Tukio la kusikitisha limetokea katika shule ya sekondari ya wasichana Tabora (Tabora Girls) mkoani Tabora, baada ya mwanafunzi wa kike kujifungua mtoto akiwa chooni shuleni hapo. Tukio hili limeibua maswali mazito juu ya ufuatiliaji wa afya, ustawi na malezi ya wanafunzi katika shule hiyo maarufu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, mwanafunzi huyo aliripoti kuumwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete, ambako vipimo vilibainisha kuwa alikuwa amezaa mtoto. Taarifa hiyo iliwashangaza viongozi wa shule na serikali ya mkoa kwani hakuna mwalimu wala kiongozi yeyote wa shule aliyebaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mjamzito hadi kufikia hatua ya kujifungua.
“Hili linasikitisha sana, vitendo vya wanafunzi kujihusisha na ngono wakiwa shuleni vimekuwa vikipigwa marufuku mara kwa mara, wazazi tunapaswa kushirikiana na walimu kukemea tabia hii,” alisema Dkt. Mboya.
Tukio hilo lilimlazimu Mkuu wa Mkoa Paul Matiko Chacha kutembelea shule hiyo kwa ziara ya kushtukiza, ambako alitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa kijana aliyempa ujauzito mwanafunzi huyo anasakwa haraka na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Walimu waliokaa hapa zaidi ya miaka 10 wabadilishwe vituo vya kazi. Wamezoea mazingira, hawafuatii nidhamu wala mienendo ya wanafunzi. Haiingii akilini mwalimu wa darasa kushindwa kujua hali ya mwanafunzi wake, hasa wa kike,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kusikitishwa na uzembe uliofanywa na walimu pamoja na daktari aliyemfanyia vipimo mwanafunzi huyo awali bila kubaini ujauzito huo. Alisisitiza kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu dhidi ya wote waliohusika na uzembe huo.
Uchunguzi uliofanywa na timu maalum ya mkoa umebaini kuwa hali ya utendaji shuleni hapo imeathiriwa na walimu kukaa kwa muda mrefu bila uhamisho, hali inayochochea mazoea, kudhoofisha maadili ya kazi na kuathiri ufuatiliaji wa mwenendo wa wanafunzi.
HAKI ZA MSINGI ZA MTOTO WA KIKE: MAZINGIRA YA SHULE SALAMA NI WAJIBU WA JAMII
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989, ambao Tanzania imeridhia, kila mtoto ana haki ya kuishi, kupata elimu, huduma za afya, na kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote. Ibara ya 19 ya mkataba huu inazitaka serikali kuchukua hatua zote zinazowezekana kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za ukatili, madhara ya kimwili au kiakili, unyanyasaji au kutendewa vibaya.
Kadhalika, Azimio la Jomtien (1990) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa lengo la 4 (elimu bora) na lengo la 5 (usawa wa kijinsia), yanasisitiza umuhimu wa kumpatia mtoto wa kike elimu bila vikwazo ikiwemo ndoa za utotoni, mimba za shule, na ubaguzi wa kijinsia.
Kwa tukio kama hili kutokea ndani ya taasisi ya elimu ya serikali, ni kiashiria cha kushindwa kwa mifumo ya uangalizi wa watoto mashuleni. Ni dhahiri kuwa shule nyingi bado hazina mifumo madhubuti ya kusaidia na kufuatilia afya ya uzazi ya wanafunzi wa kike, pamoja na kutoweka wazi kwa huduma za ushauri nasaha na elimu ya afya ya uzazi.
Tukio hili la Tabora linapaswa kuwa chachu ya mabadiliko ya kina katika mfumo wa malezi na ufuatiliaji wa wanafunzi mashuleni. Serikali, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kwa dhati kuhakikisha mtoto wa kike analindwa, anapata elimu bora na anakua katika mazingira salama na yenye kumjenga. Msingi wa taifa lolote lenye maendeleo ni elimu — na elimu ya mtoto wa kike ni kichocheo cha ustawi wa jamii nzima.

0 Comments:
Post a Comment