ADO SHAIBU NA WENGINE DHIDI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


MAOMBI NA. 046/2020

HUKUMU KUHUSU UZINGATIAJI WA SHERIA NA FIDIA

6 MACHI 2026

UAMUZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU 



Arusha, tarehe 6 Machi 2026: Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (Mahakama) leo imetoa Hukumu katika kesi ya Ado Shaibu na Wengine dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


Bw Ado Shaibu, Bw Ezekiah Dibogo Wenje, Bw Omar Musa Makame, Bi Dorah Seronga Wangwe, Bw Enock Wegesa Suguta na Bw Kassim Ali Haji (hapa wanarejelewa kama ("Waleta Maombi") ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wanachama wa chama cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo). Waliwasilisha Maombi yao dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ("Mjibu Maombi") wakidai ukiukwaji wa haki zao za kiraia na kisiasa, kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 katika nchi ya Mjibu Maombi.


Kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha Itifaki ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kuhusu Kuanzishwa kwa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (“Itifaki”), kwanza Mahakama iliangalia endapo ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza Maombi hayo. Katika suala hili, Mjibu Maombi alipinga mamlaka halisi ya Mahakama, akisema kwamba mamlaka ya Mahakama yana kikomo na kwa hivyo haiwezi kuamua masuala ambayo yako chini ya mamlaka ya mahakama zake za kitaifa. Mahakama katika uamuzi wake ilitupilia mbali pingamizi hilo na kubaini kwamba ingawa mamlaka yake ya kisheria yanawekewe mipaka na Itifaki, ina uwezo wa kuamua maombi ambayo yanaibua madai ya ukiukaji wa haki zilizohakikishwa na Mkataba, Itifaki au hati zingine zozote za haki za binadamu zilizoidhinishwa na Mjibu Maombi. Kwa hivyo, kwa kuwa Waleta Maombi wametoa madai kuhsu ukiukaji wa haki za binadamu zinazolindwa na Mkataba na hati zingine za haki za binadamu, mamlaka halisi ya Mahakama yalitimizwa.


Ingawa vipengele vingine vya mamlaka ya Mahakama havikupingwa na Mjibu Maombi, Mahakama ilivichunguza kwa mujibu wa Kanuni zake. Katika suala hili, Mahakama ilibaini kuwa ilikuwa na mamlaka binafsi kwani, tarehe 29 Machi 2010, Mjibu Maombi iliweka Azimio kwa mujibu wa Kifungu cha 34(6) cha Itifaki. Azimio hili linaruhusu watu binafsi kuwasilisha maombi dhidi ya Mjibu Maombi kulingana na Kifungu cha 5(3) cha Itifaki. Mahakama ilisisitiza kwamba Mjibu Maombi kuondoa Azimio hilo mnamo tarehe 21 Novemba 2019 hakukuathiri Maombi haya, kwani Maombi haya yaliwasilishwa mbele ya Mahakama hii mnamo tarehe 20 Novemba 2020, wakati uondoaji wa Azimio ulianza kutekelezwa mnamo tarehe 22 Novemba 2020. 


Kuhusiana na mamlaka ya muda, Mahakama ilibaini kuwa ukiukaji mwingi unaodaiwa kufanywa ulitokea mnamo mwaka 2020, yaani, baada ya Mjibu Maombi kuridhia Itifaki. Aidha, madai ya ukiukaji kuhusu kifungu cha 41(7) cha Katiba ya Mjibu Maombi ya mwaka 1977 kuhusu kutoweza kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, yanaendelea kwa kuwa kifungu hicho bado kipo kwenye Katiba hadi sasa, na kwa hivyo, mamlaka ya muda ya Mahakama yalitimizwa. Mwisho, Mahakama iliona kwamba ilikuwa na mamlaka ya kieneo kwa kuwa ukiukaji unaodaiwa kufanywa ulitokea katika eneo la Mjibu Maombi ambaye ni mhusika wa Mkataba na Itifaki. Kwa hivyo Mahakama iliona kwamba ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

 

Kisha Mahakama, kwa mujibu wa Kifungu cha 56 cha Mkataba na Kanuni ya 50(2) ya Kanuni za Mahakama (hapa inarejelewa kama “Kanuni”), iliangalia endapo Maombi haya yalikubalika. Katika suala hili, Mjibu Maombi aliibua mapingamizi matatu kuhusu ukubalifu wa Maombi haya. Kwanza, Mjibu Maombi alisema kuwa Maombi haya yalitokana tu na habari zinazosambazwa na vyombo vya habari, na kwa hivyo hayakuzingatia Kanuni ya 50(2)(d) ya Kanuni za Mahakama. Katika uamuzi wake, Mahakama ilibaini kuwa Maombi hayo yalitokana na baadhi ya ripoti za vyombo vya habari lakini pia yalitokana nyaraka nyingine kama vile hati za kiapo. Kwa hivyo, Mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo na kuona kwamba Maombi haya yalizingatia Kanuni ya 50(2)(d) ya Kanuni za Mahakama.


Pili, Mjibu Maombi alisema kwamba Waleta Maombi waliwasilisha kesi yao mbele ya Mahakama, kabla ya wakati kwani walikuwa hawajakamilisha taratibu za ndani. Mahakama katika uamuzi wake ilibaini kwamba Waleta Maombi walikuwa hawajakamilisha taratibu za ndani kwani walikuwa wametoa tu taarifa za jumla zisizo na uthibitisho kuhusu kuwepo na hali ya hofu nchini ambayo iliwazuia kukamilisha taratibu za ndani. Hata hivyo, Mahakama ilibaini kwamba madai yanayohusiana na kukosekana kwa njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yalikubalika kwani hakukuwa na njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika mahakama za kitaifa za Mjibu Maombi.


Mwisho, Mjibu Maombi alipinga kwamba madai yanayohusiana na kukosekana kwa njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais hayakubaliki kwa sababu tayari yalikuwa yameamuliwa na Mahakama katika uamuzi wake kwenye kesi ya Jebra Kambole dhidi ya Tanzania. Katika uamuzi wake, Mahakama iliona kwamba ili kesi iamuliwe lazima kuwe na muunganiko wa masharti matatu: (i) utambulisho wa wahusika; (ii) utambulisho wa maombi au hali yake kuwa ya ziada, ya mfululizo au mbadala au endapo kesi hiyo inatokana na ombi lililotolewa katika kesi ya awali na (iii) kuwepo kwa uamuzi wa kwanza kuhusu uzingatiaji wa sheria. Katika suala hili, Mahakama ilibaini kuwa utambulisho wa wahusika haukuwa sawa kwani kesi ya Kambole iliwasilishwa na mtu binafsi kwa maslahi ya umma wakati kesi ya sasa iliwasilishwa na watu wanaodaiwa kuathiriwa na jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa. Kwa hivyo, Mahakama ilibaini kuwa ukiukaji unaodaiwa hapa haukuwa umetolewa uamuzi.


Kuhusiana na madai ya kukosekana kwa njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika mahakama za kitaifa za Mjibu Maombi ambayo Mahakama iliona kuwa yanakubalika, Mahakama ililazimika kuhakikisha kwamba masharti mengine ya ukubalifu yametimizwa kabla ya kuamua uzingatiaji wake wa sheria. Katika suala hili, Mahakama ilibaini kwamba Waleta Maombi walikuwa wametambuliwa wazi kwa majina, madai ya Waleta Maombi yalitaka kulinda haki zao zilizohakikishwa chini ya Mkataba na lugha iliyotumika katika Maombi haya haikuwa ya dharau au ya matusi kwa Mjibu Maombi katika kutimiza matakwa ya Kanuni ya 50(2)(a), (b) na (c) mtawaliwa. 


Kuhusiana na sharti la kuwasilisha Maombi ndani ya wakati unaofaa, Mahakama ilibainisha kuwa wakati unaopaswa kuzingatiwa ulikuwa muda kati ya kuweka Azimio, yaani, tarehe 29 Machi 2010 na tarehe ya kuwasilisha Maombi, tarehe 20 Novemba 2020, kipindi cha miaka 10, miezi sita na siku 22. Katika uamuzi wake, Mahakama ilibaini kuwa kwa kuwa ukiukaji huo unaendelea kwa sababu kfungu kinachopingwa bado kipoa katika Katiba ya Mjibu Maombi, kikomo cha muda wa kuwasilisha Maombi katika Mahakama hii kilikuwa hakijaanza. Kwa hivyo, Maombi haya yalizingatia Kanuni ya 50(2)(f) ya Kanuni za Mahakama. Mahakama pia ilibaini kuwa madai ya haki ya kupinga uchaguzi wa rais hayahusu suala ambalo tayari limetatuliwa kwa mujibu wa Mkataba, Sheria ya Katiba ya Umoja wa Afrika au Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa Kanuni ya 50(2)(g) ya Kanuni za Mahakama.


Kuhusu uzingatiaji wa sheria wa kesi hiyo, Waleta Maombi walidai kwamba hakukuwa na njia ya kupinga uchaguzi wa rais baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza mshindi na kwamba hali hii ilikiuka haki yao ya kusikilizwa kwa haki kwa mujibu wa Kifungu cha 7(1) cha Mkataba na wajibu wa Nchi Wanachama kuweka hatua ambazo zingezingatia Mkataba chini ya Kifungu chake cha 1. Mahakama katika uamuzi wake, kwa mujibu wa uamuzi wake awali, ilibaini kwamba kifungu cha 41(7) cha Katiba ya Mjibu Maombi, kwa kadiri inavyozuia mahakama kuhoji kuhusu ushindi wa mgombea wa urasi ambaye ametangazwa Tume ya Uchaguzi, kinakiuka Kifungu cha 1 na 7(1) cha Mkataba.


Baada ya Mahakama kubaini ukiukaji wa Kifungu cha 1 na 7(1) cha Mkataba, iliamuru Mjibu Maombi kuchukua hatua zote muhimu za kikatiba na kisheria, ndani ya mwaka mmoja, ili kuhakikisha kwamba kifungu cha 41(7) cha Katiba yake kinarekebishwa na kuzingatia masharti ya Mkataba.


Kila upande uliamriwa kubeba gharama zake. 


Maoni ya Pamoja ya Jaji Tchikaya na Jaji Anukam yameambatishwa kwenye hukumu hii kwa mujibu wa Kifungu cha 28(7) cha Itifaki na Kanuni ya 70(3) ya Kanuni ambazo walidai kwamba Mahakama ilipaswa kutenganisha kushughulikia ukiukaji wa haki unaodaiwa kufanywa unaohusisha ukatili wa kimwili na haki zinazodaiwa kukiukwa na sheria za uchaguzi.


Maelezo zaidi

Maelezo zaidi kuhusu kesi hii, ikiwa ni pamoja na hati kamili ya uamuzi wa Mahakama ya Afrika, yanaweza kupatikana kwenye tovuti kupitia: https://www.african-court.org/cpmt/details-case/046/2020 


Kwa maswali mengine yoyote, tafadhali wasiliana na Msajili kwa barua pepe registrar@african-court.org.


Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ni mahakama ya bara zima iliyoanzishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ili kuhakikisha haki za binadamu na watu barani Afrika zinalindwa. Mamlaka ya Kisheria ya Mahakama kuhusu kesi na mizozo yote iliyowasilishwa kwake kuhusu tafsiri na utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na chombo kingine chochote cha Haki za Binadamu kilichoidhinishwa na Nchi zinazohusika. Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea tovuti yetu www.african-court.org. 


0 Comments:

Post a Comment