“Nilivunjika Moyo Sana na Mazungumzo Yangu na Rais Putin” – Trump Atishia Vikwazo Vipya kwa Urusi

 


“Nilivunjika moyo sana na mazungumzo yangu na Rais Putin. Anataka kwenda mbali mno, kuendelea tu kuua watu, hiyo haikubaliki,” amesema Rais wa Marekani Donald Trump, akielezea hali ya kutoridhishwa na mwenendo wa Urusi katika vita vya Ukraine.

Trump alitoa kauli hiyo akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mazungumzo ya hivi karibuni aliyofanya kwa simu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Katika maelezo yake, Trump alifichua kuwa mazungumzo hayo hayakumridhisha na kwamba sasa anafikiria kuchukua hatua kali zaidi kwa kuweka vikwazo vipya dhidi ya Moscow.

“Nimekuwa mkali zaidi kwa Urusi kuliko nilivyo kwa Iran. Na kuliko nilivyo kwa nchi nyingine yoyote,” alisema Trump, akisisitiza kuwa licha ya ukosoaji kwamba analegeza msimamo kwa Moscow, ukweli ni tofauti.

Akiendelea kufafanua, Trump alisema bado anaheshimu uhusiano kati yake na Putin, lakini alionya kuwa uvumilivu wake una mipaka.

“Mpaka sasa tumeelewana vizuri kuhusu vikwazo, na anaelewa kwa nini vinaweza kuwekwa. Yeye ni mtaalamu,” alisema Trump, lakini akaongeza kwa msisitizo kuwa hali ya sasa imefikia kiwango kisichovumilika.

Trump, ambaye mara kadhaa amekuwa akikosolewa kwa kukosa msimamo mkali dhidi ya Urusi, sasa anaonekana kubadilisha mwelekeo hasa kutokana na kile alichokiita "urahisi wa Putin kuendeleza mauaji."

Kauli hii ya Trump imeibua mijadala mikali katika duru za kimataifa, hasa kwa kuzingatia kuwa Urusi inaendelea na mashambulizi yake nchini Ukraine huku jamii ya kimataifa ikishinikiza suluhu ya kidiplomasia.

Taarifa zaidi kuhusu hatua ambazo Marekani inaweza kuchukua bado hazijawekwa wazi, lakini Trump alisisitiza kuwa vikwazo viko mezani na anaweza kuvitangaza wakati wowote iwapo hali haitabadilika.

Kauli hii inaashiria mabadiliko ya kimkakati katika msimamo wa Marekani kuelekea Urusi, na inafuatia mfululizo wa matukio ya kijeshi na kidiplomasia yanayotikisa Ulaya Mashariki.

0 Comments:

Post a Comment