TUMETIMIZA MATAKWA YA ILANI YA CCM YA KUFIKISHA WATALII MILIONI TANO – Dkt Pindi Chana

 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana, amewapongeza watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa sekta ya utalii kwa kufanikisha lengo la kuvutia watalii milioni tano, kama lilivyoainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020.



Akizungumza katika uzinduzi wa siku maalum ya Ngorongoro (Ngorongoro Day) katika viwanja vya Sabasaba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya maonesho ya 49 ya biashara ya kimataifa, Dkt Chana alisema:

“Niwapongeze sana watendaji wenzangu wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa sekta ya utalii, kwani ilani ya CCM ilitutaka tufikishe watalii milioni tano na sasa tunatembea kifua mbele kwani idadi hiyo imetimia.”

Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa jumla ya watalii 5,360,247 walitembelea Tanzania. Kati ya hao, watalii wa kimataifa walikuwa 2,141,895 huku watalii wa ndani wakifikia 3,218,352. 


Kwa mujibu wa waziri, mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya serikali, taasisi binafsi na wananchi waliotambua umuhimu wa utalii kama kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa taifa.



Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya makubwa, Dkt Chana alisisitiza kuwa bado yapo malengo mengine yanayopaswa kufikiwa. Alitaja mojawapo kuwa ni kuongeza mapato yatokanayo na utalii hadi kufikia dola bilioni 6 ifikapo mwisho wa mwaka 2025, ambapo hadi sasa sekta hiyo imeingiza dola bilioni 3.9.

Katika hafla hiyo, Waziri Chana pia aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025. 



NCAA imekusanya shilingi bilioni 269.9 dhidi ya lengo la shilingi bilioni 230. Aidha, mamlaka hiyo imepokea jumla ya watalii 830,295 kuanzia Julai 2024 hadi Februari 2025, ambapo 509,610 walikuwa ni watalii wa kimataifa na 320,685 ni wa ndani.

Meneja wa huduma za utalii na masoko wa NCAA, Mariam Kobelo, alieleza kuwa maadhimisho ya siku ya Ngorongoro yana lengo la kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, katika kutangaza vivutio vya utalii na kuhamasisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea Tanzania.

“Kupitia siku hii, tunaleta hadharani historia, utajiri wa maliasili, na umuhimu wa eneo la Ngorongoro kwa uchumi wa taifa letu. Ni sehemu ya juhudi za kumuenzi rais wetu kwa jitihada zake kubwa katika kutangaza utalii duniani kote.”


 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru, alieleza kuwa bodi hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine chini ya wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano na ubunifu katika kutangaza utalii kwa njia za kisasa zaidi.

“Tutahakikisha kwamba idadi ya watalii inaendelea kuongezeka sambamba na mapato ya serikali kupitia sekta hii muhimu.”

Kwa ujumla, mafanikio haya yanaonesha mwelekeo chanya wa sekta ya utalii nchini, huku serikali ikitarajia kwamba kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu, masoko ya kimataifa, na huduma bora kwa watalii, malengo yaliyosalia ya Ilani ya CCM yatafikiwa kwa wakati.

0 Comments:

Post a Comment