Dk Mpango: Tanzania Yakaribisha Uwekezaji wa PPP na Marekani



Na Mwandishi Wetu, New York

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango, ametoa mwito wa kuimarishwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ili kuvutia wawekezaji kutoka hapa.



Aidha, Dk Mpango amesema ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ni nguzo muhimu ya kufungua fursa kubwa za kiuchumi Tanzania.

Makamu wa Rais alisema hayo juzi nchini hapa katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).



Dk Mpango alisema PPP si tu muhimu katika kukusanya dola za Marekani bilioni 185 zinazohitajika nchini kwa miaka mitano ijayo, bali ni njia bora kuhakikisha ustawi wa pamoja kati ya Watanzania na wafanyabiashara wa Marekani unaongezeka.

“Sekta binafsi ni mshirika muhimu katika jitihada zetu za maendeleo,” alisisitiza, akibainisha kuwa Tanzania imefanya maboresho ya mfumo wa uwekezaji, ili kuunda mazingira rafiki zaidi kwa PPP, kuanzia nishati, usafirishaji, afya na sekta za kidijitali,” alisema.



Makamu wa Rais alibainisha fursa za PPP katika sekta za kipaumbele kuwa ni miundombinu, ambapo Tanzania ipo kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya kilometa 2,561, inayofadhiliwa kwa kiasi kikubwa kupitia PPP.

Alisema reli hiyo inatarajiwa kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda, yenye zaidi ya watumiaji milioni 300.


“Kiwanda kilichopo Tanzania kinaweza kuhudumia kirahisi Afrika Mashariki na Kati,” alisema Dk Mpango, akiongeza kuwa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZs) yanayounganishwa na bandari na kuendeshwa kwa nishati mbadala, yako tayari kwa uwekezaji wa pamoja, hivyo kutaka Wamarekani kuwekeza.

Makamu wa Rais alisema pia kuna madini ya grafiti, nikeli na lithiamu na Tanzania inatafuta washirika wa Marekani si tu katika uchimbaji, bali pia kuongeza thamani kupitia PPP kwenye usindikaji, uzalishaji wa betri na uendelezaji viwanda vya nishati safi.

Kuhusu uchumi wa kidijitali, alisema PPP na kampuni ya Visa ambayo tayari ina kituo cha ubunifu Dar es Salaam, unaweza kusaidia kupanua mifumo ya uvumbuzi.

Aidha, alisema kwenye sekta ya kilimo hadi sasa ni asilimia 24 pekee ya ardhi inayofaa kwa kilimo ndiyo inatumika,  hivyo Tanzania inakaribisha PPP katika kilimo cha kisasa chenye teknolojia sahihi.

Lakioni pia matumizi ya ndege zisizo na rubani, kinachoendeshwa na Akili Unde (AI) na minyororo ya thamani ya uchakataji mazao, ili kukidhi mahitaji ya chakula Afrika na duniani kwa ujumla.

Dk Mpango alisema Tanzania inakaribisha kampuni za dawa na vifaatiba kutoka Marekani, kuanzisha uzalishaji wa ndani kupitia PPP, hatua itakayopunguza utegemezi wa Afrika kwa dawa zinazoagizwa nje.

Makamu wa Rais alisema Serikali imefanya mageuzi na kuwa kitovu bora cha PPP, ambapo kwa sasa usajili wa biashara umepunguzwa kutoka siku 14 hadi saa 24, huku vibali vya uwekezaji sasa vikitoka ndani ya saa chache kupitia kituo cha huduma kwa wawekezaji.

Alisema Serikali pia inawekeza katika elimu na ukuzaji ujuzi, ili kuhakikisha miradi ya PPP ina wataalamu wa kutosha.

“Tanzania imeendelea kuwa na utulivu wa kisiasa kwa takriban miaka 60 na miundombinu inabadilika kwa kasi na kampuni zinapata faida za asilimia 20 hadi 30, hivyo ni wakati sahihi kwa kampuni za Marekani kuingia kupitia ushirikiano wa kimfumo,” alisema.

Dk Mpango alisema kwa kuwa Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA) iko mbioni kumalizika muda wake, kuhuishwa kwake kutakuwa ni mkakati wenye manufaa kwa Marekani na Afrika kwa ujumla.

Alihimiza wawekezaji wa Marekani kuchukua hatua haraka, akibainisha kuwa wakati wengine bado wanachambua, washindani kutoka kanda nyingine tayari wanachukua hatua.


0 Comments:

Post a Comment