MUFTI na Shekh Mkuu Nchini, Shekh Issa Bin Shaaban Simba, ameingilia kati mgogoro wa kiuongozi uliodumu ka muda mrefu mkoani hapa kwa kuamua kutangaza viongozi halali wa Bakwata kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya ya Arusha na misikiti ya Ijumaa, Bondeni na Masjidi Quba.
Alitangaza majina ya viongozi hao Julai2,mwaka huu akiwa ameambatana na viongozi wa Bakwata pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapa ambapo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, alimwakilisha Mkuu wa mkoa.
Mufti Simba alisema kuwa mgogoro wa kiuongozi uliokuwepo ulisababishwa na ukaidi wa makusudi wa baadhi ya watu walioamua kukiuka taratibu za kuweka viongozi kama ulivyoainishwa na katiba ya Bwakwata.
"Hali hii imepekelea kuwa na makundi mawili ya uongopzi katika ngazi ya mkoa, wilaya ya Arusha, Msikiti Mkuu wa Ijumaa na Masjid Quba jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya uislam mkoani Arusha," alisema Mufti Simba.
Alisema kuwa kwa mujibu wa katiba ya Bakwata ya mwaka 1999 toleo la 2008 ibara ya 10 kwenye muundo wa uongozi inaeleza wazi kuwa kutakuwa na viongozi wa kuchaguliwa isipokuwa nafasi za makatibu wa wilaya na mikoa ambao wao watateuliwa na katibu Mkuu wa Bakwata.
Aliowatangaza kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ni pamoja na Mwenyekiti wa Bakwata Mkoa,Shekh Shaaban Juma Abdala, Katibu wake, Ustadhi Abdallah Masoud na Mwenyekiti wa Halmashauri, Ustadhi Mohamed Juma Marawi.
Mufti Simba alitaja wajumbe watano wa baraza la mkoa, Wajumbe nane wa Halmashauri ya Bakwata mkoa, viongozi wa Bakwata wilaya ya Arusha pamoja na wajumbe wa halmashauri ya Bakwata wilaya na wale wa mamlaka ya msikiti mkuu wa Ijumaa Arusha Mjini.
Pia alichagua wazee watano wasuluhishi wa migogoro misikitini pamoja na uongozi wa Masjid Quba wa levelosi.
APINGWA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa, Abdulazizi Mkindi akiongea mara baada ya Mufti Simba kutoa msimamo huo alisema kuwa uongozi uliotangazwa jana ni batili hivyo yeye ataendelea kuuongoza msikiti huo mpaka shauri lao lililopo mahakamani lkitakapomalizika.
"Siwezi kuingilia mwenendo wa kesi iliyo mahakamani, nachowaomba waumini wa kiislam mkoani Arusha wawe na subira kwa sababu masuala haya yako mahakamani na mahakama ndiyo chombo pekee cha kupata haki hapa nchini hivyo tusubiri uamuzi," alisisitiza Mkindi.
Kiongozi mwingine, Shekh, Mustafa Kiligo, alisema kuwa Mufti ameshauriwa vibaya na wasaidizi wake kuingilia suala hilo ambalo liko mahakamani huku akisema kuwa wao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida ikiwemo kuswalisha ibada kwani uongozi uliotangazwa ni batili.
"Uamuzi huu wa Mufti ni batili, viongozi aliowatangaza ni batili, kuna 'order' ya mahakama hii hapa, sisi tutaendelea kuongoza ibada pale msikitini mpaka shauri liishe mahakamani," alisema Shekh Kiligo.
Zuio waliloonyesha kwa waandishi limesainiwa na mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la wilaya ya Arusha, C P Kamugisha Machi 21, mwaka huu kupitia maombi namba 43 la mwaka 2014.
0 Comments:
Post a Comment