Rais Samia Azindua Daraja Refu Zaidi Afrika Mashariki: "Ni Ushindi kwa Watanzania






“Ndugu wananchi, miongoni mwa vitu nilivyoahidi nilipokabidhiwa dhamana ya kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kukamilisha miradi ya kimkakati ukiwemo mradi huu wa Kigongo-Busisi,” alisema Rais Samia katika hafla hiyo.



Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi ya kilomita 1.66 limegharimu serikali ya Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 718, sawa na takribani dola za Kimarekani milioni 300. 



Kwa mujibu wa Serikali, daraja hilo litatatua moja ya kero kubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa waliokuwa wakitegemea kivuko kuvuka eneo hilo la ziwa Victoria.



Rais Samia amesema kukamilika kwa daraja hilo ni "ushindi kwa Watanzania wote" na kielelezo cha dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuendeleza miradi ya kimkakati.



“Kukamilika kwa ujenzi wa Daraja hili ni ushindi kwa Watanzania wote na kunazidi kuifungua nchi yetu,” alisisitiza Rais Samia.



Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema kuwa mradi huo umeonesha uwezo wa Watanzania kufanya maamuzi ya kimaendeleo bila kusubiri mataifa ya nje.



“Daraja hili ni kielelezo kikubwa cha uwezo wetu kama taifa wa kufanya maamuzi, wa kufanya maendeleo ya kwetu sisi wenyewe. Kanda ya Ziwa inakwenda kuchechemka katika uchumi wa kisasa ambao utaleta ajira kwa vijana,” alisema Ulega.


Mradi huo umetekelezwa na wakandarasi wawili wa China: **China Civil Engineering Construction Corporation** na **China Railway 15 Bureau Group Corporation**.


Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Ujenzi, daraja hili linatarajiwa kutumiwa na magari takribani 800 na watu zaidi ya 13,000 kwa siku, huku likipunguza muda wa kuvuka kutoka saa mbili hadi sita kwa njia ya kivuko hadi chini ya dakika 10.


Wakazi wa mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na Kigoma – pamoja na nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – wameeleza furaha yao kuhusu mradi huu.


“Miaka sitini na nne ya kadhia, vilio, na manung’uniko juu ya kero ya usafiri wa majini katika ziwa Victoria kupitia eneo la Kigongo-Ferry hatimaye leo imekwisha. Ni furaha,” alisema mmoja wa wakazi waliokuwa kwenye hafla hiyo ya uzinduzi.


Kwa upande wa kitaalamu, wachumi na wanasaikolojia wametoa tathmini chanya juu ya athari za daraja hilo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Dr. Francis Nyoni, mchumi na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) amesema:

“Daraja hili linaweza kuimarisha pia biashara na ushirikiano wa kikanda wa eneo la Kanda ya Ziwa na nchi jirani.”


Aidha, wataalam wa saikolojia walieleza kuwa matumizi ya vivuko yalisababisha msongo wa mawazo, sonona na hata vifo kwa baadhi ya watu waliokuwa wakilazimika kutumia njia hiyo ya zamani.


Ujenzi wa daraja hilo ulizinduliwa rasmi mwaka 2019 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli, ambaye kwa heshima yake daraja hilo limepewa jina lake.


Kwa sasa, daraja hilo si tu litaimarisha usafirishaji na biashara baina ya mikoa ya Tanzania bali pia linafungua fursa mpya za kiuchumi kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.



0 Comments:

Post a Comment