MFANYAKAZI wa kampuni ya simu ya Tigo, (MIC T LTD), jijini hapa, Mwita Makore, amekutwa amekufa nyumbani kwake maeneo ya Kimandolu huku akiwa na kamba za viatu viatu shingoni kuashirikia alijinyonga nazo na kujitundika kwenye bomba la bafuni kwake.
Hali hiyo imezua gumzo miongoni mwa wakazi wa jijini hili wakihoji inawezekanaje mtu kujinyonga kwa kamba ya viatu hadi kufa huku wengine wakihoji uwezekani wa mwili wa mtu mzima kuweza kuning'inia kwenye bomba ya bafuni.
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa mwili wa Makore ambaye alikuwa kitengo cha 'store' ulibainika Juni 20,mwaka huu baada ya Mwita kutoonekana wala kupatikana kwa simu zake za kiganjani kwa siku mbili mfululizo hali iliyowalazimu wafanyakazi wenzake kwenda kumtafuta nyumbani kwake ndipo wakabaini kafa.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo jijini hapa aliyeongea kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini alisema kuwa mara ya mwisho Makore kuingia ofisini ilikuwa ni juni 18, mwaka huu (jumatano iliyopita).
"Unajua yeye kazi yake haimlazimu kuwa ofisini muda wote hivyo akishamalizana na wateja wake huondoka, hivyo siku ya alhamisi hakuja kabisa ofisini lakini hakuna aliyekuwa na wazo kuwa kakutwa na jambo baya.
"Alikuja mteja anayehitaji vocha, ikabidi apigiwe simu, simu ikawa inaita haipatikani, siku inayofuata wakaja wateja wengine, Mwita akapigiwa simu zake zikawa zinaita tu lakini hazipokelewi.
"Yule mteja akachukia akaamua kupiga simu makao makuu kueleza usumbufu anaoupata ndipo nao wakawapigia viongozi hapa wakawaeleza kama hapokei simu kwa nini wasimfuatilie nyumbani kwake pengine amepata matatizo," alisema mfanyakazi huiyo.
Alisema kuwa walipofika nyumbani kwake walikuta gari ya kampuni ya Tigo ikiwa imeegeshwa vizuri lakini funguo zake ziko ndani na milango imerejeshewa tu huku kwenye mlango wa kuingia ndani kwa Makore kukiwa na viatu vyake ambapo walipopiga simu zake wakasikia zikiita kutoka ndani ndipo wakaingia ndani.
"Tulipoingia pale mezani tulikuta kuna chupa ya soda, na simu zake tatu pamoja na kadi zake za benki tukaendelea kuangalia maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo ndipo tukamkuta Makore bafuni na kamba ya viatu shingoni'" alisema Mfanyakazi huyo wa Tigo.
Mwananchi mwingine anayeishi maeneo ya Kimandolu alisema kuwa tukio hilo limewashangaza sana kwani marehemu walikuwa wakimuona ni kijana mtaratibu asiyekuwa msemaji ila alikuwa mpenzi wa mchezo wa Pool table.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa kifo hicho alichodai ni cha kawaida kwani amekutwa amekufa nyumbani kwake na hakuna mahali palipovunjwa.
"Achana na habari za barabarani, amekutwa amekufa nyumbani kwake hakuna mahali pamevunjwa hiyo ni 'natural death' ," alisema Sabas wakati Tanzania Daima ilipokuwa ikimweleza kile kinachoelezwa na majirani pamoja na wafanyakazi wenzake.
Kwa upande wake,Meneja Mauzo wa Tigo mkoani hapa, Aidan Komba, alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwani licha ya kuwa kwa sasa bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo lakini pia kwa utaratibu wa kampuni yao atakayelizungumzia suala hilo pindi wakipata taarifa rasmi ya polisi ni msemaji wa kampuni ambaye yupo jijini Dar es Salaam.
"Mwili wake umefanyiwa uchunguzi jana (jumanne) ndipo ukasafirishwa kwa maziko nyumbani kwao Rorya (Mkoani Mara) hivyo bado hatujapewa taarifa yoyote, lakini hata zikipatikana taarifa itatolewa na msemaji wa kampuni ambaye yuko Makao makuu Dar, hivyo kwa sasa tunasubiri polisi wamalize uchunguzi wao," alisema Komba.
MWISHO
0 Comments:
Post a Comment