Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua kampeni mpya ya kitaifa inayolenga kuhamasisha wateja wake kulipa madeni na kulinda miundombinu ya umeme, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma endelevu ya umeme nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TANESCO, Irene Gowelle, amesema kampeni hiyo yenye jina la “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie” imezinduliwa rasmi leo tarehe 19 Juni 2025, ikibeba kaulimbiu isemayo “Huduma Endelevu Huanza na Wewe.”
“Malengo ya kampeni hii ni kuwahamasisha wateja wa malipo ya baada kulipa madeni yao kwa hiyari kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria, na kutoa motisha kwa ulipaji wa wakati ikiwemo msamaha wa riba kwa wateja watakaolipa madeni yao kikamilifu,” amesema Gowelle.
Ameeleza kuwa kampeni hiyo pia itahusisha ukaguzi wa mita za LUKU kwa wateja wa malipo kabla, kwa lengo la kuhakikisha mita hizo zinafanya kazi ipasavyo na hazijafanyiwa udanganyifu na wateja wasio waaminifu.
“Tutahakikisha kuwa mita zote ziko katika hali nzuri na hazijachezewa. Zoezi hili ni muhimu kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya umeme na uadilifu katika mfumo wa usambazaji,” amesema.
Gowelle amesema kuwa TANESCO pia itaendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu ulinzi shirikishi wa miundombinu ya umeme, kwa kushirikiana na jamii na kuwajengea uelewa wa namna bora ya kulinda rasilimali za shirika hilo.
“Tunaendelea kuhimiza ulinzi wa miundombinu kwa kuwashirikisha wananchi. Tunataka jamii iwe sehemu ya suluhisho kwa kutoa taarifa na kulinda miundombinu inayowahudumia wao wenyewe,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wateja waliodaiwa na TANESCO kutoa ushirikiano kwa kulipa madeni yao kwa wakati ili kuzuia usumbufu wa huduma na kuepuka hatua za kisheria.
“Tunatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi wa umeme au uharibifu wa miundombinu kwa kushirikiana na vyombo vya dola. Hii itapunguza athari zinazoweza kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme na kuzuia hasara kwa shirika,” amesisitiza Gowelle.
Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za TANESCO kuhakikisha huduma ya umeme nchini inakuwa ya kuaminika, salama, na endelevu .


0 Comments:
Post a Comment