MKUTANO WA AFRIKA MASHARIKI KUJADILI AMANI

Grace Macha na Mayalla wakifuatilia kwa makini mkutano huu ili kuweza kuhabarisha ipasavyo
Mwenyekiti wa kamati  ya mahusiano na utatuzi wa migogoro, bunge la Afrika Mashariki, Abubakar Zein, (Kenya) akifuatilia mjadala.
Washiruiki ambao ni wenyeviti wa kamati mbalimbali za bunge la EALA, wawakilishi wa serikali toka nchi wanachama na wataalam wa EAC na wale kutoka taasisi za kimataifa wakifuatilia mjadala.

TAASISI za usalama za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC), zimetakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana huku wakitumia mfumo wa kisasa wa sayansi na teknolojia katika kupeleleza ili kudhibiti matukio ya uhalifu ambayo kutokana na kuongezeka kwa mtangamano wa wananchi kwa kurahisisha mwingiliano kwenye mpaka na wahalifu nao hupita kwa urahisi.
 
Aidha imeelezwa kuwa nchi nyingi za EAC zimepakana na nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ambayo iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe hali inayopelekea kuongezeka  kwa matukio ya uhalifu ikiwemo upitishwaji wa pembe za ndovu na usafirishaji wa madawa ya kulevya kutoka nchi hiyo sanjari na wizi wa magari kutoka nchi wananchama ambayo hupelekwa Kongo.
 
Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Mtaalam wa masuala ya usalama wa EAC, Dkt. Leonard Onyonyi, wakati alipokuwa akielezea hali ya usalama kwenye ukanda wa jumuiya hiyo kwenye mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na kamati ya mahusiano na utatuzi wa migogoro ya  bunge la Afrika Mashariki na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.
 
Alisema kuwa katika kuhakikisha eneo la EAC linakuwa salama ni vema nchi wanachama zikaelimisha wananchi wake kuelewa na kujua wajibu wa kulinda usalama ni wa kila mmoja na si kuachiwa serikali pekee ambazo nazo zimeshauriwa kutumia wataalam na vifaa vya kisasa katika kukabiliana na matukio hayo.
 
Dkt. Onyonyi alisema kuwa mifumo ya kudhibiti matukio ya utakasaji fedha  haramu ni vema ikaboreshwa ili iweze kufanya kazi ipasavyo ya kuzuia na kubaini matukio hayo huku akitolea mfano kuwa tayari imejulikana kuwa soko kuu la meno ya tembo liko nchini China lakini bado haijajulikana malipo yanafanyikaje jambo alilodai kuwa huenda hufanyika kwa kupitia bidhaa zinazokuja kwenye ukanda huu kwa makontena jambo ambalo huzitakasa fedha hizo.
 
Akiongelea tatizo la kuongezeka kwa matukio ya usafirishaji wa madawa ya kulevya huku akitolea mfano kiwango kikubwa kilichofanikiwa kukamatwa kwenye nchi za Tanzania na kenya, mtaalam huyo alisema kuwa mbali na kuwa eneo la EAC kuwa njia ya kuyapitisha kwenda mabara mengine lakini soko la ndani pia limekuwa likiongezeka ambapo waathirika wakuu ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.
 
Alisema kuwa kwenye ukanda huu wa EAC matukio ya usafirishaji wa binadamu yamekuwa yakijitokeza hasa wale wanaotolewa vijijini kupelekwa maeneo ya mijini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na wengine kufanyishwa biashara ya ngono, (ukahaba).
 
Awali Mwenyekiti wa makati hiyo ya bunge, Abubakar Zein, (Kenya), alisema kuwa waliamua kuandaa mkutano huo kutokana na umuhimu wa amani katika suala zima la maendeleo kwa kile alichodai kuwa mambo hayo mawili yanategemeana kwani huwezi kuwa na amani kama hakuna maendeleo na hauwezi kuwa na maendeleo kama hauna amani.
 
Alisema kuwa mkutano huo umelenga kujua chanzo cha migogoro kwenye ukanda huu ili kujenga misingi ya kitaasisi kuitatua na kuhakikisha haitokei jambo alilodai kuwa watafanikiwa kwani kwenye mkutano huo kuna wataalam wakiwemo watafiti wa masuala ya migogoro, watunga sera ambao ni wabunge na wawalikishi wa serikali toka nchi zote tano.
 
Zein alisema kuwa wanalenga kuhakikisha kunakuwa na sera ya usalama ambayo baadaye itatungiwa sheria ili kuhakikisha wananchi wote wa EAC wanashiriki kulinda amani ambapo alisema kuwa mkutano huuu ulitanguliwa na ule wa waandishi wa habari uliofanyika nairibi Nchini Kenya ambapo baada ya huu kutakuwa na mkutano mwingine utakaowakutanisha wabunge wa nchi wanachama wa jumuiya hii.

Sent from my iPhone

0 Comments:

Post a Comment