Na Mwandishi Wetu
WAZAZI wametakiwa kuwa makini na kujenga msingi mzuri wa maadili na elimu kwa watoto wao wa shule za awali.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi ya Aniny Nndumi, Martin Malera kwenye mahafali ya 22 ya darasa la awali katika shule hiyo iliyoko Kimara, Dar es Salaam.
Katika mahafali hayo, wanafunzi hao waliwashangaza wazazi wao kwa namna walivyoonesha uwezo mkubwa wa kuzungumza Kiingereza, kuimba, kucheza na burudani zingine zilizopamba shughuli hiyo.
Akizungumza katika mahafali hayo, Malera aliyekuwa mgeni rasmi, alipongeza wazazi wa wahitimu, kwa kupeleka watoto katika shule hiyo, kwani ni mahala sahihi kujenga msingi wa malezi ya watoto wao kiroho, kimaadili na kielimu.
“Hakuna anayejenga nyumba akaanza kujenga baa, tunaanza kujenga msingi imara, tunajenga hadi kwenye paa. Mlichofanya kwa watoto wenu kuwaleta hapa, ni kujenga msingi imara.
“Walichotuonesha hapa, sisi ni ushuhuda tosha wa namna walivyojengewa msingi imara wa maisha yao ya baadaye, kwa hiyo nawapongeza na hongereni sana wazazi,” alisema Malera.
Akijibu risala ya wahitimu, Malera alimsihi Mkurugenzi wa Shule, Humphrey Swai kutimiza ombi la vifaa vya kisasa vya michezo na kuwekewa kona za kujifunzia, ili kurahisisha welewa wa watoto.
Mkuu wa shule, Erasto Joseph alisema shule hiyo ilianza mwaka 2000 ikiwa na watoto saba, lakini sasa ina wanafunzi 97 , huku 37 kati yao, ndio wahitimu.
Alitoa ofa kwa wazazi watakaosajili watoto kuanzia jana, kwamba watasoma bure katika muda uliosalia hadi Januari mwakani.
“Lakini mzazi au mtu yoeote akifanikiwa kumshawishi mzazi alete au mjukuu wake au mtoto wa rafiki au jirani, atapata zawadi ya Sh 50,000,” alisema Joseph.
Kwa mujibu wake, wazazi ni muhimu kulipa ada mapema, ili kuondoa usumbufu kwa watoto na kuwezesha uendeshaji shule, ikiwamo kulipa mishahara ya walimu na watumishi wote wa shule kwa wakati.
Swai, alisema wanaendelea kufanya ukarabati mkubwa ili kuweka mazingira mazuri kwa watoto kusoma.
Alisema uongozi unaendelea kuboresha mazingira ya shule, kuwa na walimu wenye taaluma ya kutosha, watumishi wenye weledi wa kusimamia maadili na nidhamu, hivyo aliwahikikishia wazazi kuendelea kuleta watoto shuleni hapo, kwani ni mahali sahihi.




0 Comments:
Post a Comment