TWENDE ZETU KILELENI AWAMU YA TANO YAZINDULIWA RASMI

 

Na Gift Mingi, Moshi

Kampeni ya Twende Zetu Kileleni awamu ya tano imezinduliwa rasmi mkoani Kilimanjaro, ikilenga kuhamasisha utalii wa ndani na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya utalii.



Uzinduzi huo umefanywa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ambaye amesema kuwa kampeni hiyo imekuwa ikiandaliwa na kampuni ya Zara Adventures kwa kushirikiana na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).



“Kampuni hiyo imekuwa ikiratibu kampeni hii kwa mafanikio na kwa mwaka huu tukio litafanyika mwezi Desemba,” amesema Babu.



Ameongeza kuwa kampeni hiyo inaunga mkono jitihada za kutangaza utalii kupitia filamu ya The Royal Tour iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kupitia filamu hiyo, watalii wameongezeka tofauti na miaka mingine na kukuza pato la taifa kwa ujumla,” amesema Babu na kusisitiza kuwa:
“Kwa mkoa wa Kilimanjaro, hoteli zinajaa hivyo ipo haja ya kuendelea kujenga hoteli ili kukidhi idadi ya watalii.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Zara Adventures, Zainabu Ansell, amesema mwaka huu kampuni yake imeshinda tuzo ya kampuni bora ya utalii kitaifa kutokana na juhudi zinazoendelea kufanyika.

“Kwa mwaka huu tunatarajia kuwa na wapandaji mlima takribani 200, wakiwemo watalii kutoka nchi mbalimbali pamoja na waandishi wa habari,” amesema Zainabu.


0 Comments:

Post a Comment