"CCM HAIJAWAHI KUFELI" – JOHN TARIMO ACHUKUA FOMU YA UDIWANI MWIKA KISINI


Na Gift Mingi, Moshi

Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) John Tarimo ambaye pia ni mdau wa maendeleo katika kata ya Mwika Kisini, leo amekuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya udiwani katika kata hiyo iliyopo jimbo la Vunjo.



Tarimo alichukua fomu hiyo leo Juni 28, siku rasmi ya kuchukua fomu kwa watia nia wa nafasi za udiwani, ubunge, na uwakilishi kupitia CCM. 

Baada ya kuchukua fomu, hakuzungumza na vyombo vya habari, bali alielekea moja kwa moja nyumbani kwake, nyumba namba 758 A, kitongoji cha Kiruweni Kati, kijiji cha Kiruweni.

Akiwa nyumbani, Tarimo alisema kuwa kila kitu kinaendelea vizuri na kuwa mchakato umefuata taratibu zote za chama.

“Jambo hili limesainiwa na walio wengi wakitamani nifanikishe maendeleo hapa nyumbani, ndiyo maana nimekuja leo kutimiza adhima ya wananchi,” amesema Tarimo.

Tarimo hakufanya shamrashamra kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita, jambo ambalo limefuata maagizo ya chama kutoka makao makuu. 


Hata hivyo, baadhi ya wananchi walionekana kuwa na hamasa kubwa ya kumpokea kwa shangwe, japo walihimizwa kuzingatia kanuni.

“Tumetii hizi kanuni za chama, ila kiukweli tulihitaji maandamano na tarumbeta, ila kwa kuwa kanuni haziruhusu basi,” amesema Jackline Mmbando, kada wa CCM na mkazi wa Mwika Kisini.

Wakazi wa kata hiyo wameeleza matumaini yao kwa Tarimo wakiamini kuwa anaweza kuwa kiongozi atakayeleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya eneo hilo, hasa katika sekta ya miundombinu.


0 Comments:

Post a Comment