Anguko la Joyce Banda


Rais Joyce Banda


SIRI ya kuanguka kwa Rais wa nchini hapa, Joyce Banda, zimeanza kuvuja baada ya kugundulika kuwepo kwa kura za maruhani katika baadhi ya maeneo.

Malawi, ilipiga kura wiki iliyopita ambapo matokeo ya awali yalionesha, Banda alikuwa nyuma ya Peter Mutharika ambaye ni ndugu wa aliyekua rais wa taifa hilo, marehemu Bingu Mutharika.

Imebainika kwamba kuna baadhi ya maeneo wapiga kura walikuwa wengi kuliko idadi sahihi ya wale waliojiandikisha.

Baadhi ya maeneo ambayo yamebainika kuwepo kwa kura zilizokuwa nyingi zaidi ya watu waliojiandikisha ni Machinga ambako waliojiandikisha walikuwa 38, 000 lakini waliopiga kura walifikia 184 000.

Eneo jingine ambalo limetokea tatizo hilo ni Mangochi ambalo wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 39, 000 lakini idadi ya kura imefikia 180, 000.

Mambo hayo yote yanaelezwa yamechangiwa na uchaguzi huo kuendeshwa kwa misingi ya rushwa, hujuma.

Maeneo ambayo yamechangiwa kupatikana kwa kura za maruhani ni yale ya wilayani ambayo yamefanikisha kuamua kiongozi atakayeongoza Malawi kwa miaka mitano ijayo.

Mkanganyiko huo wa kura umesababisha kulalamikiwa na vyama vya PP, MCP na UDF kuwa haukuwa wa haki na huru.

Tume ya uchaguzi ya nchini humo (MEC), juzi imetangaza kuwa leo itarudia kuhesabu kura zilizopigwa kwa kile ilichokiita kubainika kuwepo kwa mchezo mchafu katika matokeo ya awali.

Hata hivyo tayari Rais wa nchi hiyo Joyce Banda, ambaye matokeo ya awali yalionyesha ameachwa nyuma na wapinzani, ametangaza kufutwa kwa uchaguzi huo Licha ya kutangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo yake, Banda aliagiza kufanyika kwa uchaguzi mwingine ndani ya siku 90 huku akitangaza kutoshiriki kwenye kinyang'anyiro hicho.

Agizo hilo la Banda, lilipingwa na majaji na baadhi ya wananchi kila kona ya nchi hiyo kutokana na wengi kutafsiri kwamba hatua yake hiyo ina lengo la kujiondoa madarakani kwa heshima.

Kauli hiyo ilisababisha wengi kuhoji mamlaka iliyompatia uhalali wa kutoa maamuzi hayo ambayo hata hivyo Mahakama Kuu ya nchini humo ilimaliza mjadala huo kwa kuweka wazi kiongozi huyo hana mamlaka hayo kwasababu alikuwa mgombea kama walivyokuwa wengine.

Mahakama hiyo iliigiza Tume ya Uchaguzi wa nchi hiyo kuendelea na shughuli za kuhesabu matokeo ya urais na ubunge ziendelee kama ilivyopangwa.

Pia Mahakama imesema kuwa italitazama upya lalamiko la rais Banda la uchaguzi huo kufanyika kwa udanganyifu.

Katika matokeo ya awali yaliyokwisha tangazwa yanaonesha kwamba, rais Banda yuko katika nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikiangukia kwa Peter Mutharika ambaye ni ndugu wa aliyekua rais wa taifa hilo, marehemu Bingu Mutharika.

source Tanzania Daima

0 Comments:

Post a Comment