Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) inaendelea na mikakati ya kuboresha mazingira ya Kituo cha Kimondo cha Mbozi, kwa lengo la kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo na kukifanya kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa Serikali.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-razaq Badru, alipofanya ziara ya kikazi katika kituo hicho kilichopo mkoani Songwe.
Akiwa katika ziara hiyo, Kamishna Badru alizungumza na watumishi wa kituo hicho na kuwataka kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na moyo wa uzalendo ili kuhakikisha kituo hicho kinatumika ipasavyo kama kivutio cha utalii na kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.
“Serikali kupitia NCAA imefanya kazi kubwa ya kuboresha kituo hiki kwa kujenga jengo jipya la makumbusho ya kisasa pamoja na kuweka vioneshwa mbalimbali vinavyohusiana na historia, mila na tamaduni za makabila ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa uwekezaji huu unaleta matokeo chanya kwa taifa,” alisema Badru.
Aidha, alieleza kuwa NCAA imeweka mipango madhubuti ya kuendeleza hifadhi hiyo kwa kuweka miundombinu bora, huduma rafiki kwa wageni na kuongeza ubunifu katika utoaji wa elimu ya urithi wa utamaduni ili kuwavutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
“Tunataka eneo hili liwe kivutio cha kweli cha utalii wa kiutamaduni. Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa tunalinda na kuendeleza urithi huu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” aliongeza Badru.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Kimondo cha Mbozi ambaye pia ni Afisa Uhifadhi Mwandamizi, Andrew Lowasa, alieleza kuwa mafanikio ya awali ya kituo hicho yanadhihirika kupitia ongezeko la idadi ya wageni.
“Katika mwaka wa fedha 2024/2025, tumepokea jumla ya wageni 2,525 kutoka ndani na nje ya nchi. Hili ni ongezeko linaloonesha kuwa hatua zilizochukuliwa na NCAA zinaendelea kuzaa matunda,” alisema Lowasa.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za serikali katika kuliboresha eneo hilo na kulitangaza kupitia maonesho ya kihistoria na makumbusho ambayo yanavutia wageni wa rika na mataifa mbalimbali.
Ziara ya Kamishna Badru katika Kituo cha Kimondo cha Mbozi ni sehemu ya mpango wa NCAA wa kutembelea na kukagua vituo vya urithi wa utamaduni na mambo kale vinavyosimamiwa na Mamlaka hiyo nje ya Hifadhi ya Ngorongoro. Lengo ni kujionea utendaji kazi, changamoto zilizopo na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya hifadhi hizo.
Kupitia juhudi hizo, NCAA inalenga kuhakikisha kuwa maeneo ya kihistoria kama Kimondo cha Mbozi yanatumika kikamilifu kama sehemu ya kukuza utalii wa ndani, kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo husika, na kuchangia pato la taifa kupitia sekta ya utalii endelevu.




0 Comments:
Post a Comment