Wakulima Wanufaika na Mikopo ya Riba Nafuu ya TIB

 


Wakulima na wawekezaji nchini wameendelea kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Serikali (TIB Development Bank), hususan kupitia Dirisha la Kilimo ambalo limekuwa chachu ya kuongeza thamani ya mazao na kuibua fursa za kibiashara.



Akizungumza leo, Agosti 24, 2025 katika banda la TIB lililopo pembezoni mwa Mkutano wa Tatu wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma jijini Arusha, Kaimu Meneja Mawasiliano ya Umma na Masoko wa TIB, Edward Kaguo, alisema kuwa benki hiyo ni ya kisera na ya serikali, ikifanya kazi tangu mwaka 1970.

“TIB ni benki ya kisera na kwa kuwa inamilikiwa na Serikali, tunatekeleza moja kwa moja vipaumbele vyote vinavyowekwa na Serikali. Tunatoa mikopo ya muda mrefu, wa kati na mfupi katika sekta za kimkakati ikiwemo kilimo, utalii, miundombinu, madini, nishati, maji, viwanda na wawekezaji wadogo na wa kati (SMEs),” alisema Kaguo.

Alibainisha kuwa Serikali imewekeza zaidi katika sekta ya kilimo kupitia TIB, ambapo ilitenga shilingi bilioni 40 kwa ajili ya Dirisha la Kilimo na hadi sasa limekua hadi kufikia thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 83.

“Kupitia dirisha hili, wakulima wanapata mikopo kwa riba ya kuanzia asilimia tano – riba ambayo ni rafiki na ya kipekee nchini. Pia tunakopesha taasisi za fedha kwa riba ya asilimia nne ili nao wawakopeshe wakulima kwa riba isiyozidi asilimia nane, hivyo kuhakikisha mkulima anakopeshwa kwa masharti nafuu kabisa,” alieleza.




 

Kwa upande wake, Meneja wa TIB Kanda ya Arusha, Samwel Marco Minja, alisema kuwa kanda hiyo inayohudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Singida imekuwa mstari wa mbele kusaidia sekta za kilimo, utalii, viwanda na miradi ya maji.

“Tumekuwa tukishirikiana na mamlaka za maji Tanga kuongeza upatikanaji wa huduma, kuunga mkono miradi ya viwanda hususan ya packaging hapa Arusha, na pia kuwezesha miradi ya hoteli katika maeneo ya hifadhi kama Serengeti na Ngorongoro. Pia, kupitia ushirikiano na benki za biashara kama Uchumi Commercial Bank ya Moshi, wakulima wamekuwa wakipata mikopo hii ya kilimo kwa riba nafuu,” alisema Minja.





Amesema TIB imekuwa mshirika wa karibu wa Taasisi ya TAHA katika miradi ya kilimo cha maua na mazao mengine ya kimkakati, huku wakihimiza wakulima waliothibitisha maeneo yao kisheria kupitia Wizara ya Ardhi kutembelea benki hiyo kupata mikopo.

Aidha, Kaguo aliongeza kuwa vikao kazi kama vilivyoendelea jijini Arusha vimekuwa msaada mkubwa kwa taasisi kama TIB, kwani vinawawezesha kupata mwongozo wa moja kwa moja kutoka kwa Serikali kuhusu vipaumbele vinavyopaswa kutekelezwa.



“Vikao hivi vinatupa dira. Wakuu wanapokubaliana na Serikali, sisi watendaji tunapewa maelekezo ya utekelezaji, na kama benki ya Serikali tumekuwa mstari wa mbele kuyatekeleza kwa ufanisi,” alisema Kaguo.


 

Kwa sasa, TIB imejipanga kupanua zaidi huduma zake kikanda kupitia ofisi zake za Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, na pia kwa kushirikiana na benki za kibiashara ili kuwafikia wakulima na wawekezaji wengi zaidi nchini.

0 Comments:

Post a Comment