JANUARY MAKAMBA AITII CCM: ASEMA SI MGOMBEA WA URAIS,“SIHAMI CCM, NIKO NA NITAENDELEA KUWEPO”

 


Mbunge wa Jimbo la Bumbuli anayemaliza muda wake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), January Yusuph Makamba, amesema amepokea kwa utulivu na heshima maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM ya kutomteua tena kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu na mshirika wa maendeleo ndani ya chama hicho.

Makamba ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, Julai 31, 2025, ikiwa ni siku moja baada ya Kamati Kuu ya CCM kutangaza rasmi orodha ya majina ya wanachama walioteuliwa kugombea ubunge katika majimbo yote ya Tanzania Bara na Visiwani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

“SIJAKATWA, SIKUTEULIWA”

Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake kwa kushtukiza, Makamba alifafanua kuwa ndani ya CCM hakuna dhana ya "kukatwa", bali mchakato wa uteuzi unafuata misingi ya kupendekeza au kutopendekeza.

“Kwenye CCM dhana ya kukatwa haipo. Ni aidha umependekezwa au umeteuliwa. Kukatwa maana yake ni kwamba kuna nafasi ambayo unastahili kwa hiyo umekatwa. Wakati unapoomba nafasi hizi wote mnakuwa mpo sawa, hujastahili, kwa hiyo hakuna dhana ya kukatwa. Ni hukupendekezwa au haukuteuliwa. Sisi hatukuteuliwa,” alisema Makamba.

“NAITII KEFYA NA MAAMUZI YA CHAMA”

Makamba alisema amepokea kwa moyo mkunjufu uamuzi wa Kamati Kuu na kuwa anaendelea kuwa mwanachama na kiongozi mtiifu kwa misingi na maamuzi ya vikao vya chama hicho kikongwe.

“Ninaipokea na kuitii kwa moyo mmoja uamuzi wa Kamati Kuu. Mimi ni mwanachama na kiongozi mtiifu wa Chama Cha Mapinduzi. Chama kina taratibu zake, na wajibu wangu ni kutii maamuzi ya vikao vyake,” alisema Makamba.

Aliendelea kwa kueleza kuwa tayari amewasiliana na uongozi wa CCM wilayani Bumbuli kuwaarifu utayari wake wa kushirikiana nao kuhakikisha ushindi wa chama hicho katika uchaguzi ujao.

“MIMI SIO MGOMBEA WA URAIS”

Akijibu kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kuwa sababu ya yeye kutopitishwa ni tuhuma kuwa anataka kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamba alikanusha vikali madai hayo.

“Mimi si mgombea wa urais, wala sijawahi kutangaza nia hiyo. Hayo ni maneno yanayozunguka kwenye medani za siasa. Kwenye siasa changamoto kama hizi ni za kawaida, na mimi niko tayari kuzipokea kwa heshima na utulivu,” alisema.

“SIHAMI CCM, NIKO NA NITAENDELEA KUWEPO”

Makamba alitumia nafasi hiyo pia kukanusha uvumi kuwa ana mpango wa kuhama chama kutokana na hatua hiyo ya kutopitishwa.

“Niko CCM, na niko sana. Chama hiki ndicho kilichonilea, kimenipa nafasi za kuwatumikia wananchi na bado naamini katika misingi yake. Sio kila changamoto ni sababu ya mtu kuhamahama,” alisisitiza.

UTAALAMU NA SAFARI YA UONGOZI

January Makamba ni mmoja wa viongozi waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini na bungeni. Amewahi kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Waziri wa Nishati.

Alianza kutumikia wananchi wa Jimbo la Bumbuli mwaka 2010, ambapo alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge na tangu wakati huo, alihudumu kwa vipindi vitatu mfululizo.

Katika kipindi chake bungeni, Makamba alijijengea heshima kwa mtazamo wake wa kisasa kuhusu maendeleo, mazingira, na matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma.

MWANGAZO KATIKA KIVULI

Wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa Makamba anaweza kuwa mfano wa viongozi wanaokubali maamuzi ya chama kwa ustaarabu na kutoa nafasi kwa wengine, bila kushusha hadhi ya taasisi au kuanzisha mgogoro wa ndani.

“Ni nadra sana kuona mwanasiasa mwenye nafasi na uzoefu kama wake kukubali kwa utulivu kutopitishwa. Hili linaonyesha ukomavu wake wa kisiasa,” alisema mchambuzi mmoja wa siasa za ndani ya CCM aliyeko Dar es Salaam.

Kwa sasa, macho yanaelekezwa kwenye sura mpya itakayoiwakilisha Bumbuli, huku Makamba akiweka bayana kuwa bado ataendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama, ndani ya vikao vyake, na katika ujenzi wa taifa kupitia majukwaa mengine ya uongozi na huduma kwa umma.

0 Comments:

Post a Comment