Happy Lazaro,Arusha
Shirika linajishughulisha na uhifadhi wa Tembo la WILD SURVIVORS waja na teknolojia ya kisasa ya utatuzi wa migogoro kati ya Tembo na jamii zinazopakana na hifadhi.
Hayo yamesemwa jijini Arusha leo na Afisa miradi ya jamii wa shirika hilo,Masalu John Masaka wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kongamano la 15 la kisayansi la TAWIRI linalofanyika jijini Arusha .
Amesema kuwa lengo la kushiriki kongamano hili ni kuwaambia watu kazi wanazofanya ili kufanikisha hizi kazi za utatuzi wa migogoro kati ya tembo na jamii zinazopakana na hifadhi
Amefafanua kuwa, lengo la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kuhakikisha kwamba jamii zinazopakana na hifadhi zinaishi kwa amani na Tembo kwa kutumia njia rafiki kama mizinga ya nyuki .
Aidha ametoa wito kwa jamii pamoja na wahifadhi kufanya kazi pamoja kwa kukutumia njia rafiki ili tuweze kuishi pamoja na tembo kwani idadi ya watu inapoongezeka na idadi wanyama inapoongezeka ardhi haiongeki ,hivyo tunahitajika kufanya kazi kwa pamoja wakiwemo jamii iliyoathiriwa wahifadhi pamoja na wanyamapori.
" Tunafanya kazi zaidi za kuhifadhi Tembo kwa namna ambayo tunatatua migogoro kati ya Tembo na wakulima wanaopakana na hifadhi ."amesema Masaka .
"Tumekuja hapa kwenye mkutano huu kwa ajili ya kuwaeleza watu shughuli ambazo tunazifanya kwa mfano tunatumia mizinga ya nyuki ambayo inatoa mazao kama asali ambayo inakuwa faida kwa vikundi vya akinamama katika vijiji ambavyo tunafanya kazi."amesama Masaka .
"Tumekuja pia kwenye huu mkutano kwa lengo la kueleza watu namna ambavyo tunakusanya data na tunatumia vifaa gani tunatumia kamera pamoja na teknolojia ya simu ambayo tunakuwa na application inayoitwa survey one two three tunatumia kukusanya data ."amesema .
Amefafanua kuwa tangu shirika lianzishwe wamepiga hatua kwani wameshaweka uzio wa mizinga ya nyuki zaidi ya kilometa 20 katika maeneo mbalimbali kwani wana uzio wa nyuki kilometa saba upande wa Ngorongoro vijiji vya wilaya ya Karatu na kilometa sita kwa upande wa serengeti na kilometa sita katika vijiji vya Rukwa katavi vijiji ambavyo vinapatikana na hifadhi ya Taifa Katavi .
"Tumeona mabadiliko yapo matukio ya Tembo kuingia mashambani na kula mazao ya wakulima yamepungua na tumeona katika vijiji ambavyo tumefanya navyo kazi mwanzoni ikiwemo Ngorongoro wakina mama wameanza kupata kipato kutokana na mazao ya nyuki ."amesema .
"Tunawafundisha na tunawapa mafunzo ya namna ya kuweka uzio wa mizinga ya nyuki namna ya kuvuna mazao ya nyuki na na namna ya kuchakata na kuwaunganisha na soko ."amefafanua Masaka .
"Kwa uchunguzi ambao tumefanya ni kuwa tembo anawaogopa nyuki hivyo anavyokaribia karibu na mzinga wa nyuki na anapousukuma ule waya ambayo umeunganisha mzinga mmoja hadi mwingine na nyuki anapotikiswa wakiwa na asali wale nyuki walinzi wanatoka nje kuangalia kitu ambacho kinataka kuchukua mazao yake ba wale nyuki wanapotoka nje wanatoa ile sauti na tembo akisikia anaamua kuondoka."ameongeza Masaka .


0 Comments:
Post a Comment