya Dr. Heri Mwandolela, Daktari
Bingwa wa Moyo, rafiki yangu), iliyopo eneo
la Scout na pia Muhimbili kwa Dr. Tulizo
Shemu (rafiki yangu, daktari bingwa wa
moyo) - kote huku anatibiwa kwa 'bill'
ninazolipa mimi. Ukiangalia hizo video
utaona anaonesha vipimo vya gharama sana
alivyofanya kule Regency, Aga Khan, MNH -
mtu mwenye akili atajiuliza: Mzee Kigwangalla
anasema hana hela za kula, alitoa wapi hela
za hivyo vipimo vyote kama si mimi
niliyemlipia? Kwa nini huyo kijana hakumhoji
ni nani aliyegharamia hivyo vipimo? Ni
Daktari gani anayemuona na nani alimpeleka
huko? Na analipaje gharama za vipimo hivyo?
Ni kwa nini huyo kijana alikuwa
anang'ang'ania kuuliza kuhusu Uraia wangu,
majina yangu na elimu yangu kama lengo
lilikuwa kumsaidia Baba yangu kupata fedha
za matibabu? Ni kwa nini mpaka leo
hawajampelekea Mzee huyu fedha
walizokusanya kutokana na harakati zao za
kutafuta msaada wa matibabu yake?
3. Namshukuru Mungu, matibabu ya Baba
yangu yanaendelea vizuri, na barua za rufaa
zimeishaandikwa, muda si mrefu nitampeleka
India kwa ajili ya matibabu. Kuna watu
waliingilia 'maisha binafsi' ya mimi na familia
yangu kwa sababu za kisiasa kwa malengo ya
kunichafua na kuniharibia haiba na
muonekano wangu kwenye jamii, wakimlaghai
kuwa watamsafirisha kwenda nje ya nchi
kwenye matibabu; hakuna hata mmoja wao
aliyeenda kumuona kumjulia hali achilia
mbali kumchangia hata shilingi 10,000 ya
matibabu hadi leo hii! Haya ya kwangu
yanaelezeka, ya kwao na familia yao
yamegubikwa na aibu na kashfa nzito. Mimi
sijawahi kuhangaika nayo na sintoyatumia
kisiasa kwa malengo ya kumchafua mtu kwa
minajili ya kulipiza kisasi. Aliyefanya kazi hii
aliona ni bora atoe shilingi milioni 3 kwa
waliotengeneza video hii badala ya kuwasaidia
chakula wazazi wake wanaoishi kidhalili zaidi
hata ya wazazi wangu! Mungu atawalipa
stahili ya chuki na ubaya wanaohangaika
kunifanyia, amina. Kamwe sintowalipizia ili
wauone utofauti na utukufu wa Mungu.
Harakati za kutafuta uongozi siyo vita ya kufa
ama kupona kiasi cha kusahau hata udugu
wetu kama wanadamu, na Utaifa wetu kama
waTanzania.
4. Mama anayehojiwa hapo si mama yangu
mzazi, ni mama, mke wa Baba yangu. Mama
yangu mzazi ni mtumishi wa CCM wilayani
Uyui, Tabora. Ninamjengea nyumba huko
huko Tabora, na nimemnunulia gari ya
kuendea kazini ili astaafu vizuri.
5. Naomba mnisamehe kwa kuchelewa kutoa
majibu yangu juu ya jambo hili. Sikuona haja
ya kushughulika na 'ki-mbwa koko'
kilichotumwa kubweka, maana nilijua
kimetumwa tu na kinatekeleza majukumu ya
bwana'ke, na zaidi nilijuwa kinategemea
malipo ya mifupa na makombo ya mwenye
mbwa; nilitamani 'mwenye mbwa' mwenyewe
ajitokeze apambane nami hadharani kama
yeye kweli ni Mwanaume wa shoka! Na zaidi
sikuona haja ya kushughulika na upuuzi huu
ilhali nina mambo mengi yanayopaswa
kushughulisha akili yangu jimboni na Taifani
kwa ujumla.
6. Nitafanya mkutano na waandishi wa habari
ndani ya siku si nyingi kuhusiana na tetesi
zilizozagaa nchini kuhusu kama nimefanya
uamuzi wa kugombea Urais 2015 ama la,
atakayeona anahitaji ufafanuzi zaidi afike na
atapata majibu ya maswali yake ya ziada
hapo.
Wakatabahu,
HK.
laana ya mzazi mbaya sana, fatilia kwenye link hii chini. .
http://www.youtube.com/v/d4XCnJ53CRw
AMVUNJA MBAVU MKE WAKE KWA WIVU WA MAPENZI
-
Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi linamsaka Hamidu Abdalah kwa kosa la
kumjeruhi kwa kumpiga na chaga ya kitanda mke wake Amina Athuman Said 40,
mkazi wa Likon...
4 hours ago
0 Comments:
Post a Comment