Sabaya Arejea Kisiasa kwa Kishindo Arumeru Magharibi: "Namwachia Mungu afanye kazi yake"





Joto la kisiasa katika Jimbo la Arumeru Magharibi limepanda kwa kasi, kufuatia kurejea kwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ambaye jana alijitokeza kuchukua fomu ya kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). 


Sabaya, anayefahamika kwa siasa zake zenye msimamo na ujasiri, ameibua hisia mbalimbali huku akitajwa kuleta mtikisiko mpya katika kinyang’anyiro hicho chenye ushindani mkubwa.



Sabaya alifika katika Ofisi za CCM Wilaya ya Arumeru majira ya saa 10 jioni akiwa ameongozana na mke wake, Jesca Thomas. 

Alipokelewa rasmi na Katibu wa CCM Wilaya ya Arumeru, Camila Kigosi, huku wanahabari wakimzonga kwa maswali .

Hata hivyo, aliepuka kuzungumza kwa undani na wanahabari kuhusu kurejea kwake kisiasa baada ya ukimya wa muda mrefu. 

Kauli yake fupi lakini yenye uzito iliwacha gumzo:
"Namwachia Mungu afanye kazi yake, mbarikiwe sana," alisema Sabaya, akiwa ameambatana na mkewe, na kuendelea kutembea huku akikwepa maswali ya ziada.

Wanahabari walipojaribu kumbana na maswali kuhusu wapi alikokuwa kipindi chote cha ukimya wake, Sabaya alishikilia msimamo wake na kurudia kauli hiyo hiyo:
"Namwachia Mungu afanye kazi yake, mbarikiwe sana."

Hata alipohojiwa juu ya tetesi kuwa alikuwa mgonjwa au hakuwa na mpango wa kugombea, alijibu tena kwa msimamo ule ule:
"Namwachia Mungu afanye kazi yake, mbarikiwe sana."

Historia ya Kisiasa ya Sabaya

Lengai Ole Sabaya si jina geni katika siasa za Tanzania. Alianza safari yake ya kisiasa mwaka 2015 aliposhinda nafasi ya udiwani katika Kata ya Sambasha jijini Arusha, wakati huo kukiwa na ushindani mkali dhidi ya CHADEMA. 


Mwaka mmoja baadaye, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha. Tarehe 28 Julai 2018, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli.


Hata hivyo, Mei 13, 2021, Sabaya aliondolewa katika nafasi hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan, kufuatia tuhuma mbalimbali zilizomkabili. Oktoba 15, 2021, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela. Baadaye aliachiwa huru baada ya kushinda rufaa na pia kukiri makosa katika kesi nyingine.

Sabaya aliibuka tena hadharani Februari 4, 2024, alipotokea katika Kanisa la Ebenezer Restoration Ministry for All Nations lililopo Moshono, Arusha, kutoa sadaka ya shukrani kwa kuachiwa kwake.

Washindani Wake

Mpaka kufikia leo, Julai 1, 2025, zaidi ya wagombea 20 tayari wamechukua fomu za kuwania ubunge kupitia CCM katika Jimbo la Arumeru Magharibi, ambapo wanawake watano wamejitokeza. Miongoni mwa wagombea waliokwisha chukua fomu ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Noah Lebris (Saputu), Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru Noel Severe, Elias Lukumay, Ezekia Mollel, Dkt. Johanes Lukumay, Henry Mejili, Lekoko Piceli, Luteni Kanali Mstaafu Joel Madia na John Tahaki.

Ujio wa Sabaya umeonekana kuwa pigo kwa baadhi ya wagombea, hasa kutokana na historia yake ndani ya chama, ushawishi mkubwa katika siasa za  Arusha na uwezo wake wa kujenga hoja.

Katika jimbo hilo lenye kata 27 na wapiga kura wa CCM wapatao 13,000, Sabaya anatambuliwa na baadhi ya makundi kuwa ni "mwanasiasa mchachari, asiyechoka, na msimamo mkali", sifa ambazo zinatajwa kumpa nafasi kubwa katika uteuzi wa chama.

Mtikisiko wa Kisiasa Kanda ya Kaskazini

Rejea ya Sabaya si tukio dogo. Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa kurejea kwake kunaweza kuamsha upya mvutano wa kisiasa Kanda ya Kaskazini, ambapo wanasiasa vijana kama Paul Makonda (anayeomba kuteuliwa katika Jimbo la Arusha) na Joshua Nassari (anayelenga Arumeru Mashariki) pia wameonesha nia ya kurudi kwenye ulingo wa siasa kupitia CCM.

Wengi wanaamini kuwa ikiwa atateuliwa, Sabaya anaweza kuwa mpinzani mwenye nguvu si tu kwa wagombea wa vyama pinzani, bali hata ndani ya chama chake mwenyewe kutokana na umaarufu na uzoefu wake katika siasa za kimkakati.

Kwa mara ya kwanza tangu kuachiwa kutoka gerezani, Sabaya ameonekana hadharani akiwa kwenye shughuli rasmi ya kisiasa. Ujio wake umeamsha hisia tofauti kwa wapiga kura, wanachama wa CCM na wachambuzi wa siasa.
Kama ambavyo yeye mwenyewe amesisitiza:
"Namwachia Mungu afanye kazi yake."


Kwa habari zaidi, endelea kufuatilia 


0 Comments:

Post a Comment