Tanzania imeanza rasmi ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini katika eneo la Kizota, jijini Dodoma — hatua inayotajwa kuwa chachu ya mapinduzi ya sekta ya madini na kuifanya nchi kuwa kitovu cha huduma za kimaabara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Maabara hiyo inatajwa kuwa kubwa kuliko zote kwa aina yake katika ukanda huo, na inatarajiwa kutoa huduma za kitaalam kwa ufanisi, uharaka na viwango vya kimataifa kwa wachimbaji na wadau wa sekta ya madini nchini na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi leo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema ujenzi huo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendelea chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa mageuzi makubwa ya sekta ya madini na kwa kuandika historia ya ujenzi wa maabara hii ya kisasa, miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) mwaka 1925," alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa: "Leo tunaandika historia ya kuanza kwa ujenzi wa maabara kubwa ambayo itafungwa mitambo na vifaa vya kisasa katika kutoa huduma za kimaabara ndani na nje ya nchi. Huu ni ukombozi mkubwa kwa wadau wa sekta ya madini katika kupata taarifa sahihi za kimaabara kwa wakati na zenye ubora wa hali ya juu."
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, maabara hiyo inatarajiwa kuchochea ukuaji na maendeleo ya sekta ya madini kwa kuongeza tija, kupunguza gharama na kuongeza ushindani wa sekta hiyo kimataifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), Dkt. Notka Huruma Batenze, alisema kuwa maabara hiyo italeta mapinduzi ya kweli kwa wadau wa madini nchini.
"Maabara hii ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini italeta tija kubwa kwa wadau wa sekta ya madini na kurahisisha upatikanaji wa huduma hii muhimu kwa maendeleo ya sekta," alisema Dkt. Batenze.
Ujenzi wa maabara hiyo unatarajiwa kugharimu Shilingi bilioni 14.3 na kukamilika ndani ya kipindi cha siku 690.
Mara baada ya kukamilika, Tanzania inatarajiwa kuwa kitovu cha huduma za uchunguzi wa kimaabara kwa madini, sio tu kwa matumizi ya ndani bali pia kwa nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

0 Comments:
Post a Comment