Katika kuendeleza juhudi za kuikuza sekta ya utalii nchini Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TANAPA, Jenerali mstaafu George Waitara, ametoa wito kwa wawekezaji kuelekeza macho yao katika Hifadhi za Kusini, akisisitiza kuwa maeneo hayo yamejaliwa hazina kubwa ya vivutio vya kipekee ambavyo bado hayajatumika kikamilifu.
Akizungumza Julai 12, 2025, alipotembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Jenerali Waitara alieleza kuwa Hifadhi za Kusini zinahitaji uwekezaji mkubwa hususan katika huduma za malazi, miundombinu na bidhaa za utalii ili kuongeza mvuto kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
“Ukanda wa Kusini una hazina kubwa ya vivutio vya kipekee ambavyo vinaweza kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na utalii endapo vitawekewa nguvu ya uwekezaji na kutangazwa kikamilifu. Ni muda muafaka sasa kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kupitia TANAPA katika kuibua na kuendeleza maeneo hayo, ili kupanua wigo wa kitalii na kuongeza pato la Taifa kupitia sekta hiyo,” alisema.
Akaongeza kuwa uwekezaji umekuwa ukielekezwa zaidi katika hifadhi za Kaskazini kama Serengeti, Tarangire na Kilimanjaro, hali inayosababisha msongamano wa watalii katika maeneo hayo. Kwa mujibu wa Waitara:
“Kama ilivyozoeleka wawekezaji wengi wa sekta ya utalii wamewekeza sana upande wa Kaskazini katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Ni wakati sasa wa kugeukia Hifadhi za Kusini katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Katavi ili watalii wetu wagawanyike kwa ajili ya kupata vionjo na ladha tofauti ya utalii wa kitamaduni kwa makabila ya Wahehe, Wangoni, Wagongwe na makabila mengine ya Kusini, pia waonje mazingira mengine yenye vivutio tofauti.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TANAPA, baadhi ya hifadhi za kusini kama vile Ruaha, Kitulo, Katavi, Mikumi na Udzungwa, zimekuwa zikiibuka na tuzo mbalimbali kutokana na upekee wa vivutio vyake. Ruaha kwa mfano, ni hifadhi kubwa zaidi Tanzania na mojawapo ya hifadhi kubwa kabisa Afrika, huku ikiwa na idadi kubwa ya tembo, simba, na ndege adimu. Hifadhi ya Kitulo imepata umaarufu kutokana na mandhari ya maua ya asili, na kupewa jina la "Bustani ya Mungu" (Garden of God), ikichukuliwa kuwa moja ya maeneo bora ya fungate barani Afrika.
“Hifadhi za kusini kama Ruaha ilishinda tuzo ya kivutio bora cha kiutamaduni barani Afrika, na Kitulo ikinyakua tuzo ya eneo bora la fungate Afrika, hivyo sifa hizi na nyingine kedekede zinatarajia kuleta watalii wengi, ndio maana tunawasisitiza kuwekeza upande huo kwani wawekezaji hawatajutia fedha zao walizowekeza,” aliongeza Jenerali Waitara.
Kwa upande mwingine, mwitikio wa wananchi katika kujifunza kuhusu utalii na uhifadhi umetajwa kuongezeka, ambapo zaidi ya watu 6,000 walitembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho hayo hadi kufikia Julai 12, 2025.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka TANAPA, Neema Mollel, alisema kuwa taasisi hiyo imetumia maonesho hayo kama jukwaa la kutoa elimu kwa umma na kuwahamasisha wawekezaji kuingia katika sekta ya utalii.
“TANAPA imetumia fursa ya maonesho haya kama jukwaa la kutoa elimu kwa umma, kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa,” alisema Mollel.
Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yaliyoanza Juni 28 yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 13, 2025, yakibeba kaulimbiu isemayo “Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania.” Maonesho haya yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua fursa mpya za kibiashara na uwekezaji, huku sekta ya utalii ikiwa miongoni mwa maeneo yanayopigiwa chapuo kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Kwa muktadha huu, uwekezaji katika Hifadhi za Kusini si tu kwamba utaboresha miundombinu ya utalii, bali pia utasaidia kuleta usawa wa kimaendeleo baina ya Kanda ya Kaskazini na Kusini, sambamba na kutunza urithi wa asili wa Tanzania.




0 Comments:
Post a Comment